Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kushukuru, kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini nimshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Lazima tukiri kwamba wakati fulani Taifa letu linahitaji kufanya maamuzi magumu sana ili tuweze kupiga hatua za maendeleo na sisi kizazi cha leo tunatambua waasisi wetu waliotangulia wa Taifa hili kuanzia kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuja kwa Rais wetu wa Awamu ya Sita yamefanyika maamuzi mengi magumu ambayo yamelifanya Taifa hili kuwa Taifa imara, yamelifanya Taifa hili kuwa Taifa lenye amani na utulivu na mambo mengi kadha wa kadha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuchukua hatua muhimu kabisa za uchumi katika Taifa letu. Tunampongeza sana Rais wetu kwa kuendelea kuchukua maamuzi magumu ya kiuchumi na Baba wa Taifa aliwahi kusisitiza miaka ya 1961 wakati wa Arusha Manifesto. Sisi katika Sekta ya Utalii Baba wa Taifa aliyaondoa na kuyapandisha hadhi baadhi ya maeneo ili tuweze kuhifadhi na alisema kwamba tutafanya kila tuwezalo ili tuweze kuhifadhi, kwa sababu uhifadhi si tu kwa ajili ya kustaajabishwa na wale wanyama lakini bali tunahifadhi ili iwe mustakabali wa kizazi cha leo na kizazi cha kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunasema Hotuba ya Waziri wa Fedha, kwanza nimpongeze sana na sisi tunampongeza na kumtia moyo aendelee kufanya kazi nzuri ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika eneo hili la fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu Dkt. Samia kwa mara ya kwanza kabisa alifanya maamuzi magumu ya kutoka ofisini na kwenda kuitangaza Tanzania kupitia Filamu ya Royal Tour na watu wengi walibeza. Watanzania wengi walizungumza maneno mengi sana kuhusu ni kwa nini Mheshimiwa Rais leo hii ametoka ofisini na kwenda kuitangaza Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha amezungumza kwa kina mapato yaliyopatikana kutokana na utalii ambayo yametokana na kazi kubwa ambayo imefanywa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi tunasema tutaendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na wakati mwingine Taifa letu kama ambavyo nimesema tunahitaji kufanya maamuzi magumu na maamuzi haya aliyoyafanya, anayoendelea kuyafanya katika uchumi, katika sekta yetu ya utalii ni maamuzi ambayo yatalifanya Taifa hili kupiga hatua sana kwenye sekta hii ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewasikia Waheshimiwa Wabunge wengi katika hoja walizozizungumza hapa kwa mara ya kwanza kabisa tumewaona Waheshimiwa Wabunge wamezungumza sana kuhusiana na utalii. Katika miaka mingi sana tumekuwa tukizungumza kuhusu hifadhi. Msingi wa uhifadhi ulianzia nyakati za Baba Taifa, utalii haukuzungumzwa kwa muda mrefu sana kwenye Bunge hili katika miaka mingi sana, lakini tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge wamezungumza sana kuhusu utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kwamba maeneo mengi ambayo wametushauri, tutakwenda kuyafanyia kazi. Hoja nyingi ambazo zilikuwa zinakwama kwa sababu ya urasimu kwenye Sekta ya Utalii tutakwenda kuzikwamua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukiri na kumshukuru Mheshimiwa Rais. Tulipoteuliwa kwenye nafasi hii mimi na Mtendaji Mkuu katika Wizara hii, tumeingia katika nyakati ambazo tumekuta kuna changamoto nyingi sana katika sekta ya uhifadhi. Tumekuta kuna changamoto nyingi za wanyama wakali, kuna changamoto nyingi za wanyama waharibifu na lazima nisimame hapa kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi, toka tulipoanza kujadili Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, tukaja kujadili Bajeti hii Kuu kila Mheshimiwa Mbunge aliyesimama hapa, alisema moja kwa moja. Katika misingi ya Ibara ya 21, wananchi wengi wanawakilishwa leo hii Bungeni na Wabunge waliochaguliwa na wananchi. Sauti za wananchi zimezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yao yote tukianzia kule kusini mpaka magharibi na maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nitambue mchango wa Mheshimiwa Kuchauka, Mheshimiwa Kitandula ambaye pia amezungumza kwa uchungu sana kuhusiana na matatizo ya uhifadhi, matatizo ya ndovu katika eneo la kule Jimboni kwake. Sisi kama Serikali ni lazima tujitafakari sana kwenye eneo hili, kwa sababu michango mingi iliyozungumzwa nikiri kabisa kwamba kama Serikali tusipochukua hatua za haraka tatizo hili linaweza kuwa kubwa zaidi hata ile dhamira ya uhifadhi tunaweza tusiione. Dhamira ya Baba wa Taifa kuhusu uhifadhi tunaweza tusiione. