Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi nichangie kwenye hoja zilizoko mbele yetu. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutupa uhai ili tuweze kulitumikia Taifa letu. Nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja, naunga mkono bajeti yetu. Bajeti nzuri inayoendelea kutoa matumaini kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyoliongoza Taifga letu kuweza kupata maendeleo ya kiuchumi. Wote tunafahamu kwamba bajeti iliyoko mbele yetu, tunazungumzia bajeti ya shilingi trilioni 44.4, ni bnajeti kubwa na ni bajeti inayoenda kugusa maisha ya Watanzania. Lakini kinachofurahisha zaidi ni kwamba takribani shilingi trilioni 30.2 zitatokana na mapato ya ndani ambayo yataweza kusaidia kuendesha bajeti hii, naipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile, naipongeza Serikali kwa jitihada inazozifanya katika kuvutia uwekezaji katika nchi yetu. Taarifa zinatuonesha kwamba kuanzia mwezi wa pili mwaka huu TIC imeweza kuidhinisha miradi 162 yenye thamani ya dola milioni 1,833 na miradi hii inakwenda kuzalisha ajira ya takribani 25,900. Hongera sana Serikali kwa jitihada hizi tunazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia kitabu cha Mpango wa Hali ya Uchumi nikawa naangalia takwimu zilizoko pale ndani; takwimu zile zimenifariji. Wote tunafahamu kwamba ulimwengu sasa unapitia kwenye mdololo wa kiuchumi lakini licha ya kuwepo kwa mdololo wa kiuchumi bado kwenye nchji yetu tumeweza kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa kwa mwaka huu kilikuwa ni asilimia 4.7 ukilinganisha na asilimia 4.9 ya mwaka jana. Sasa unaweza kuona kwamba kuna kushuka kidogo. Lakini tukizingatia athari za kiuchumi zinazotokana na vita ya kule Ukraine na matatizo ya mafuta katika ulimwengu lazima tuseme kama Taifa tumefanya vizuri sana kuhakikisha kwamba tuna-maintain ukuaji wa uchumi wa kiwango hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na jambo linalofurahisha ni jinsi ambavyo Serikali imekuwa na uwekezaji wa kimkakati kwenye miradi ya kimkakati. Wote tumeona uwekezaji mkubwa umefanyika kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, reli, sekta ya maji pamoja na kwenye sekta ya elimu. Uwekezaji huu ndio umetuhakikishia tumekuwa na ukuaji huu unaoridhisha, Serikali hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja tu ambalo tunapaswa kuliangalia kwa umakini ni ukuaji huu wa uchumi. Ukiuangalia kwa kina unaona kwamba sekta zilizochangia ukuaji huu sekta inayoongoza ni sekta ya burudani kwa asilimia 19, sekta inayofuata ni madini kwa asilimia 10.9, sekta nyingine ni bima asilimia 9.2, malazi na chakula asilimia tisa. Lakini sekta inayogusa Watanzania walio wengi, sekta ya kilimo, ukuaji wake umeshuka na hapa kama Taifa lazima tuongeze maarifa tuone tunatokaje kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa sekta hii umeshuka kutoka asilimia 3.9 ya mwaka 2021 mpaka asilimia 3.3 mwaka 2022. Kitabu cha Hali ya Uchumi kinatuambia, mchango wa sekta hii kwenye GDP umeshuka kutoka asilimia 26.8 mpaka asilimia 26.2. Lakini alarming katika sekta hizi ni kwenye eneo la sekta ya uvuvi, hapa ndipo nilipo na maneno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa sekta ya uvuvi umeshuka kutoka asilimia 2.6 mwaka 2021 mpaka asilimia 1.9. Lakini mchango wa sekta hii kwenye GDP umedumaa, upo kwenye asilimia 1.8. Hii haiwezi kuwa sawa kwa sababu potential iliyopo kwenye sekta ya uvuvi ni