Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ya bajeti kuu iliyoko mbele yetu, pamoja na mwenendo wa uchumi wa nchi yetu. Nianze kwa kumpongeza sana ndugu yangu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mwigulu Mchemba, Daktari wa Uchumi; Naibu Waziri wa Fedha, Makatibu Wakuu wote ambao wapo katika Wizara hii na watendaji wote kwa ujumla. Kwa kweli, wameleta bajeti ambayo inatupa mwelekeo mzuri wa tunakokwenda na tunakotoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wetu unakwenda vizuri, unaonesha uhimilivu. Sekta ya benki inaonekana ina afya, lakini siyo hilo tu, mapato yetu ya ndani yamezidi kuongezeka mwaka hadi mwaka pasipo kutumia nguvu kwa utawala wa sheria wala bila mabavu wala kuwindana. Dalili inaonesha kabisa kwamba mambo haya hayaji kwa bahati mbaya, ni kwa sababu ya uongozi mahiri wa Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na kuwa na maono mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii imekuja na msukumo mkubwa sana kwenye sekta ya binafsi. Tumeweza kuona mambo mengi ambayo yamekuwa yakifanyika na yanayoonekana yatafanyika katika kipindi hiki cha mwaka unaokuja, yanayoashiria ni kwa namna gani Serikali sasa inaona sekta binafsi ni muhimu kwa ajili ya kukua kwa uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona Sheria ya Kwanza ya PPP ambayo imetengenezwa kwa ajili ya kuleta sasa miradi ya sekta binafsi ya kimkakati. Tumeona hatua nyingi za kikodi, nisingependa kuzitaja hapa kwa sababu ya muda, lakini nitaje moja tu kwenye eneo la sekta ya madini ambako kwa kweli kulikuwa na ukakasi mkubwa wa kuweka vifungu ambavyo havitabiriki katika sekta ya madini ambavyo vilikuwa vinazuia kutafuta fedha pale ambapo ungeweza kutumia shares zako za kampuni ambayo iko hapa ndani kwa ku-invite wanahisa wale wale au wanahisa wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Sheria ya Kodi ilikuwa inaonekana kama ni deemed realization na kwa hiyo, ilikuwa ina-attract kodi. Sasa hiyo imeondolewa na nina uhakika sekta yetu ya madini inaenda kupaa kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mengi ambayo yamefanyika, lakini napenda niliongee lingine moja kuhusu mambo ambayo Serikali imeamua kuyafanya kwenye uthibiti. Kwenye BRELLA kulikuwa na ukakasi mkubwa sana, nami nilikuwa kwenye Kamati ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara ambapo tulikuwa tumetoa maoni kwamba ni vizuri Serikali ikaangalia, kule ndipo kwenye MSMEs nyingi zinakuwa registered, lakini kwa mfumo uliokuwepo ilikuwa ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu uchumi wake umekua, sasa tunaongelea Shilingi bilioni 85.4 na umetoka bilioni 69.9. Ni nchi ya sita na tuna nchi tano juu yetu. Kwa jinsi ninavyoona, uwekezaji unaoendelea, hali ya kutabirika inavyozidi kuwa katika nchi yetu, miradi ya mikakati, uwekezaji katika sekta ya LNG na rasilimali tulizonazo, bila kusita uongozi kamili, barabara, mahiri wa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, nadhani katika miaka michache ijayo, lazima nchi hizi tatu za juu yetu tutazipita kama tutakwenda katika mwendo tunaoendanao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea sekta moja kwa undani kidogo. Sekta ambayo nadhani ingeweza kuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wetu ni sekta ya isitu. Sekta hii ni kubwa, lakini mchango wake kwenye uchumi ni mdogo sana. Sekta hii kwa nchi nyingine ni sekta inayoleta mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi nyingine, lakini sekta hii inaweza kutusaidia kuokoa fedha za kigeni. Sasa hivi pamoja na ukuaji wa uchumi hapa nchini, lakini bado tuna tatizo la kwamba balance of payment kidogo tuko kwenye deficit, kwa sababu, bado