Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa asubuhi ya leo na mimi kuwa miongoni mwa wachangiaji wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/2024. Nami nianzae moja kwa moja kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na afya njema, pia nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Wasaidizi wake wote hususan Wizara hii ya Fedha inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Mheshimiwa Naibu Waziri Chande na Katibu Mkuu Dkt. Natu na watendaji wote kwa kuwasilisha bajeti nzuri ambayo imeonesha Serikali hii namna gani ilivyokuwa sikivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge hili, tunafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Fedha na Taasisi mbalimbali. Tumeona mambo mengi kama tulivyoainisha kwenye taarifa yetu na nimpongeze Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Sillo kwa kuwasilisha vizuri, tumekutana na wadau mbalimbali, mapendekezo mengi yameingia kwenye bajeti ya mwaka huu na hatua mbalimbali za kikodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niipongeze Serikali kwa usikivu huo tulishauri iwepo Tume ya Mipango, Tume ya Mipango Sheria yake imeshapitishwa, tulishauri mapitio ya Sheria ya PPP imeshapita, tulishauri mifumo ya makusanyo ya mapato, Serikali imeboresha kupitia TAMISEMI imekuja na mfumo wa TAUSI, pia imekuja na Mfumo wa Manunuzi ya Umma ambayo imeboreshwa na ipo mbioni kuleta Sheria ya Manunuzi ya Umma, yote haya yanaonekana namna gani Serikali yetu ilivyo Sikivu, nampongeza sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo leo tunajadili bajeti ya trilioni 44, ni kiwango cha juu kabisa tangu tumepata uhuru wa nchi yetu, lakini inaonyesha namna gani Serikali hii inajiamini kwamba itaweza kufikia kukusanya trilioni 44 na kutumia trilioni 44, na mimi nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Bajeti ninaamini uwezekano huo upo, kwa sababu kati ya trilioni 44 inatarajia mapato ya ndani kukusanya trilioni 31. Nikiangalia mwenendo wa makusanyo ya mapato ya ndani kuanzia tu mwaka 2020/2021 ilikusanya trilioni 20 ikaja 2021/2022 trilioni 25 na mwaka huu unaoendelea wanatarajia Serikali kukusanya trilioni 27. Kwa hiyo, ni wazi trilioni 31 na hatua mbalimbali za kikodi walizopendekeza zinaweza kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba naiunga mkono Serikali inapokuja na mipango mingine ya kuongeza mapato. Ukiangalie umbile la bajeti, Serikali kwa shilingi trilioni 31 tu ya mapato ya ndani, lakini ina dhamana ya kulipa shilingi trilioni 10 mishahara tu na hii ni ongezeko la zaidi ya trilioni tatu kwenye mishahara, ina maana ajira mpya, ongezeko la mishahara na upandishaji wa madaraja. Naipongeza sana Serikali, lakini ina dhamana ya kulipa madeni shilingi trilioni 10 na sio madeni yaliyochukuliwa na pengine na Awamu ya Sita ni awamu mbalimbali, kwa hiyo, ina dhamana hiyo. Maana yake kuna kuwa na tofauti ya shilingi trilioni 13. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naipongeza Serikali kwa mipango mbalimbali ya kuongeza mapato na hapa mahsusi niendelee kuiomba Serikali tumepitisha azimio hapa IGA kwa ajili ya masuala ya bandari, naomba Serikali mchukue muda haraka mje na mikataba yenyewe, muendelee kuingia mikataba ili mwekezaji yule aje bandarini ili bandari iwe na nafasi ya kuchangia kwenye pato la Taifa, kwenye mapato ya ndani ili Serikali ipunguze kukopa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa naishukuru Serikali imepunguza kukopa kwenye vyanzo vya biashara, imejielekeza kwenye mahusiano ya kidiplomasia na ndio maana tumepata tena shilingi trilioni nane kupitia kwenye Benki ya Dunia kwenye mikopo ya masharti nafuu ambayo haina riba na haya yote ni kutokana na mahusiano ya Mheshimiwa Rais na nchi mbalimbali. (Makofi)

Kwa hiyo, nimpongeze na uimarishaji wa demokrasia ndani ya nchi yetu. Nataka pia niweke rekodi sahihi Kamati ya Bajeti hakuna mahali ambako tumekuwa na mashaka na matumizi ya mikopo kwenye miradi ya maendeleo. Tulichosema ni kushauri kwamba watizame kwenye yale matumizi ambayo hayaendi kwenye asset pengine wapunguze matumizi yale ya kawaida ambayo ni ya msingi yajielekeze kwenye sekta za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naipongeza sana Serikali nataka niseme pamoja na mjadala unaoendelea kwamba kwa nini; kuna kiongozi namuheshimu sana, anasema kwa nini Wabunge hatukuitwa jina moja moja kupiga kura, lakini nataka nimwambie yeye amekaa humu ndani ya Bunge miaka kumi, utaratibu wa kupiga kura ya