kubwa, sekta hii hatujaitumia ipasavyo. Lazima tuongeze maarifa ya jinsi ambavyo kama Taifa tunaweza kunufaika zaidi na sekta ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia kwenye ufugaji wa samaki, kwa mwaka huu tumevuna tani 25,000 zilizotuingizia bilioni 170. Lakini tunazungumzia mabwawa ya kufuga samaki kwenye nchi hii, na ukubwa wake wote, tuna mabwawa 31,000. Vilevile tuna vizimba 780 vya kufugia samaki. Ongezeko la vizimba 307 kwa mwaka mzima, hii haiwezi kuwa sawa. Mheshimiwa Waziri tuongeze maarifa hatujatumia rasilimali yetu ipasavyo kwenye kufuga samaki kwenye ukanda wa Bahari; ni lazima tuongeze maarifa ili tunufaike. Kama wenzetu wanavyonufaika kama wenzetu wanavyonufaika kwenye blue economy lazima na sisi tujielekeze huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine nililoliangalia ni kiwango cha shughuli za uzalishaji kwenye kiwanda. Ukiangalia takwimu za hali ya uchumi zinaonesha kwamba kiwango kilishuka kutoka asilimia 4.2 ya mwaka 2021, na sababu ziko wazi, Vita ya Ukraine, kuongezeka kwa gharama za mafuta pamoja na kuongezeka kwa pembejeo za uzalishaji mali. Hapa sasa lazima tujiulize, kama uzalishaji wetu kwenye viwanda ulishuka, measures tunazoziweka kwa mwaka huu wa fedha zinatuhakikishia kwamba tutapandisha? au zitasababisha kuwa na ushukaji mkubwa kwenye uzalishaji kwenye viwanda vyetu. Hili lazima tuliangalie kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge hapa wamekuwa wakipiga kelele kwamba tumeweka tozo kubwa kwenye saruji, viwango vyetu vile vinaonekana ni vikubwa. Sasa tujiulize, kama tumeweka kodi kubwa kwenye saruji, je, wananchi wetu watamudu kutumia saruji zile? Kama hawatamudu, Je, mchango tunaoutegemea kutoka kwenye viwanda hivi kwenye pato letu la Taifa utakuaje? Utaathirika au utabaki vile vile? Maeneo haya ni vizuri tukayaangalia kwa umakini ili tuweze kutoka vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine nawapongeza kwa jinsi ambavyo wamekuwa wasikivu na kadhia ile ya biashara kule Kariakoo na mpaka tunazungumzia kupandisha kiwango cha VAT kwa turn over ile ya kutoka milioni 100 mpaka milioni 200 na kuendelea. Hapa lazima tuwe makini sana. Tumekuwa na ukuaji wa viwanda vidogo vidogo katika nchi hii na vimeleta msisimko kwenye uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, sasa, wawekezaji wengi kwenye viwanda hivi mtaji wao huo unalenga hapo kwenye milioni 100. Sasa tunapowatoa kwenye eneo hilo tunawapeleka kwenye turn over ya milioni 200, lakini tukumbuke kwamba, kwa sababu hawa uwezo wao ni mdogo wamekuwa wakinunua raw materials kwenye viwanda ambavyo vyenyewe viko kwenye mfumo wa VAT. Kwa hiyo, raw materials watakazonunua itakuwa ni ghali, lakini wao hawapo kwenye mfumo wa VAT. Kwa hiyo, hawatakuwa na uwezo wa ku–recover kile kiwango cha VAT walichokitumia kutokana na kununua raw materials. Hapa naona kuna mgogoro, tunaweza kukuta tunaua ukuaji wa hivi viwanda vidogo. Mheshimiwa Waziri waliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka siku zilizopita kulikuwa na utaratibu wa kuruhusu wafanyabiashara wanaotaka kuingia kwenye mfumo wa VAT, wakaruhusiwa kwa mpango maalum. Wizara waliangalie hili ili hawa wawekezaji kwenye hivi viwanda vidogo vidogo wanaolazimika kununua raw material kwenye viwanda ambavyo viko kwenye mfumo wa kulipia VAT wasije wakaathirika na waweze ku–recover fedha hizi wanazozitumia.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)