Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi nichangie katika Bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja kwa asilimia 100 bajeti ambayo imeletwa na Waziri wa Fedha; na nimpongeze sana pamoja na timu yake kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kiasi kwamba wamerahisisha mambo mengi kwa sababu imegusa maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuunga mkono niendelee kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameweka mkono wake kwa kiasi kikubwa sana katika bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wanachangia Waheshimiwa Wabunge kwenye bajeti wengi walikuwa wakilalamikia tozo mbalimbali ambazo zilikuwa pengine ni changamoto kwa wananchi na namna ambavyo wengi walikuwa wanakwepa kodi. Nakumbuka kuna baadhi ya Wabunge, Mheshimiwa Manyanya na Mheshimiwa Kamonga waliongelea habari ya capital gain. Capital gain mara nyingi watu wamekuwa wakinunua ardhi au wananunua nyumba kufanya transfer walikuwa wanakwepa kwa sababu ya kiwango kilikuwa kikubwa cha asilimia 10. Kwa kilio kile Mheshimiwa Rais amepunguza kutoka asilimia 10 mpaka asilimia 3 ni punguzo kubwa sana ambalo halijawahi kutokea. Mara nyingi tukipunguza tunakwenda kwenye 50 percent, lakini Mheshimiwa Rais amekwenda mbali zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe watanzania wale wote ambao walikuwa wanasita sasa kubadilisha hati zao kuwa kwenye majina yao wabadilishe kwa sababu tayari wameshapata fursa nzuri ya kuweza kumiliki ardhi zao kwa majina yao na wakatumia pia kwa shughuli za kimaendeleo. Punguzo hili limeleta nafuu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja, walizungumza Mbunge alikuwa ananiuliza hapa kwamba na kwa wale warithi inakuwaje maana hawana uwezo. Naomba niseme kwenye suala la transfer kwa mrithi halipi ile capital gain tax kwa sababu ni transmission tu kutoka kwa mzazi kwenda kwa mrithi ambaye yupo kutoka kwa marehemu. Anacholipa yeye ni mambo ya stamp duty pamoja na ile gharama ya registration. Kwa hiyo nao pia watambue ya kwamba wana haki ya kuweza kumilikishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nimpongeze pia sana Mheshimiwa Rais na hasa katika suala zima la umiliki wa nyumba. Mara nyingi watu wengi wamekuwa wakiogopa, kwamba tunasema nyumba za gharama nafuu lakini bado walikuwa wanaona si gharama nafuu; na kubwa lililokuwa linaleta changamoto ilikuwa ni suala la VAT. Sasa Wizara ya Fedha wamekuja na pendekezo ambalo ni zuri kwa kushirikiana na wizara husika ambayo tunatarajia wale wote ambao walikuwa na mpango wa kumiliki nyumba hasa zile zinazouzwa na taasisi zetu National Housing, TBA, Watumishi Housing, NSSF, ambazo zinaitwa za gharama nafuu sasa watazinunua bila VAT. Kwa hiyo nasema tu kwamba tutumie fursa hiyo kwa sababu ni namna ambavyo unaweza kumwezesha mwananchi, akiweza kuipata ile pia ataitumia katika shughuli zingine za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii haikuishia hapo tu, wengi walikuwa wakilalamika gharama za umilikishaji zilikuwa ni kubwa kiasi kwamba wanashindwa kupima na kurasimisha maeneo yao; lakini sasa gharama za kumilikisha zimepunguzwa kwa asilimia 50. Maana yake ni kwamba yeyote yule ambaye alikuwa pengine ana hofu ya kuweza kuomba hati sasa hivi imepunguzwa. Tuna viwanja 1,500,000 ambavyo tayari umiliki wake, kwa maana ya kwamba vina watu lakini hawamiliki kisheria, na wote hawa walikuwa wanaogopa kwenye suala zima la tozo zile ambazo zinatakiwa kulipwa lakini sasa hivi malipo yote yamepunguzwa. Ukienda kwenye premium imepungua kutoka asilimia 0.5 imekwenda 0.25 iko kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, punguzo lingine la hati kutoka asilimia 20 kwenda asilimia 10, ile deed plan ambayo ilikuwa inachajiwa 20,000, tunaita kiziduo kwa lugha yetu ya Kiswahili, sasa hivi unaipata bure. Sasa hivi kila kitu kimeshuka na ile kiziduo tena hakichajiwi. Niwaombe sana Watanzania bajeti hii imeleta nafuu sana katika suala zima la umiliki wa ardhi pamoja na umiliki wa nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais aliona changamoto kubwa ya watanzania katika suala zima la ulipaji wa kodi alitoa nafuu. Haijawahi kutokea Mheshimiwa Rais yeyote yule katika historia ya Tanzania, aweze kutoa msamaha kwa miezi kumi haijawahi. Sana sana tutapata mwezi mmoja, miezi miwili maximum miezi mitatu. Lakini Mheshimiwa Rais alitoa msamaha huo kuanzia Julai, 2022 mpaka 31 Aprili na katika kipindi hicho watanzania waliochangamkia fursa wamejitokeza kwa wingi na tumeweza kukusanya bilioni 38 lakini tozo ambayo walisamehewa ni bilioni 27 na zile zilizosamehewa Watanzania hawa wanaweza kuzifanyia shughuli zingine. Kwa hiyo