kuitwa mmoja-mmoja ni kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali, lakini masuala mengine yote tu ni kwa utaratibu wa kuhojiwa na tulihojiwa na ndio maana tulisema kura ya ndio kwa wingi na ndio maana azimio lile limepita kuipa Serikali sasa muda wa kuendelea kuingia mikataba moja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nimkumbushe Profesa Tibaijuka alipokuwa Waziri mwaka 2013 aliwasilisha mpango wa kuifanya Mji wa Kigamboni kuwa Mji wa Kigamboni mpango wa shilingi trilioni 11 ndani ya Bunge ambao haukufanikiwa na tuliupitisha kwa kura hizi za kuhojiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo aiche Serikali inayoongozwa na mwanamama mwenzie ambayo imefanya mambo mengi na yeye akiwa mwanaharakati. Kwa namna ambayo Serikali imeingia madarakani, Mheshimiwa Rais Samia na kurithi miradi mikubwa mikubwa zaidi ya shilingi trilioni 21 SGR zinatakiwa, zaidi ya shilingi trilioni sita kwa ajili ya Bwawa la Mwalimu Nyerere, zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa ajili ya Daraja la Busisi na mabilioni na pesa nyingi, hakuna namna yoyote, lazima tutafute vyanzo vingine vya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo bandari haiwezi kuwa tunasema inauzwa kwa kusema mwekezaji atachukua gati namba zero mpaka saba, sisi Serikali tutabaki na gati namba nane, tisa, kumi, kumi na moja; huo sio uuzaji kwa lugha tu ya kawaida, ni lugha ya kushirikisha sekta binafsi, lakini tumeiona dhamira ya Serikali kwenye bajeti ya mwaka huu imeandaa mazingira ya kurejesha export credit guarantee scheme, zaidi ya shilingi bilioni 800 imetenga kwa ajili ya kuwawezesha wazalishaji wa mazao waweze kuuza nje, lakini ili kuweka fedha za ndani za kigeni nataka kusema Bunge tulitimiza wajibu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka niishauri Serikali imetambua kwamba vipo vikwazo mbalimbali kupitia utekelezaji wa blue prints taasisi za udhibiti kila taasisi inakuja na adhabu, tozo zake kaukaguzi, kwa kuwa imegundua inakuja na mfumo wa dirisha moja la malipo ya tozo mbalimbali na hili sisi tulilipata kwenye Kamati ya Bajeti. Chama cha Wafanyabiashara Wanawake; wanawake misingi yao si mikubwa lakini kwenye taasisi zetu hizi mfano OSHA wanatoza shilingi 1,200,000 kwa biashara mpya. Wana mafunzo kwa shilingi 300,000; wana certificate ya afya kila mfanyakazi shilingi 200,000; wana booklet sijui material shilingi 360,000; ukienda TBS tozo hizi ni nyingi kwa biashara ndogo ndogo. Serikali mmeliona namba mlisimamie kuanzia sasa kama mlivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili niipongeze kwa namna ambavyo mmefanya maboresho kwenye sekta ya utalii, kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye masuala ya uuzwaji na ukodishaji wa vifaa mbalimbali vya ndege ambavyo vinakwenda kuunga mkono kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Rais juu ya masuala ya Royal Tour. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba Serikali muangalie vyanzo vingine. Tuna vivutio vingi natoa mfano, kwa mfano Wilaya yetu ya Mafia kuna samaki mkubwa duniani hajapata kutokea, lakini bado hatujaona taratibu za kuweka kukuza utalii kupata vyanzo, lakini uwanja wetu wa ndege wa Mafia bado haujawekewa taa.

Kwa hiyo, naiomba Serikali iiangalie ili Mafia iweze kutoa mchango mkubwa katika sekta ya utalii, lakini sambamba na hilo Serikali ilifanya vizuri kuwekeza shilingi bilioni 90 kwenye miundombinu mbalimbali kwenye sekta ya utalii. Naiomba Serikali ule mpango wa kuanzisha kampuni ya kuweza kudhibiti au kusimamia matumizi ya mitambo iliyonunuliwa kwenye mbuga zetu mbalimbali ifanye haraka ili kampuni hiyo ianze kazi, lakini kana kwamba haitoshi pia naipongeza Serikali katika masuala mazima ya marekebisho ya sheria kama balozi wa kodi, kupunguza viwango vinavyotozwa kwenye makosa ya kutotoa risiti na ya kutodai risiti ili kuhakikisha kwamba wanatii sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Watanzania tuendelee kudai risiti na kutoa risiti. Kuna vyanzo vimependekezwa hapo, shilingi 100 kwenye mafuta, lakini pia shilingi 20 kwa kila kilo 20 ya mfuko wa cement. Yapo maneno yanasemwa yataongeza ugumu wa maisha lakini nataka niwaambie Watanzania hakuna namna ambavyo Serikali itapata shilingi trilioni 13 kupeleka kwenye miradi ya maendeleo bila ya kodi, lakini kama tunataka tupunguziwe vyanzo mbalimbali vya kodi lazima tudai risiti na tutoe risiti na sababu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana napenda kuunga mkono hoja. (Makofi)