Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Salim Alaudin Hasham

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge hii Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kufika hapa leo nikiwa hai, salama salmini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, na wasaidizi wake pamoja na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Imeweza kusimamia vyema kabisa na tunaona mambo yakiwa yanakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitachangia katika sehemu mbili tatu, lakini nianze kwenye upande wa afya. Tumeona ambavyo bajeti imeongezeka kwenye Wizara ya Afya, lakini tumeona jinsi ambavyo Serikali yetu imeweza kuongeza vituo vya afya, hospitali pamoja na zahanati kwa wingi sana. Hatuna budi kupongeza hilo, hatuna budi pia kuchangia au kutoa mawazo yetu kwenye sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli tuna vituo vya afya vingi sana, pia tuna zahanati nyingi pamoja na hospitali. Lakini tuseme ukweli, huduma za afya bado hazijatengamaa, hazijawa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mbunge atakayekuwa anachangia humu ndani atakuwa anajua na atakuwa anajua changamoto ya jimboni kwake. Kikubwa zaidi watumishi wa afya kwenye hospitali zetu au kwenye zahanati zetu bado ni hafifu, japo Serikali imeajiri lakini bado. Ni lazima Serikali itupe jicho la tatu kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia dawa bado ni changamoto, wananchi wetu tunawahamasisha wakate bima za afya lakini dawa bado ni changamoto. Lakini vifaa tiba bado ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nikumbushe tena, ni mara yangu ya pili nachangia kwenye Bunge hili, niliwahi kusema Jimbo langu la Ulanga kuna changamoto kubwa ya afya kwa sababu hospitali ya wilaya imekuwa ndogo, lakini pia ongezeko la watu limekuwa ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kupata wawekezaji wengi kwenye Jimbo la Ulanga. Leo tutashindwa kuhudumia kwenye sekta ya afya, waende kwenye wilaya nyingine au waende mkoani kwenda kutibiwa, tutaonekana kwamba sisi pia hatuko serious. Kwa hiyo, naomba mlichukue hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana baada ya Bunge hili kuisha, ningependa sana Waziri wa afya aje jimboni ili aje kujionea haya ambayo nazungumza. Leo ni mara ya pili au ya tatu nazungumza hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Madini; kuna maamuzi yalitoka ya kuhamishia biashara ya tanzanite kwenda kufanyika Mererani. Niseme ukweli kabisa maamuzi yale hayakuwa sahihi, na mtu mzima akivuliwa nguo huchutama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ruhusuni biashara ya tanzanite ifanye Watanzania wale mazao ya nchi yao. Maamuzi yale yalikuwa yanakwenda kuwanufaisha watu wachache sana, na wengi wao siyo Watanzania. Leo hii unakwenda kuacha biashara ikafanyike sehemu moja wanufaike watu wachache na wakati sekta hii imeajiri zaidi ya watu milioni sita kwenye nchi nzima. Iruhusuni biashara ya tanzanite ifanyike kwa uhuru ili watu wale matunda ya nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nichangia kwenye upande wa leseni zetu za brokers; kama ambavyo nimesema, nchi hii imewaajiri watu zaidi ya milioni sita kwenye sekta ya madini, lakini leo hii ukienda kwenye upande wa ma-broker, tunajua ni wale watu wa kati ambao huwa hawana mitaji – wameweka leseni ni dola 100, watu wale hawawezi, hawana uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufanye tu mahesabu kama Wahindi. Mhindi anaweka faida ya shilingi 100 anauza bidhaa zake 200 kwa siku, sisi tunalazimisha hapa tunaweka faida ya shilingi 300 unauza bidhaa 10 kwa siku. Ni mahesabu madogo hayahitaji hata degree. Punguzeni bei ya leseni watu wakate leseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoka kwenye jimbo ambalo yanatoka madini. Unakuta wenye leseni kubwa wako 60, halafu ma-broker ambao ni wengi zaidi, wako chini ya 50. Maana yake ni kwamba anashindwa ku-afford kukata leseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi unarudi upande wa TRA na wenyewe wanawakadiria kodi zaidi ya 400,000, 500,000 kwa mwaka; watu hawawezi kufanya biashara. Ukiwaangalia hata kula yao ya chakula cha mchana inakuwa ni ngumu. Kwa hiyo, nafikiri kama Mheshimiwa Waziri angekuwa ananisikia, angeweza kuwasiliana na Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba TRA wanaweka viwango ambavyo wananchi wale wanaweza ku-afford kufanya vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leseni zetu kutoka kwenye dola 100, wekeni hata dola 50, hata dola 30, watu wengi watakata leseni na tutapata faida, lengo ni kukusanya mapato. Ukikatisha watu wengi zaidi utapata hela, ukikatisha watu wachache utapata hela kidogo. Kwa hiyo, ni hesabu ambayo haihitaji degree. Ni watu tu kujipanga na kuweza kufanya mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninapenda kuchangia kwenye Wizara ya Ardhi. Kwenye mijadala hapa Wabunge wamepiga kelele sana kuhusu migogoro ya ardhi, naamini Serikali imechukua na inakwenda kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto kwenye upande wa uthamini. Ni kweli Mheshimiwa Rais kisheria anayo haki ya kuchukua ardhi ya mtu yeyote sehemu yoyote kwa manufaa ya Umma, kwa ajili ya maendelezo ya Umma. Lakini kuna taratibu ambazo zimewekwa juu ya ulipaji fidia za wale watu ambao wanataka kuhamishwa kwa ajili ya maendeleo ya Umma kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria inasema kwamba ukiwa umekwenda kufanya fidia, umemaliza kufanya fidia kwa wananchi, inatakiwa kulipwa ndani ya miezi sita. Baada ya miezi sita valuation inakuwa ime-expire. Sasa ikisha-expire maana yake ni kwamba unatakiwa wewe umlipe fidia ya usumbufu yule mwananchi, yule mwananchi anakuwa halipwi fidia, baada ya muda, anakuja tena mtu yuleyule anataka kufanya tena valuation upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hajalipa fidia, mbaya zaidi haji na jedwali ambalo liko kwenye bei ya soko ya muda huo, anakuja na jedwali la mwaka 2015, leo mwaka 2023, mdizi uliuwa unauzwa shilingi 2,000, leo anataka kumfanyia valuation mwananchi yuleyule kwa bei ya shilingi 2,000, kitu ambacho…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)