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi kama Serikali lazima tukajipange na nimewaambia wenzangu kila mmoja kwenye eneo lake tujipange hasa. Tunatambua kwamba eneo hili linahitaji fedha nyingi na Baba wa Taifa alisema kwamba pamoja na kwamba uhifadhi ni faida kwa Taifa letu lakini peke yetu hatutaweza ni lazima tupate msaada kutoka maeneo mbalimbali. Mashirika ya Kimataifa, lakini nilipotoka hapa asubuhi nilikuwa nateta na Waziri wa Fedha kumwomba zipo fedha ambazo zimetengwa kwa mujibu wa sheria na hizi kwa muda mrefu zimekuwa hazitufikii Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhifadhi ni gharama kubwa. Wahifadhi wetu wanafanyakazi kubwa na kazi nzuri sana, kazi ngumu sana pamoja na changamoto nyingi ambazo tunaendelea nazo lakini lazima tukiri kwamba changamoto la wanyama wakali ni janga ambalo tunahitaji kama Serikali kujipanga hasa ili tuweze kulimaliza. Inawezekana changamoto hizi zikawa zimesababishwa na pande nyingi; upande wa wananchi wanaweza wakawa na mchango wao, lakini sisi pia kama Serikali lazima tujipange hasa kwa sababu ipo mipango mingine ambayo inapangwa bila kushirikisha Wizara ya Maliasili na Utalii wakati mwingine, ndiyo inapelekea leo hii tunajikuta kwamba tuna matatizo mengi ambayo tunahitaji kwenda kuyatatua na matatizo haya yanahitaji fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nateta pale na Waziri wa Fedha kuona ni namna gani wataweza kuendelea kutusaidia kwa sababu mchango wa sekta hii hauwezi kudharauliwa. Sekta hii inatoa mchango kwa asilimia karibu 25 fedha za kigeni na kwa fedha za ndani GDP mchango zaidi ya asilimia 22, lakini mchango huu ni mdogo. Tunaamini kabisa tukijipanga vizuri tukaweka mikakati mizuri ya uhifadhi na utalii tukaweza kudhibiti wanyama wakali, tukaweza kutengeneza sera nzuri, tukadhibiti ubadhirifu wa fedha, tukadhibiti rushwa katika uhifadhi, tukadhibiti rushwa katika uwekezaji wa uhifadhi. Naamini kiasi hiki ambacho leo hii tunakiona asilimia 25, asilimia 21 kwenye pato la Taifa, basi tunaamini kabisa tunaweza kuvuka lengo na kufika mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha amenithibitishia, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge pamoja na Mwenyekiti wa Kamati, alipokuwa anazungumzia suala la retention na fedha nyingine za kisheria ambazo zinapaswa kuja kwenye Wizara. Waziri wa Fedha amenithibitishia na yeye ni msikivu sana, naamini tutakaa pamoja kuweza kuona ni namna gani tunawenda kumaliza changamoto hizi kwa kupata fedha ambazo ameniahidi kwamba Wizara itapata ili tuweze kuzimaliza hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na michango mingi ambayo Waheshimiwa Wabunge wamechangia katika Bunge lako hili tukufu pamoja na mambo mazuri ambayo Waziri wa Fedha ameyazungumza. Sisi kama Wizara tutaendelea kujipanga vizuri. Naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge, tunatambua Wizara yetu ina–cover karibu asilimia 50 ya nchi yetu, asilimia 50 ya nchi yetu ipo ndani ya hifadhi. Tuna kazi kubwa kila mmoja wetu na sisi tunawaahidi Waheshimiwa Wabunge, wawakilishi wa wananchi, kama ambavyo wameweza kuzungumza kwa kina hapa kuhusu changamoto za wananchi kwenye maeneo yao, tutafika huko, tutakwenda tuweze kuona namna gani tunatatua changamoto ambazo zinawakabili katika maeneo ambayo Wabunge wanawawakilisha wananchi kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tuwathibitishie Watanzania, changamoto hizi zimepata mwenyewe na mwenyewe si mwingine ni huyu Mndengereko. Tutakwenda kuhakikisha kwamba changamoto hizi tumezimaliza, tutafika kusini, tutafika magharibi, mashariki na kaskazini kuhakikisha kwamba mzigo huu tuliokabidhiwa tunautendea haki na Watanzania wawe na furaha na nchi yao katika nyakati zote za masika na kiangazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda ni mdogo nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)