Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na afya ili niweze kushiriki kuchangia Bajeti kuu. Jambo la kwanza, nichukue fursa hii kwa niaba ya wananchi wa Kilolo kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana anayoifanya. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu na ofisi yake kwa kuwasilisha bajeti nzuri yenye mwelekeo na dira nzuri kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza bajeti hii kwa sababu za msingi kabisa. Bajeti ya mwaka jana 2022 ilikuwa na Shilingi bilioni tatu kwa ajili ya shule za wasichana za mikoa inayojengwa Kilolo. Nina sababu ya kupongeza. Pia kuna kilometa 33 za barabara kutoka Ipogoro mpaka Kilolo, nina sababu ya kupongeza. Vile vile tumesema juzi tu kuhusu bypass ya Mlima Kitonga, kilometa 10, usanifu tumeshauona kwenye bajeti ili angalau watu wasikwame pale, tuna sababu ya kupongeza. Pia hii bajeti ina miradi mingi sana kwa ajili ya Kilolo; miradi ya VETA, miradi ya maji, ina mabwawa na mambo mengi mbalimbali, lakini na ruzuku ya mbolea na Kilolo ina maeneo mengi ya wakulima, nina sababu ya kupongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, nami naamini kwamba kwa mwenendo huu nchi yetu inaenda kupata sura mpya ya maendeleo katika uongozi wake. Nami namwombea maisha marefu, Mwenyezi Mungu ambariki ili aendelee kuwatumikia Watanzania katika kipindi ambacho Mwenyezi Mungu amempa nafasi hiyo kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye hoja chache ambazo ningependa kuchangia kwenye hii Bajeti Kuu. Jambo la kwanza, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kupiga marufuku maduka yasifungwe kwa sababu yoyote ile. Naomba nimwongezee kitu kimoja, naomba atakaposimama pia aagize magari yasikamatwe yanapokuwa yamebeba mizigo ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko hivi, mtu anatoka mjini, amenunua vitu vyake, amepakia kwenye gari, ile gari siyo yake, lakini aliyenunua vile vitu hajadai risiti, na yule mtu anaenda anafika, gari inakamatwa. Ile gari ikikamatwa inapelekwa yard. Ikipelekwa yard, kama ni Ijumaa ni hadi Jumatatu, na huyu mtu ni mfanyabiashara, na gari ile siyo ya yule aliyefanya kosa na aliyefanya kosa anajulikana. Kwa hiyo, huyu mwenye gari anapata hasara kubwa ya kutoendelea na biashara yake kwa sababu ya yule ambaye hakudai risiti. Kwa sababu anayenunua, haendi na mwenye gari dukani, wala hajashiriki hilo kosa la kutokudai risiti. Kwa hiyo, napendekeza kutokufunga maduka kuambatane pia na kutokukamata magari yale yaliobeba mali ili yale magari yaendelee na shughuli zake. Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili linalohusiana na mambo yaliowekwa kwenye bajeti hii kuhusu kodi ni suala la faini ile ya kutokudai risiti ile ya Shilingi milioni nne hadi Shilingi milioni tatu. Ni ukweli usiopingika kwamba ile ilikuwa inatengeneza kichaka cha rushwa, kwa sababu kama mimi nina mzigo wa Shilingi 300,000/= na sikudai risiti, hata gari ikipelekwa yard siwezi kupata hiyo Shilingi milioni tatu wala milioni nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona pale kuna pendekezo la punguzo, lakini Mheshimiwa Waziri naomba wasaidizi wako waangalie lile punguzo vizuri ili liendane na bei ya mzigo huu ambayo sikudai risiti. Huwezi kumdai mtu ambaye hakudai risiti ya shilingi 50,000, umwambie alipe shilingi milioni tatu hadi shilingi milioni nne, kwa sababu hana na kwa hiyo, mara nyingi unafungua milango ya majadiliano tu ya rushwa ili aweze kuondoka na huo mzigo wake. Kwa hiyo, hilo pia ningeomba niwasilishe kwa namna hiyo kwamba pia liendelee kuangaliwa ili lisiweze kuleta changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependekeza jambo moja kwenye mambo ya kodi, katika kipindi cha hivi karibuni, tulimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwani aliwaagiza TRA kuangalia zile kodi ambazo ni za muda mrefu zisiweze kulipwa, lakini kuna tafsiri nyingi sana kwenye hizo kodi za muda mrefu. Pale Iringa kuna mlipakodi mkubwa tu alikuwa anadaiwa kodi ya