Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DENNIS L LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti hii ya Serikali. Kwanza, nianze kwa kumpongeza Rais wetu Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo inafanywa na Serikali yake. Kwa kiasi kikubwa bajeti hii ni ushahidi tosha kwa Bunge lako kwamba wamechukua kikamilifu maoni na mapendekezo ya Wabunge kuhusiana na maeneo ya vipaumbele katika kuibua fursa kwa wananchi wetu na kuimarisha uchumi wetu. Kwa hiyo, tunaweza kuona haya katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Mikumi nina kila sababu ya kupongeza Serikali ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu ndani ya kipindi kifupi kabisa tumeona mambo mengi ambayo yalikuwa ni kero kwa wananchi wa Jimbo la Mikumi yakipata suluhu ya kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mambo hayo ilikuwa ni suala zima la jibu la uhakika kuhusiana na soko la miwa la uhakika kwa wakulima wa Bonde la Mto Luhende. Tunaona Serikali kama Mbia wa Kiwanda cha Ilovo wamewekeza bilioni 571 kupanua kiwanda kile cha sukari ambacho kinakwenda kuwa suluhu ya kudumu kwa wakulima wa zao la miwa katika bonde lile. Pia, inaenda kuwa ni suluhu ya kudumu katika suala zima la uagizaji wa sukari kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaona sekta ya kilimo inachangia pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 26.2, lakini pia inaajiri Watanzania kati ya asilimia 60 na 70. Vilevile tunaona kwamba ina ukuaji usioridhisha kwa asilimia takribani tatu ukilinganisha na asilimia tano kwa mwaka uliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii sio njema sana kwa uchumi wetu kwa sababu tuna changamoto ya naksi ya bajeti katika urali wa fedha za kigeni. Vilevile tunaona kabisa moja ya suluhu ya kudumu ya changamoto hiyo ni kuzalisha sana mazao ya kilimo ambayo ni uti wa mgogo wa uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili tunaweza kuona asubuhi tulikuwa na mjadala kuhusiana na bei ya mahindi. Pia, naomba nirudie tena, kama tunaweza tukawekeza fedha nyingi katika uzalishaji wa chakula, tunaweza tukapunguza bei tuka-stabilize thamani ya fedha yetu lakini pia tunaweza tukawa na uhakika wa chakula. Kwa hiyo, tunaweza tukampelekea mwananchi uwezo wa kuweka akiba. Pia tunaweza tukajikita zaidi kwa kuwawezesha wananchi wetu katika kuzalisha mazao ya biashara kwa ajili ya Soko la Dunia, fedha za kigeni na kwa ajili ya kuimarisha thamani shilingi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumza mengi, lakini naomba niunge mkono Serikali kwa wazo la kuwa na Tume ya Mipango ya Taifa. Moja ya changamoto kubwa tuliyonayo ni kwamba, tuna bajeti nzuri sana, lakini hatuna coordination point, hatuna sehemu ya uratibu ambayo inaweza ikafanya taasisi zetu na Wizara zetu zikazungumza, zikawasiliana na tukawa na Tume ya Mipango ambayo kwa niaba ya Serikali inaweza ika–coordinate mambo yote makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Kwanza, wa Pili na wa Tatu ni jinsi gani unavyozungumzia suala zima la viwanda na biashara, lakini linkage ya ukuaji wa suala la viwanda na biashara, suala zima la ukuaji wa kilimo na suala zima la utengenezaji wa barabara za vijijini kuwaunganisha wakulima na masoko, bado kuna changamoto. Hapo ndipo unaona kuna umuhimu wa kuwa na Tume ya Mipango ya Taifa ambayo inaweza ika– ddress mahitaji ta maeneo mbalimbali kulingana na mahitaji ya uchumi wetu, kulingana na malengo ya ukuaji wa uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naamini kabisa kwa ujio wa hii National Planning Commission unakwenda kutuletea mipango ya muda mfupi, kati na muda mrefu