nachotaka kusema tu ni kwamba bajeti hii imegusa maisha ya mtanzania katika kila Nyanja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo suala zima la uwekezaji, wawekezaji wetu nchini wamekuwa pia wakitafuta ardhi ya kuwekeza lakini imechangiwa pia na Mheshimiwa Rais kufungua nchi. Katika kipindi kifupi hichi ambacho tumekuwa nacho tumetoa ardhi kwa wawekezaji yenye hekta 29,820 ambayo imeimngiza fedha za Kitanzania trilioni 7.8 na haya yote ni ule mtaji ambao wamewekeza. Kwa hiyo, kwa maana nyingine wanaporahisisha pia masharti mbalimbali katika suala zima la umiliki wa ardhi inaleta nafuu. Na hii imekwenda mbali zaidi sasa hivi, ukiangalia ile Sheria ya Uhamiaji namba 54 nayo pia kwenye habari ya resident permit imepunguzwa pia imewekwa kiasi cha dola 150. Mwenye mtaji wa dola 150,000 anaweza kujenga nyumba yake na anaweza akauza kama watanzania wengine na hii inafungua fursa pia kwa Diasporas ambao watatambuliwa kwa hati maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunasema bajeti hii inakwenda kugusa kila mmoja lakini inakwenda kukuza pia mtaji katika sekta ya nyumba ambako pia wawekezaji wamepewa fursa. Mara nyingi tulikuwa tunalalamika kwamba wawekezaji hawapewi fursa. Maana yake ni kwamba akijenga nyumba haondoki nayo, akikiuka masharti ya nchi manake ataondoka atatuachia nyumba yetu, hapo tayari atakuwa ameshaendeleza mji. Kwa hiyo hili nalo limeleta nafuu kubwa katika suala zima ambalo lilikuwa likipigiwa kelele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kuliko yote katika suala zima la bajeti ya mwaka huu, ukilinganisha na bajeti ya mwaka jana; mwaka jana kwenye fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo zilikuwa ni bilioni 27 lakini mwaka huu fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo ni bilioni 82.13 sawa na ongezeko la asilimia 203 haijawahi kutokea. Ndiyo maana nasema Mheshimiwa Rais kwa kweli amefanya jambo la msingi sana na tukiangalia ardhi ndiyo sekta wezeshi katika maeneo mengine yote. Unapokuwa umewezeshwa katika suala zima la kuwa na program hii ya maendeleo ya sekta ya ardhi kwa kiasi kikubwa hiki tunachokipata ni utekelezaji wa kuzingatia sheria namna ambavyo Watanzania tunatakiwa tuzizingatie. Hii kwetu imekuwa ni rahisi kwa sababu tunakwenda kuwekeza pia katika miundombinu ya upimaji ambayo ilikuwa ina shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, mtakumbuka wakati mnachangia Wizara ya Ardhi mlipiga kelele sana kuhusiana na suala la kwenda kwenye vijiji, kwamba vijiji vilikuwa vichache. Kilio hicho kimesikika na kwenye bajeti kimeoneshwa ya kwamba sasa vijiji vitakavyokwenda kupimwa ni vijiji 2000 ambavyo vimeongezeka kutoka vile vijiji 250 vilivyokuwepo. Katika upimaji wa hivi vijiji pia vinatoka katika vijiji 1,059 ambavyo tayari vina mpango wa matumizi. Na katika suala hili kwa sababu tunahitaji pia kuona kwamba uwekezaji mkubwa unaenda kwenye sekta ya kilimo. Tumekuja kukubaliana na wenzetu wa kilimo kwamba, ardhi yote ya kilimo ambayo inafaa kwa kilimo itatambulika na itatangazwa katika gazeti la Serikali ili iweze kutunzwa kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wote ambao watapata fursa ya kupewa maeneo yale kwa ajili ya kilimo, niwaombe sana watimize masharti ambayo tunahitaji pengine kila mwekezaji anapopewa aweze kutumia eneo lake kwa faida na kama jinsi alivyoomba. Kuna wengi wanapewa ardhi lakini wanaiacha na watu wanavamia tunakuwa na migogoro. Naomba sana katika wale ambao watapata fursa ya kumilikishwa ardhi kipindi hiki niwaombe sana kwamba watekeleze masharti yote yanayotakikana ili tuweze kuondokana na kero ambayo tulikuwa nayo katika kipindi cha nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yamefanyika katika sekta hii ya ardhi ambayo mara nyingi imekuwa na migogoro mingi lakini kwa hiki ambacho kimefanyika katika bajeti ya mwaka huu tuna imani tunakwenda kuboresha na hasa mifumo ambayo tayari tumekwishaanza. Sasa hivi ukiangalia hata usafishaji wa takwimu zetu, kwa maana ya data cleaning inaendelea kufanyika na nyingi zimefanyiwa tathmini na kuweza kurekebishwa, na tunakwenda kupata taarifa zetu kupitia kiganjani. Tulikuwa tunazungumzia habari ya maji unaweza kupata bili ukalipa sasa hivi pia kwenye sekta ya ardhi imekwishaanza na watu wameshaanza kupata taarifa zao kiganjani kama una deni unaletewa pale na unaweza kulipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo haya yote ni kwa sababu tu tumewezeshwa kama wizara kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda sawa. Ninakushukuru nimekuibia dakika zako mbili lakini Mungu ni mwema nimemaliza niliotaka kusema, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)