VAT lakini alipoenda akasema hizi zote zimeshasamehewa. Kwa sababu muda mrefu wenyewe yeye alitafsiri labda ni wiki moja, wiki mbili, wiki tatu, mwezi au mwaka. Kwa hiyo, napendekeza ofisi yenu inayo wajibu wa kutoa tafsiri ya huo muda mrefu na aina ya kodi ambazo zimepata huo msamaha ili kusitokee watu wa TRA kuwaonea wale ambao hawakupaswa kulipa wamesamehewa, lakini pia wale wanaotakiwa kulipa walipe bila kutumia hiyo kama kivuli cha kujitetea kutokulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda mliangalie ili mlipe tafsiri ya hiyo kauli, pia mpeleke kwa maandishi maelezo TRA ili wale vijana wanaosimamia hizo wasijiamulie wenyewe kwamba hii ndiyo iliyofutwa, hii haikufutwa. Kwa hiyo, hilo nafikiri ni vizuri mkaliwekea mkazo na mkaangalia katika utaratibu huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la kikodi, napenda kuzungumzia zaidi hii kwa sababu tunachangia bajeti na ni mapato na matumizi, ni kuhusu kuweka utaratibu mzuri kwenye mazao ya kilimo ambayo hayawezi kuwa na risiti za EFD. Kila kitu kimewekwa EFD, gari zinazobeba mchanga EFD na ukweli hamjasambaza hizo EFD kwamba magari yanayosomba michanga huko hayana EFD lakini na wao wanadaiwa EFD. Sisi tunaotoka kwenye maeneo ya kilimo tunapata shida sana kwa wakulima ambao wanataka kuuza mazao yao, kila siku ni lazima wachukue barua ya Mtendaji wa Kijiji, wapite TRA wachukue barua; anakuwa na barua karibu tano, kwa nini? Kwa sababu tu ajieleze kwamba yale mazao ni ya kwake ameyavuna shambani anayapeleka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huo usumbufu wa aina hiyo, utengenezeeni utaratibu ambao hausababishi hiyo kero. Pamoja na hizo barua zote, ukifika hapo Migori bado utakamatwa na hadi bei ya rushwa inajulikana, kwamba ukifika pale, ukitoa shilingi 200,000 ndiyo unapita. Kwa hiyo, sasa hii inakuwa pia ni mwanya wa rushwa ambao siyo mzuri. Kama kuna changamoto yoyote, kama ni mbao, kama ni njegere, kama ni viazi tunapopita pale ieleweke, nimetokanavyo shambani. Hata kama hukutokanavyo shambani, ukinunua kwa wakulima, umekusanya, hauna EFD na hawajapewa na huwezi ukawagawia wakulima wote EFD. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, uwekwe utaratibu mzuri ili iwe ni routine kwamba upo utaratibu, badala ya sasa hivi ambapo ni uamuzi wa unayemkuta getini kwamba inakuaje? Hiyo inawasumbua wakulima wetu sana, kwa sababu kila siku lazima watakupigia simu, “eeh, nipo hapa getini, leo wamenisumbua.” Unaanza tena kupiga simu kwa huyo mtu ili awaruhusu. Sasa hiyo inakuwa ni kero na nafikiri ni vizuri mkiiwekea mkazo ili iweze kutatuliwa na wakulima waweze kusafirisha mazao yao bila shida yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mimi sisemi wasilipe kodi, kama kuna kodi inatakiwa kulipwa, wekeni utaratibu mzuri wajue. Ile rushwa ambayo inatolewa pale, ile Shilingi laki mbili mbili, basi iwekeni angalau basi iwe ni Shilingi laki moja, ipungue nusu, iingie Serikalini badala ya kila siku kuacha Shilingi laki mbili pale kwa mtu. Nafikiri ile ingeweza kuwa ni suluhisho kubwa zaidi kuliko kujua kabisa kwamba nikienda pale ni lazima niwe na shilingi 200,000 na inaenda kwenye mfuko wa mtu. Hilo napenda liwe hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mawili ya mwisho, kwenye bajeti zijazo, hebu tuangalie, hiki chanzo cha hewa ya ukaa kimekaaje? Kwa sababu tunaona wawekezaji binafsi, mtu ana hekta 5,000 tu pale Kilolo anapanda miti, analipa watu hela nyingi tu anakuwanazo, huyo ni mwekezaji binafsi. Sisi Kilolo tuna hekta 52,000 za miti ya asili, hatulipwi hata buku na mtu yeyote. Sasa najiuliza, huyu amekuja amepanda hekta 5,000, analipwa hela, analipa watu 200 wafanyakazi kwenye ardhi yetu, sisi wenye hekta 52,000 hata buku hakuna. Kwa utaratibu upi? Hiyo bado nafikiri Serikali pengine iunde kikosi kazi kifanyie kazi. Hizo nazo ni hela atakuwa anapata, na Mheshimiwa Waziri utapata hela nyingi zaidi, pengine hata kodi nyingine zitapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)