tukafanya maamuzi ambayo yatakuwa na tija kwa wananchi wetu, maamuzi ambayo hayatapendelea watu kwa sababu ya influence yao bali mahitaji ya maeneo kulingana na umuhimu wake kwa uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba Sekta ya Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Pia, ni wazi kwamba dunia sasa hivi iko kwenye knowledge economy ambayo inahitaji uwekezaji mkubwa na ambapo hatuna fedha za kuwekeza huko. Hata hivyo, tuna maeneo kama ufugaji wa mifugo, uvuvi na kilimo ambayo yanatupa advantage ya ku–compete katika uchumi wa dunia, tuyashikirie hayo. Tukipambana kuyawekea nafuu ya kodi, ushuru, lakini incentive kwa wale wote wanaojikita katika maeneo hayo, nina imani kabisa uchumi wetu unakwenda kukua ili kukidhi matarajio yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la ardhi na mazingira. Ni wazi kwamba ardhi yetu haiongezeki ila Watanzania wanaongezeka, lakini mtaji mkubwa katika dunia hii ni ardhi. Tunajua kwamba eneo kubwa la Tanzania bado halijapimwa. Ni vizuri kupitia bajeti hii tupime maeneo yetu, tupange maeneo yetu, tuendeleze maeneo yetu sio kwa sababu yetu ila kwa vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika muktadha huo unaweza kuona hata upangaji wa miji yetu, maeneo mengi miradi yetu inakwama kwa sababu ya kutumia fedha nyingi kulipa fidia lakini tuna vijana ambao wamesoma kwa ajili ya upangaji miji, kupima miji na kuendeleza miji. Kwa nini wanashindwa ku–project mahitaji ya Tanzania kwa miaka 50 ijayo? Kwa nini wenzetu wanaweza sisi tushindwe? Kuna suala la commitment.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutakuwa na commitment na tukaiweka Tanzania ndani ya mioyo yetu, hatutakuwa sehemu ya kupiga besenga kwa kutengeneza mipango mikakati ya kutengeneza mazingira ya kupiga hela ya fidia ili tu ujineemeshe ama ujifaidishe wewe na familia yako. Haya tunayaona na tunayashuhudia kwa sababu wanaofanya hivi ni majirani zetu, ndugu zetu, jamaa zetu, ni lazima ifike mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu, bajeti hii imeongezeka na mapato ya makusanyo yameongezeka. Ni vizuri tukatumia technology kwa mfano hii electronic tax system ili ku–monitor uzalishaji lakini pia uuzaji wa bidhaa zetu kutoka viwandani mpaka kwa mlaji. Vile vile tupanue wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa kuanzisha vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea vyanzo vile vile ambavyo tayari vimeshachoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukafanya haya kama tunaweza kuwekeza kwa muda mrefu. Kwa mfano, kama tutatoa incentives kwa watu ambao wanajenga majengo kama National Husing, Watumishi Housing lakini pia Real Estate Developers ambao ni private, wakajenga units nyingi na tukawawekea tax exemption maana yake wanaweza wakauza properties kwa bei nafuu, watu wakanunua kwa wingi na Serikali ikapata mapato ya uhakika badala ya kuwachomekea kodi katika vifaa vya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, muda wako umekwisha.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sekunde 30, namalizia tu. Moja ya maeneo ambayo Serikali inawea ikapata mapato ni sehemu ya utalii na kilimo. Tuna SGR station pale Kilosa, lakini mtalii akiingia pale kwenda Mikumi atasafiri zaidi ya kilometa 100 za vumbi. Hata hivyo tumekwishazungumzia hili mara nyingi, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hii barabara hii iwe kipaumbele sio tu kwa ajili ya kusafirisha malighafi kwenda kiwanda cha sukari, lakini pia kusafirisha watalii ili tuipe tija na thamani uwekezaji mkubwa wa reli ya mwendokasi pale Kilosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)