Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. HUSNA J. SEKIBOBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia mchana wa leo. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutubariki sote kupata nafasi ya kuongea siku hii ya leo. Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa bajeti nzuri sana ambayo imewasilishwa kwetu na Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwigulu bajeti ambayo umewasilisha kwetu, imeleta matumaini makubwa na tunaamini katika mwaka huu wa fedha, kuelekea hata 2025 mambo ya Chama cha Mapinduzi yatakuwa barabara, kwa nini? Kwa sababu bajeti imejielekeza zaidi katika kutatua kero na changamoto za wananchi, kwa nini? Kwa sababu bajeti ambayo umewasilisha inakwenda kupunguza mzigo wa maisha kwa akina mama masikini waliokuwa wanasomesha watoto wao kwenye elimu ya kati kwa gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aliwahi kuishi Mtume Mohammad S.A.W katika maisha yake aliyowahi kuishi zama hizo na maswahaba wenzake. Maswahaba wakawa wanamuuliza, walikuwa wakimuona kila muda anatembea na tasbihi anamuomba Mwenyezi Mungu maghfilla amsamehe, lakini yeye tunaamini katika sisi waislamu ndio kiongozi ambaye ni mwema zaidi katika sisi wanadamu wa kiislamu. Kwamba ni kiongozi wetu katika dini. Wao waliamini ni katika yule ambaye hana makosa, hana dhambi, ni mtu mwema mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini muda wote alitembea na tasbihi na kuomba maghilla Eh! Mwenyezi Mungu nisamehe. Wakamuhoji wewe Mtume wa Mwenyezi Mungu tunajua wewe unaswali unafunga, unafanya sadaka unafanya kila jema ambalo Mwenyezi Mungu ameamrisha lakini mbona muda wote wewe astaghfirullah inakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtume Mohammad S.A.W akawajibu maswahaba kwamba, bora ni yule anayemjua na kumwabudu Mwenyezi Mungu, bora siyo huyo unayemuona kwamba wewe ni kiongozi wetu lakini yule anayemuogopa mwenyezi Mungu ndio bora. Lakini akasema Mungu tunaemuabudu anapenda kutajwa sana, anapenda kuimbwa, kuombwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie tumpe sifa anayostahili Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yeye hana sifa ya Mungu kwamba anapenda kusemwa sana, lakini yeye anastahili kusemwa sana kwa nini? Kwa sababu ya yale mema mazuri ambayo anayafanya katika Taifa letu. Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba Waziri wa Fedha, na hapa ninukuu maelezo aliyokuwa ametangulia kusema Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, amezungumza vizuri sana, ame-narrate vizuri kazi kubwa ambayo inafanyika kwenye Wizara ya fedha. Lakini nataka niseme wewe ni katika watu pia ambao wanastahili kusemwa vizuri, siyo kwa sababu unapenda kusemwa lakini unastahili kwa yale mazuri ambayo unayoedelea kuyafanya katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimesema hapo mwanzo Mungu alisema yeye anapenda sana kuombwa na hivyo hata viongozi wetu wa kidunia msichoke, mpende kuombwa na mimi nakuja sasa kwenye ombi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi juzi Serikali imefanya allocation ya wanafunzi kwenda kidato cha tano katika mashule yetu. Jambo la kusikitisha kweli kweli wapo wanafunzi wenye ufaulu mzuri sana division two, wamekosa nafasi za kwenda kusoma boarding wamekosa nafasi ya kwenda kidato cha tano hata day. Nina mfano wa wanafunzi ambao nimeletewa, lakini nina mwanafunzi hapa ana division two ya point 21 ana C ya Chemistry, ana C ya Biology, ana C ya masomo mengi na combination zaidi ya mbili zime – balance, amekosa shule. Nimefanya consultation kwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, Nimezungumza na Naibu Waziri wa Elimu, nimeongea na Naibu Katibu Mkuu - TAMISEMI maelezo ninayopewa hakuna nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kosa lake yeye ni nini? Kufaulu kupata division two ya point 21 ndiyo kosa lake? Kosa lake ni nini mwanafunzi wa namna hii? Tunapotaka kutengeneza nchi ambayo ina elimu tutakayotaka kuifanya iwe chachu ya kuchachuza uchumi wa nchi hii, lazima tuheshimu maono maombi na fikra za watoto wanazoziweka kwenye malengo yao ya kupata elimu. Mtoto amefaulu vizuri amekosa nafasi ya kwenda shule, je, kosa la kwake ni lipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikizingatiwa mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan anatoa elimu bure kwa kidato cha tano na cha sita. Huyu mtoto wa masikini mama yake anachoma vitumbua, anauza magimbi mtaani, amekosa nafasi ya kupeleka mwanae shule. Mwanae aliyefaulu kwa division two, tunamuweka katika kundi gani? Ninaiomba sana Serikali itoe maelekezo mahsusi kwa watoto ambao wamefaulu vizuri, watoto ambao wanastahili kwenda kidato cha tano kwa mwaka huu watafutiwe nafasi waende, kwa sababu ukimpeleka mtoto huyo kwenye chuo cha kati, siyo lengo lake na nina mfano wa mtoto mwingine ambae amepangiwa Chuo cha Uhasibu Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua umewasha mic lakini nirihusu nimalizie. Mtoto amepangiwa Chuo cha Uhasinu Arusha ana F ya hesabu, hajawahi kusoma masomo ya biashara, alifaulu masomo ya arts na masomo ya sayansi. Je, unampeleka kwenye accounts, kwenye chuo cha biashara unategemea akafanye muujiza gani? Je, ule mtaala mpya tunaopigia chapuo humu ndani kwamba tuende kwenye mtaala mpya wa elimu. Je, kama tutawapeleka watoto kwa mtindo huu, amesoma amasomo haya, interest yake ni kusoma kitu hiki wewe umempeleka kitu kingine tofauti. Tunategemea nini kwenye Taifa hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema ni vyema tukaheshimu maono na maombi ya wanafunzi, kwa sababu kila wanavyomaliza shule huwa wanajaza fomu kipaumbele chake ni kwenda wapi, anapojaza anataka kwenda kidato cha tano. Mtoto apelekwe akasome ili tuweze kuendeleza vipaji vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.