Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hotuba hii muhimu na nitaanza hotuba yangu kwa kumnukuu Waziri wa Fedha kwenye hotuba yake ukurasa wa 72 kwa maandisha makubwa kabisa alisema; “kodi ni jambo la nchi, kodi ndio maendeleo ya nchi yetu” na mimi namuongeze kwa mwanasiasa nguli duniani alisema; “what’s the government gives it must first take away.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachomaanisha ni kwamba ili Serikali iweze kukusanya kodi ni lazima itengeneze walipa kodi wapya na sio kuongeza vyanzo vya kodi kwa walipa kodi wa zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasisitiza maneno yangu hayo kwa kumpongeza Waziri wa Fedha kwenye baadhi ya maeneo ametusaidia kuchechemua na kutengeneza walipa kodi wapya hasa katika eneo la kuweka mikopo na ada bure kwa wanafunzi wa vyuo vya kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli hilo ninampongeza sana kwa sababu moja kati ya changamoto kubwa katika Bunge hili tumeingia tuliokuwa tunapigania sisi tuliokuwa Wajumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilikuwa ni kuwapatia mikopo hawa mafundi au technicians au watu wenye ujuzi wa kati kwa sababu kimsingi watu hawa ndiyo wanaajirika kwa haraka, kimsingi watu hawa ndiyo ambao fani zao zinauhitaji mkubwa kwenye dunia ya sasa hasa Tanzania hii ambayo tunaenda kwenye viwanda vidogo vidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme ninaipongeza Serikali kwa upande huo lakini ninao ushauri mdogo. Kwanza wameondoa ada kwenye baadhi ya vyuo kwamba kwa wale wanafunzi ambao watachaguliwa na Serikali kwenda kwenye vyuo vya kati lakini pili wameweka course za vipaumbele kwa watu ambao watapewa mikopo hii na tatu wanasema kwamba wataanza kuwapa mikopo wanafunzi watakaoingia Mwaka huu wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wanasema maendeleo yanapaswa kuwafuata watu na siyo watu kufuata maendeleo. Imekuwa ni utaratibu au desturi Watanzania tunaenda tunavamia mahali, tunajenga nyumba ndiyo Serikali inakuja tunataka tufanye upimaji, urasimishaji na nini. Hao wanafunzi walioanza vyuo vya kati kipindi cha nyuma siyo kosa lao. Serikali haikuwa na mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba watu hawa wanapata mikopo na wanapata elimu katika mazingira sawa na wale walio katika vyuo vya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme viwekwe vigezo ambavyo vitaweza kuwafaa wale wanafunzi ambao tayari wapo kwenye masomo na hawapati mikopo na viwekwe vigezo kwa wale ambao wataanza ili wote kama Watanzania waweze kunufaika na rasilimali hii ndogo ya Taifa letu ambayo tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongezee kwa kusema kwamba Serikali lazima itoe ili iweze kuvuna. Huwezi kumkamua ng’ombe ambaye hujamlisha. Serikali imeweka nyenzo kwenye Sheria ya Manunuzi mwaka 2016 kwamba kwenye manunuzi yote yanayofanywa na Serikali itahakikisha 30% ya manunuzi hayo wanapewa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu lakini fursa hiyo imepokwa tena na Serikali kwa upande mwingine unasema hayo makampuni ambayo yatamilikiwa na wanawake au vijana au watu wenye ulemavu ili wapate kuzipata fedha hizo ni lazima waungane kwenye vikundi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kampuni is a legal person yaani anatambulika yeye mwenyewe kama kampuni na ana address yake, ana uwezo wa kushtaki na kushtakiwa, kwa nini unamlazimisha akae kwenye vikundi? Fedha za vikundi zipo kule halmashauri na Serikali inatengenezea mpango. Huu ulikuwa ni mkakati mwingine wa Serikali kuwainua wanawake wenye mitaji midogo na ya kati na ya juu waweze kufikia kufanya biashara na Serikali na Serikali ndiyo mfanyabiashara mkubwa duniani kote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niengomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha busara itumike, marekebisho yafanyike. Kampuni lolote ambalo linamilikiwa na mwanamke kwa 51% au inamilikiwa na kijana kwa 51% au mtu mwenye ulemavu iweze kuwa na sifa kamili bila kulazimika kuungana na makundi mengine kuweza kupata hii mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye jambo lingine la muhimu sana la upandaji wa vifaa vya ujenzi. Hii imekuwa dhana na nimesema hatuwezi kuendelea kama Taifa kama tunaongeza kodi katika maeneo mbalimbali badala ya kuongeza walipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna tatizo la msingi hapa. Serikali mwaka jana iliongeza kodi kwenye nondo, ikaongeza kodi kwenye mabati,Mwaka huu imeongeza kodi kwenye cement. Hivi mnataka tukakae kwenye nyumba za udongo? Mimi nataka kujua. Nalielewa lengo la Serikali, sekta ya cement, sekta ya nondo kwa maana ya chuma, ya mabati ni sehemu ambayo inabiashara kubwa sana lakini tusiwasahau Watanzania wa kawaida ambaye anatumia rasilimali hizi kujiboreshea mazingira yao ya kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mifumo