Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Eng. Dr. Leonard Madaraka Chamuriho

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa kuniona na kunipatoa nafasi hii kuchangia hoja hii muhimu. Kwanza ninapenda kuunga mkono hoja bajeti hii kwani ni bajeti ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda vilevile kumpa pongezi Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutuletea bajeti ya wananchi, kwani ni bajeti murua ambayo ukiangalia amefuta ada kwa kidato cha tano na sita, vilevile kwa vyuo vya ufundi ili tuweze kupata rasilimali watu nzuri kwa nafuu kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ametoa mikopo kwa vyuo vya kati na anaendelea kutafuta rasilimali kwa miradi mikubwa ya maendeleo kama vile SGR, Bwawa la Nyerere, na hivi karibuni ametutafutia wawekezaji wazuri katika Bandari yetu ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na timu yake; Naibu Waziri, Mheshimiwa Chande; Katibu Mkuu, Dkt. Natu Mwamba na Naibu Makatibu Wakuu pamoja na timu nzima, kwa kuweza kumsaidia Mheshimiwa Rais kutuletea bajeti hii ambayo ni nzuri kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ntajikita kwenye vifaa vya ujenzi ili kuona ni jinsi gani tutawezesha miundombinu hii ambayo Mheshimiwa Rais anaitolea pesa itakavyoweza kutusaidia ili tuweze kupata value for money.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 107 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeelezea vizuri kuhusu cement na jinsi ambavyo inalindwa pamoja na wafanyakazi wake. Lakini ninapenda kutoa mchango wangu kwa kuhakikisha kwamba hii cement ili isipande bei ni nini ambacho tunatakiwa tukifanye kwenye uendeshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia hapa nina orodha ya viwanda 14 vya cement (saruji) kama ambavyo vimewasilishwa, na vilevile nimeangalia hotuba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara ambayo imeonesha kwamba jumla ya uwezo wa uzalishaji (installed capacity) ya viwanda vyetu hivi ni tani milioni 10.48. Lakini uzalishaji wa sasa hivi ni tani milioni 7.6, na matumizi kwa sasa hivi ni tani milioni 7.1. Kwa hiyo, tuna ziada kidogo ambayo inakwenda nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia katika hiyo bajeti inasema kwamba bei ya cement imeonesha uhimilivu, kwani ina ongezeko la 0.5 tu. Sasa hii inabidi ilindwe ili tuweze kupata unafuu katika bei ya saruji tuweze kuendeleza miundombinu yetu ambayo tunaijenga kwa pesa ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali ijikite katika kuhakikisha kwamba hii bei haipandi. Nini kifanyike; ukiangalia uwezo wa kuzalisha saruji na baadhi ya viwanda vyetu utagundua kwamba viwanda vikubwa vinazalisha chini sana ya uwezo wao. Ukiangalia kwa Mfano Kiwanda cha Mbeya Cement, kinazalisha asilimia 43 tu; ukiangalia Dangote Cement, anazalisha asilimia 54 tu. Kwa hiyo, hivi viwanda vikiongeza uzalishaji vitahakikisha kwamba cement (saruji) inakuwepo na haitapungua bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tumeona ukosefu wa saruji umesababisha bei kupanda, lakini hawa wawekezaji wakubwa kama watapandisha uzalishaji uendane na installed capacity, tunaweza kuhakikisha kwamba tunapata saruji ambayo itakuwa ina bei ambayo inaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tulishuhudia huko nyuma kwamba viwanda hivi vikipanga matengenezo kwa pamoja vinasababisha uhaba wa saruji, kitu ambacho kinasababisha tena bei hiyo kuweza kupanda. Hivyo, tukiweza kuhakikisha kwamba hivi viwanda tunaviratibu vizuri ili vifanye matengenezo yao makubwa, siyo kwa wakati mmoja ili uzalishaji usiathirike, basi tutahakikisha kwamba upatikanaji wa saruji unaendana vizuri na uwezo wa viwanda hivyo ili viweze ku-maintain hiyo bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kama Wizara husika itaangalia, kuna orodha ya kampuni ambazo tayari zimekwishajiandikisha hapa lakini bado viwanda vyao havifanyi kazi. Kama vitaanza kufanya kazi tutahakikisha kwamba saruji itapatikana na vilevile tutaweza kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye nondo unakuta kuna changamoto hiyohiyo. Ukurasa wa 144 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeongelea hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona umeniwashia taa.

MWENYEKITI: Ndiyo Mheshimiwa, muda wako umemalizika.

MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda tu kumalizia kwa kusema kwamba viwanda tuvijengee uwezo wa kuzalisha bidhaa hizi ndani ili tuweze kupunguza bei na miundombinu anayotafutia pesa Mheshimiwa Rais iweze kudumu. Ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)