tunaagiza vitu vingi kuliko tunavyopeleka nje. Kwa hiyo, sekta hii ya misitu inaweza ikasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ni sekta jumuishi, inatoa ajira nyingi sana, ina uwezo mkubwa wa kuchochea viwanda mpaka ngazi ya vijiji. Ndiyo maana lazima Wizara na Serikali iangalie hii sekta kwa makini sana, kwa sababu mwisho wa siku sekta hii ina uwezo mkubwa sana wa kuchangia mapato makubwa kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uhalisia, sasa hivi ukichukua mti wa mbao unaweza ku-recover asilimia 30 tu peke yake. Asilimia 62 ya mazao ya misitu ni mbao. Uki-process mbao hizo utapata katika meta za ujazo 200,000, uta-recover meta za ujazo 80,000. Kwa bei ya shilingi 250,000 utapata shilingi bilioni 24. Hiyo ndiyo value ya container moja la mita za ujazo 200,000. Ukienda kwenye mazao ambayo yamehandisiwa katika magogo ya mita za ujazo hizo hizo 200,000 unaweza uka-recover up to 80 percent ukapeleka kwenye MDF. Ukisha-recover hiyo unapata meta za ujazo 170,000. Bei ukiwa China kwa hiyo MDF, ni shilingi 600,000. Maana yake ni kwamba, hizo meta za ujazo 200,000 unaweza kupata shilingi bilioni 102. Kutoka shilingi bilioni 24 kwenda shilingi bilioni 102. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukichukua hilo container la ujazo wa 200,000 linaweza likazalisha pieces 283,000. Hizo pieces zinaweza zikazalisha furniture. Kwa bei ya China, furniture hizo ambazo sisi tunanunua hapa shilingi milioni 10, zinauzwa shilingi 800,000. Maana yake ujazo wa hizo mbao unaweza ukapata shilingi bilioni 226. Kwa hiyo, umetoka kwenye Shilingi bilioni 24 ambayo tunapata hapa, kama tungekuwa tumeongeza value tungepata shilingi bilioni 102, lakini ukipeleka kwenye furniture unapata shilingi bilioni 226. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sekta hii inatakiwa iangaliwe. Ukiangalia TFS wana mashamba karibu 11. Mashamba hayo yanazalisha karibu TCF 1,300,000. Sasa mimi nimechukua 200,000 tu peke yake, uki-multiply hizo na uzalishaji wetu wa mwaka mzima wa 1,300,000 mara 200 hata calculator inakupa error. Maana yake ni trillions of money tunazipoteza kwa kutokufanya value addition on a serious way katika nchi hii. Kwa kweli, hii forestry is gold by itself. Inaweza ikatuzalishia kuliko hata dhahabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama Vietnam, juzi juzi tu tulikuwa na uchumi sawa sawa kabisa, lakini Vietnam wameingia kwenye eneo hili la forestry wame-move, na sasa wana-export mazao ya misitu kwenda nchi nyingine bilioni saba walianza mwaka 1989, wamepanda wakafika bilioni 12. Sasa target yao ni bilioni 25 kwa misitu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema, Wizara inatakiwa iliangalie hili eneo kwa ukaribu sana. Cha kufanya kwanza ni ku-import technology ambazo ni rahisi, ambazo zitasaidia sisi kuingia kwenye uhandisi wa mazao ya misitu. Tunaomba sana kwa kuanzia tu watupe zero rating katika importation. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala la madawati, mtu amelia hapa; tuna uwezo mkubwa wa madawati. Kuna vijana hapa wana uwezo mkubwa wa kutengeneza madawati 1,500 kwa siku. Tukiweza kuwa-empower, tunasema tutatengeneza mabilionea, mabilionea tuanze kwa kuwa-empower watu watu watumie soft wood kutengeneza madawati ya nchi nzima, inawezekana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: …proposal ilikuja lakini mtu mmoja akadhania kwamba watu wana maslahi binafsi, tukapoteza miaka mitano ya kutengeneza madawati, sasa tunatumia madawati ambayo kwa kweli bado tunalia kilio kikubwa katika madawati. Tuna mbao,tunahitaji technology tunaweza tuka-import halafu tukatengeneza madawati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)