Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii muhimu ya kilomo. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya njema. Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuijenga nchi yetu na kwa namna ambavyo ametoa kipaumbele kikubwa katika bajeti hii ya kilimo. Nampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugawaji wa pikipiki elfu 700, vishikwambi, 384 na extension kits 6,700 ni kilelezo tosha Mheshimiwa Rais anayo dhamira ya dhati ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo. Niwaombe sana Watanzania tumuombee mama yetu mpendwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuendeleza nchi yetu na aweze kuongoza vyema Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Bashe Naibu wake Antony Mavunde, Katibu Mkuu Edward Massawe na watendaji wote wa Wizara hii ya Kilimo kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya kuhakikisha kilimo chetu kinakuwa ni kilimo chenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia katika eneo la umwangiliaji na endapo muda utatosha nitachangia katika zao la alizeti na zao kitunguu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana mabadiliko ya tabia nchi na mazingira yetu jinsi yalivyobadilika tunahitaji kujikita katika kilimo cha umwangiliaji na si kilimo cha kutegemea mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wangu wa Singida ni miongoni mwa mikoa ambayo ni mikoa yenye jiografia iliyo kame sana. Hivyo, tunahitaji sana kuwekewa mabwawa ya umwangiliaji ili kuweza kuendeleza kilimo kwa msimu wa muda wote. Ninaomba sana tuweze kujengewa mabwawa ya kutosha katika Mkoa wetu wa Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia ni kuhusu Skimu ya Umwangiliaji ya Mbwasa. Niishukuru sana Serikali imeweza kututengea fedha katika bajeti hii kwa ajili ya kuendeleza skimu hii ya Mbwasa. Hata hivyo, kwa kuwa usanifu yakinifu umeshafanyika naupembuzi niombe sasa skimu hii ianze kufanya kazi na utekelezaji wa skimu hii uanze mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunalo Bwawa Mngamo pamoja na Bwawa la Msange ambapo wananchi wa eneo hilo wanatumia maji hayo kwa ajili ya kuendeleza shughuli za Kilimo. Niiombe Serikali, endapo mabwawa haya yataendelezwa yataweza kuwa na tija sana kwa wananchi wa Mkoa wangu wa Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Bashe alikuja akayatembelea Mabwawa haya ya Mngamo Pamoja na Msange na kujionea namna ambavyo mabwawa haya yanavyowanufaisha wananchi wa eneo hilo. Sasa nikuombe, kwa kuwa ulishatuma wataalam wakuja kuweka michoro na michoro hiyo imeshakamilika niombe sana sasa kazi hii iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wangu wa Singida tunalima zao la alizeti na kitunguu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye amekuwa ni kinara katika kuendeleza zao hili la alizeti. Pia nipongeze sana Serikali ambayo ilitoa mbegu kupitia taasisi yetu ya ASA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini yako maeneo mengine mbegu hizi zimezalisha alizeti vizuri lakini maeneo mengine mbegu hizi azijazalisha alizeti vizuri. Hivyo niiombe taasisi hii iendelee kufanya utafiti ili sasa kwa msimu unaokuja maeneo yote yaweze kulima alizeti na tuweze kuzalisha zaidi alizeti katika Mkoa wangu wa Singida, na vile vile ili upungufu wa mafuta uwe ni historia katika nchi yetu katika Mkoa wa Singida…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja.