Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Pia nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa. Nianze pia kwa kumpongeza kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amefanya kazi kubwa sana kwenye bajeti hii. Nimpongeze Naibu Waziri na Timu nzima ya Wizara ya Fedha, jambo kubwa ambalo wamelifanya ni makusanyo ya trilioni 2.63, ama hakika mifumo waliyoiweka ya EFD na ETS ni mifumo mizuri na mifumo ambayo inatakiwa iendelezwe na iweze kusimamiwa ili tuweze kupata mapato mengi kwa kadri itakavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii inaenda kujibu changamoto za Watanzania, yako maeneo ambayo nimekuwa nikiyazungumza tangu bajeti zilizopita hasa eneo la elimu na leo ninao majibu ya Serikali. Tumezungumza kuhusu wanafunzi wa vyuo vya kati kupewa mikopo, Serikali imejibu hoja hii, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwenye eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo haikutosha, Serikali imeenda mbali zaidi hata kwenye eneo la afya. Tulizungumza hapa kwenye Wizara ya Afya kwamba tuna changamoto sana ya dawa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) inahitaji kupewa nguvu ya Serikali ili iweze kujisimamia. Mheshimiwa Waziri amekuja na majibu na ameahidi na kwamba Bohari Kuu ya Dawa sasa haitakuwa kitengo cha dawa, itakuwa ndiyo bohari ya kutoa dawa. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri amezungumzia suala la NHIF, tunajua sasa hivi NHIF ndiyo huduma pekee ambayo tunaitegemea sisi Watanzania ili tuweze kupata tiba. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ameamua sasa awalipe NHIF madeni yao, hiyo itawapa nguvu na sisi atakuwa ametusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko eneo la watumishi hapa. Serikali imeeleza vizuri eneo la watumishi na imesema itawapandisha madaraja, lakini pia eneo la watumishi hili Serikali imesema itawalipa madeni yao. Maana yake inatengeneza mazingira mazuri ya watumishi kufanya kazi. Nataka nikumbushe eneo moja muhimu sana, mtumishi anayestaafu anapata changamoto kubwa sana na changamoto hii yawezekana inasababishwa na namna ya kufikisha ujumbe wa mabadiliko anapokwenda kuhakikisha anapewa mafao yake, anakutana na kitu kinaitwa kikotoo, kikotoo hiki amekuwa hakijui tangu awali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikumbushe hapo na najua kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita. Kabla ya 2018, mtumishi alikuwa anapata asilimia 50 na asilimia 50 anaendelea kulipwa kwa kila mwezi kwa miaka kumi na tano. Mwaka 2018 ikaja asilimia 25 kwa asilimia 75, hii ilileta kelele nyingi sana ikalazima kusimamishwa na mwaka jana 2022 tukaja na formula ya 33 kwa 67. Hapa nampongeza Mheshimiwa Rais kwanza kuongeza kufika hiyo 33, lakini bado 33 haitoshelezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuishauri Serikali katika hili. Mtumishi huyu anakuwa hajafanya maandalizi na anakuwa hajui huko mwishoni atapata nini? Sasa kwa kuwa tunahitaji tumwandae vizuri, ni vizuri formula hizi aweze kuzijua mapema ili aweze kufanya maandalizi, hilo jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tumpe option ajaribu kuchagua na tuweke kama utakubali 50 kwa 50 ama utakubali 33 kwa 67 ili mtumishi aweze kufanya maandalizi yake ya kustaafu vizuri badala ya huu mfumo ambao tunaendelea nao tunawatumia tu Vyama vya Wafanyakazi, tunawatumia Chama cha Waajiri. Hawa hawawafikii walengwa, walengwa hawana taarifa, walengwa hawa ambao ndiyo wanasubiri wakistaafu wapate posho yao au wapate mafao yao wanapaswa kupewa taarifa mapema. Hili nataka niiombe Serikali ikalifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida tunalima sana alizeti na alizeti ndiyo icon ya Mkoa wa Singida, nembo kuu kwetu ni alizeti. Mwaka juzi amekuja Waziri Mkuu amehamasisha na alifanya mkutano wa wadau wa alizeti uliyojumuisha Mkoa wa Simiyu, Mkoa wa Singida lakini na Mkoa wa Manyara na tukawa tumekubaliana mambo ya msingi, lakini kulifanya zao la alizeti kuwa zao la kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana, wananchi wamezalisha kwa wingi na Mheshimiwa Bashe amekuja akatupa mbegu bora, wananchi wamezalisha sana, alizeti ipo ya kutosha ila alizeti imeshuka bei. Leo gunia la alizeti ni 35,000 maana yake kwa kilo ni shilingi 500, uandaaji tu wa kilimo cha alizeti una gharama zaidi hata ya hiyo fedha ambayo sasa ukienda kwenye kilimo cha mahindi, mahindi leo gunia ni 90,000, maana yake mwananchi ata–opt kwenda kulima mahindi leo hawezi