yake ambayo inaweza kujua manunuzi haya yanafanyika kwa ajili ya viwanda, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na manunuzi haya yanafanyika kwa ajili ya wananchi kuboresha mazingira yao ya kuishi. Serikali imetueleza hapa juzi wanasema wenyewe wanayo Electronic Tax Stamps wanatumia mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kuweza ku-track. Kwa nini Serikali isitumie mfumo huo huo wakamuongezea tu huyu mkandarasi hadidu za rejea kwamba mabati, cement, nondo ambazo zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa madaraja, barabara sijui viwanda hayo yawe na tax yake tofauti na yale material yanayotumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kawaida? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi cement iuzwe leo shilingi 16,000 Dar es Salaam, Shinyanga inafika kwa shilingi 30,000. Angalia leo bati la grade 30 unaenda kuliongezea gharama. Mtu wa kiwanda hatumii bati la grade 30 lakini ikipunguziwa kodi wananchi wataacha kuezeka na nyasi kule kwangu Shinyanga. Nondo ambazo zinatumika kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ni millimeter 10, millimeter 12. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anaweza tu kusema wale watu wanaohusika na electronic taxation waweke hizo stamp. Zile zinazotumika kwa ajili ya domestic ziwe na gharama zake na zinazotumika kwa ajili ya industrial ziwe na gharama zake waongeze kodi huko lakini huku kwa wananchi kwa ajili ya kuboresha mazingira ya wananchi, kwa ajili ya kuboresha makazi na tulishasema tangu Azimio la Arusha. Mwalimu Nyerere alisema tuna ujinga, umasikini mpaka leo tunahangaikia kweli makazi wananchi sehemu nzuri ya kukaa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuhangaika na hilo, niseme niiombe Serikali kwenye eneo la kuongeza kodi kwenye vifaa vya ujenzi tunawaumiza Watanzania wa kawaida. Tunawaumiza Watanzania wa kawaida kwa hiyo tutofautishe tuweke madaraja na vifaa vya ujenzi ikibidi vitolewe bure. Wakati tunazungumzia hapa biashara ya cement na bei ya cement, tafiti zilizofanyika za haraka haraka cement Tanzania inaweza kuuzwa kwa shilingi 10,000 kwa mfuko lakini sasa hivi ukienda Mwanza cement ni shilingi 28,000. Leo tumeongeza kodi haya umetoa kwenye kodi ya cement umeongeza bado unaongeza kwenye kodi ya mafuta umeongeza shilingi 100, maana yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo cement kule imeshaongezewa gharama kuisafirisha mwisho wa siku anayeathirika ni mlaji. Umeshaiongezea gharama kuisafirisha kutoka Dar es Salaam ikifika Shinyanga imepanda bei zaidi msafirishaji anakwambia gharama ya mafuta imeongezeka wala haibebi gharama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana sana Serikali inayo mifumo tena mizuri ya kielektroniki ambayo inaweza ku-trace matumizi ya vifaa hasa vifaa vya ujenzi hivi ni kwa ajili ya domestic na kuboresha maisha ya Mtanzania, hivi ni kwa ajili ya maendeleo na ujenzi wa miundombinu watofautishe matumizi hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niongelee kuhusu bakaa. Mheshimiwa Rais anajitahidi sana kutafuta fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kimaendeleo. Kwa sasa nahudumu kwenye Kamati ya TAMISEMI. Bakaa fedha ambazo zinabaki yaani halmashauri zipo zinazoomba fedha hazipelekewi, zipo ambazo zinaomba fedha kidogo wanapelekewa fedha zaidi, zipo ambazo zinapelekewa fedha ya kutosha haitumii mpaka mwaka wa fedha unaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, ningeiomba Serikali kwa kweli na hili liko kwenye dhana ya utawala bora na kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri nimeliona. Ningeomba Serikali kwa nia ya dhati kabisa kila mtendaji apimwe kwa kazi anazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kukubali tunakwenda kwenye halmashauri kukagua unakuta Mkurugenzi ana fedha kwenye account, miradi haitekelezwi ukimuuliza anasema eti kamati haijakaa hatujakaa kujadili na kufanya nini, mara sijui mifumo haifanyi kazi. Kila mtu apimwe kwa utekelezaji wa kazi zake na sasa hivi tunavyoelekea mwishoni mwa mwaka, tathmini ifanyike ni Mkurugenzi yupi ambaye ameshindwa kutumia fedha kwa makusudi, ni yupi anafanya kwa uzembe, wengine hawawalipi wakandarasi kwa sababu wanajua itatengeneza riba ambayo na yeye atakuwa ni mnufaika kwneye riba hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali kwenye eneo hili la bakaa ni eneo ambalo limekuwa ni sumbufu sana kwenye maeneo ya halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hazijengwi, mabweni hayajengwi, miradi haitekelezwi ukiuliza anakwambia mara mifumo, kamati haikukaa, sijui force account haifunguki. Sisi hatutaki maelezo, it is either ufanye kazi kwa ajili ya Watanzania au useme umeshindwa aje mwingine atusaidie kutekeleza majukumu hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)