Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu alienijaalia uzima na afya leo kusimama hapa kuweza kuchangia kwenye hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi ya mwanzo kabisa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyosimamia utekelezaji kwa umahiri, uhodari, uadilifu na weledi. Nchi inakwenda vyema na imetulia na ninaomba kwa kupitia hadhara hii niwalaani sana wale ambao wanabeza juhudi zake na ambao wanataka kuleta utengano katika nchi yetu hii Tanzania ambayo ilikuwa imara. Hawa watu nawaombea Mungu walegee sehemu zote na wapotee kabisa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumuunge mkono Mama yetu naomba sana hawa watu wanaofanya ufukunyuku wa kuleta maneno kubeza jitihada za Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan walegee sehemu zote na wapotee kabisa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu amefanya mambo mengi katika nyanja mbalimbali na tunayaona. Amejikita vizuri kwenye miradi ya kimkakati na kwenye masuala ya kiuchumi na kabla sijaendelea mbele baada ya kutoa pongezi nyingi kwa Rais, nampongeza sana Dkt. Mwigulu Nchemba na timu yake. Dkt. Mwigulu wewe ni Mchumi mahiri, ni mchumi thabiti, ni mchumi hodari wewe ni mchumi mchuma. Mwigulu ni mchumi mchuma. Kazi zako unazofanya kumsaidia Mheshimiwa Rais ni kubwa sana na zinaonekana na mara hii umethubutu kuleta bajeti hii ya karibu trilioni 44.1 ambayo imekuwa ni bajeti elekezi, inayohusisha zaidi uzalishaji na kukuza uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii mimi nataka nijikite kwanza kwenye sehemu ya kilimo. Bajeti ya kilimo imeweza kutoka kwenye 294 mwaka wa fedha 2021 mpaka 970.0 mwaka huu wa fedha. Hizi ni fedha nyingi sana zinazoweza kuleta mageuzi makubwa katika sekta hii. Kwa kuwa, uchumi wa nchi unategemea sana kilimo, basi ningependa kutoa nafasi hii kujielekeza zaidi katika kilimo hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kilimo kinchukua nafasi kubwa, kilimo ni biashara, kinategemewa na wengi na kinaweza kuondoa Taifa letu hili kutoka sehemu hii kuipeleka sehemu kubwa zaidi. Nasisitiza kwamba iko haja ya kutilia mkazo zaidi kilimo hai, kwa kuwa kinaweza kuongeza ajira hasa kwa vijana. Mfano kuwapa nafasi ya kutengeneza viuatilifu vinavyotokana na mimea asili ambayo tunayo kwa wingi, kuanzisha kuliko kutumia kemikali za kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana na wakulima wataweza kutengeneza mbolea hai, viuatilifu hai, ikiwa ni sehemu ya kutengeneza ajira kwa vijana. Pia sehemu ya kupunguza gharama kwa Serikali kwa kuagiza kemikali kutoka kwenye makampuni ya nje. Nashauri Serikali waone fursa ya kuongeza kipato cha uchumi wa nchi hii kwa kupitia kilimo hai. Kidogo kidogo tunapendekeza Serikali ipange na iipe kipaumbele kilimo hai kama yanavyofanya mataifa mengine. Kilimo kina uwezo wa kuchangia fedha nyingi na hivyo kubadili hali za wakulima. Serikali Kuu inaweza kuchangia wakulima kwa kuweka kabisa bajeti maalum kuchangia wakulima kuondokana na kilimo cha kemikali. Mfano, USA inatenga bajeti maalum kwa ajili ya kilimo hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ni kupanua na kuongeza uzalishaji wa mbegu asili za mazao ambayo yanaonekana kupotea. Serikali ijikite kusimamia uzalishaji wa mazo kwa blocks, siyo kila mahali mtu analima, mwenye korosho nchi nzima, leo umeambiwa alizeti itapanda bei unalima, kesho alizeti inaanguka bei. Kwa hivyo, Serikali ijikite vizuri kusimamia mambo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ambalo nataka kulisimamia kwa muda wa haraka ni kwamba Serikali naipongeza sana kwa hatua zake za kuondoa ada ya elimu kutoka darasa la kwanza hadi form six na kwa sekta hii kwa kutambua jambo hili na umuhimu wa vijana hawa kupata elimu bila kikwazo sasa hapa naomba maua mama apewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa shilingi trilioni 1.44 kwa wanafunzi wa elimu ya juu, hii ni kujenga base nzuri ya kutengeneza wataalam ambao watakuja kusaidia nchi yetu kuipeleka mbele. Vilevile ni kuondoa ada, jambo zuri jingine la kuondoa ada vyuo vya ufundi. Hili jambo tunalipongeza sana, lakini tunaomba ada hii iondolewe kwa vyuo vyote vinavyofanya study hii ya kiufundi isiwe kwa vile ambavyo Serikali peke yake imeweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine nataka kuiomba Serikali ifikirie ni kupunguza tozo kwenye saruji ya kujengea, kwa kuwa hapa wananchi wa kipato cha chini wengi sasa hivi wamehamasika kujenga nyumba bora ambazo zinatumia cement, sasa kuwaongezea hii inakuwa kuwakwamisha. Kwa hivyo Serikali itafute tax base nyingine ya kuweza kupata hii fidia ili bei ya saruji isipande.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kusema kwamba kodi ni lazima kwa sababu kodi inaendesha nchi yetu, lakini tujitahidi tuweze kulipa kodi kama inavyotarajiwa lakini ulipaji na uhamasishaji kwa mamlaka uwe wa kirafiki zaidi, siyo kuendeshana mbio mpaka tena Waziri Mkuu aende Kariakoo akaeleze, akatulize hali. Jambo lile halipendezi sana. Kwa mamlaka ya kodi ijipange vizuri kuwa na lugha rahisi na kuwawezesha watu kulipa kodi kama inavyotarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kuomba mkono hoja. (Makofi)