kulima tena alizeti. Huko tunakoelekea zao hili sasa linaenda kupotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Nataka kuishauri Serikali, hapa tumeweka kodi ya ushuru wa mazao asilimia 25. Huko nyuma kabla ya kuingia kwenye Covid-19 ilikuwa asilimia 35 wakati wa Covid-19 tuliweka incentives tukapunguza, sasa hii asilimia 25 bado pia ni changamoto. Nataka kuiomba Serikali turudi kwenye asilimia 35 ili kulinda hili zao letu la alizeti. Hilo jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni lazima tuweke utaratibu wa kibali, hatuwezi tu kumruhusu mtu kuagiza holela. Leo tuna upungufu wa alizeti zaidi ya tani 350,000. Sasa kama hawatalima zitaongezeka na usipotoa kibali maana yake huyu mtu anaweza kuagiza tani 500,000 zikazidi hata ule upungufu wetu, ndiyo tunaua kabisa zao hili la alizeti na mafuta haya ya alizeti. Kwa hiyo nataka kuiomba Serikali, iweke utaratibu wa kibali na kibali kilitolewa kwa kuzingatia mazingira, kuna wakati wa mavuno huwezi kutoa kibali wakati huo, kibali kitolewe wakati sisi tunalima na kibali kitolewe kulingana na mahitaji yetu. Hilo ni jambo la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, ukitoka hapa ukiwa unaelekea Singida mpaka kule Shelui kwa Mheshimiwa Mwigulu, Iramba pale njia nzima unaona mafuta yamezagaa. Nataka kuomba Serikali tuwe na soko la mafuta ya alizeti kwenye maeneo husika, ukitoka hapa ukiwa unaelekea Morogoro utaona mafuta yamezagaa, hapo hata TBS hawawezi kutupa kiwango cha mafuta ambayo yanauzwa pale. Hapa tunatakiwa tu–brand vizuri mafuta yetu ya alizeti na tuyatengenezee mazingira mazuri. Kama Waziri anaweza kutengeneza shade kwenye maeneo ya Dumila pale mbogamboga na matunda, kwa nini asitengeneze shade kwenye mafuta ya alizeti tukayapa thamani? Nataka kuiomba Serikali ifanye hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi sana kwenye eneo hili, nataka kuiomba Serikali irudi kufanya tathmini kwenye eneo la tozo, eneo la tozo la miamala tufanye tathmini tuone kwa kiwango gani mpaka sasa tumefanikiwa na tumeathirika kwa kiwango gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nifanye rejea ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, aliwahi kusema mwaka 2019; kodi ya miamala ya simu ni regressive kwa maana kwamba alieleza naomba ninukuu kwa kiingereza; “they do not discriminate across ability to pay.” Hii haiwezi kutofautisha ya mtu mwenye uwezo wa juu na mwenye uwezo wa chini, wote wanakata sawa. Hili jambo la kwanza alisema. Jambo la pili, alisema; “cause negative impact on usage and the tax base.” inaleta matokeo hasi kwa watumiaji wa simu na walipa kodi. Jambo la tatu alisema; “create negative effects on economic growth and job creation across the economy.” Akasema pia inaleta matokeo hasi katika ukuaji wa uchumi na ajira. Maana yake kipato kikipungua na ajira inapungua. Sasa ni jukumu la Serikali leo kwenda kutathmini hali tuliyonayo sasa hivi katika hayo makusanyo ambayo tunayafanya. Inawezekana tunaona tunakusanya kwa wingi lakini kumbe tunapunguza ajira kwa wingi, pia huo ukuaji wa uchumi unaenda kwa kusuasua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maeneo yote ni ya msingi sana kuweza sisi kuyasimamia. Nataka nirudi kuipongeza Serikali, Singida Mjini tumepata mradi wa maji wa miji 28. Mradi huu ndiyo mradi mkubwa sana. Pia tumepata katika vitongoji vyetu 35 niwashukuru sana tumeweza pia kupata umeme na miradi inaendelea. Mheshimiwa Waziri nilimnukuu hapa alisema miradi yote ya Serikali ambayo iko kule akawataka viongozi walioko kule chini waweze kuisimamia na iweze kutekelezeka vizuri. Changamoto ninayoiona kuwaachia tu viongozi kusimamia bila kufanya follow up matokeo yake kesho tutarudi hapa kurudi kulalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuiomba Serikali itengeneze mfumo mzuri. Mfumo ambao unafanya follow up ya miradi yote ambayo tumepeleka kule, iwe miradi ya ujenzi wa vituo vya afya, iwe miradi ya maji, iwe miradi ya nini tufanye follow up ili kuhakikisha kwamba tunapata taarifa zilizo sahihi na zinapokuja kusomwa hapa ziwe taarifa ambazo zinaleta tija na sisi turudi kuzungumzia vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko mradi mwingine muhimu sana, tunauzungumza sana mradi wa TACTIC wa World Bank. Mradi huu naomba ufanyiwe kazi. Mradi huu unaenda kwa kusuasua sana. Kama fedha imetoka kwa nini fedha hii mradi usifanyike kwa Pamoja, hii habari ya phases inachelewesha maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)