Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo. Kabla sijaanza, hii ni bajeti ya washikaji zangu, naomba niseme hivyo. Yaani hii Wizara ni ya wazazi, yaani kuna mzazi one, na mzazi two, wanajuana wenyewe Wizarani huko wanavyofanya. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, kwa niaba ya vijana, kwa sababu ni miongoni mwa Mawaziri ambao sisi vijana tunajivunia, kwa hiyo, wanafanya vizuri, yaani mnafanya poa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kwa nini nasema hivyo kwamba wanafanya poa? Ni kwa sababu mwaka 2021 mimi nilichangia wakati tunajadili hii bajeti ya Wizara ya Kilimo na kuna vitu ambavyo nilivishauri hapa na vimefanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani tunaposema wamefanya poa, ni kwa sababu wako hatua moja mbele, wanafikiri tunavyofikiri. Yaani wanafikiri namna ambavyo Watanzania wanaamini kwamba sekta ya kilimo inastahili kupewa heshima inayopewa. Wanafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza kwa sababu kuna mambo wameyafanyia kazi. Jambo la kwanza, nilizungumza mwaka 2021 kwamba muda ambao vijana wetu wanakaa field ni mfupi sana, yaani kijana ili awe ame-master vizuri kabisa sekta ya kilimo akitoka Chuo, Waziri amezungumza kwamba wanafanya mikakati. Tunaamini, kwa sababu tutawauliza tena; wameongeza muda wa vijana kukaa field mpaka mwaka mmoja. Ni kitu kizuri, kwa sababu ninaamini wanajifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine tulizungumza kuhusu ku-miliaturize sekta ya kilimo. Nilisema kwamba tunatamani, yaani kipenga kikipigwa Wizarani, Maafisa Ugani (extension officers) wanaitikia, mambo yanaenda. Wamefanya vizuri. Wasiwasi wangu, hawa Maafisa Ugani (extension officers) wako chini ya TAMISEMI. Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI sekta zao ni tofauti, lakini hawa ambao Wizara ya Kilimo inatenga fedha nyingi na kuwapa vitendea kazi; na tulishuhudia pale, wamepewa vifaa vya kupimia udongo, wamepewa usafiri, wamepewa vitu vingi na ni kitu kizuri, na walikuja tukawaona lakini wako sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge, tumsaidie Mheshimiwa Waziri kuhamisha extension officers (Maafisa Ugani) warudi kwenye mikono ya Wizara ya Kilimo. Kwa sababu pale, mwenye uchungu na hizi fedha, kwa sababu tunasifia wote kwamba fedha ya kwenye Wizara ya Kilimo imeongezeka, lakini hatutaona tija, kama watu ambao tunaamini ndio askari wetu hatuna mandate nao, yaani Wizara ya Kilimo haina mandate na Afisa Ugani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, niwakumbushe, pamoja na kwamba tunasema bajeti ya Wizara imeongezeka na tunajua imeenda kwenye umwagiliaji na sehemu nyingine, lakini ikumbukwe kwamba mpaka sasa hivi kwenye upande wa fedha za maendeleo, imetekelezwa kwa asilimia 35.86 tu upande wa miradi ya maendeleo. Kwa hiyo, bado tunasisitiza kupelekwa kwa fedha tunavyopitisha kwenye Bunge hili, kwa sababu mikakati iko vizuri, tunaongea hapa sana lakini fedha hazipelekwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nichangie upande wa pili ushiriki wa vijana wa Taifa hili kwenye kilimo. Bado vijana wanajitahidi kwa kiasi kikubwa sana kupambana na kushiriki katika mnyororo wa thamani kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wanalima, wanachakata, wanafanya kazi za consultation, wako vijana ambao wamejifunza masuala ya kilimo, wanashauri vijana wenzao. Kwa hiyo, tunashiriki kwa kiasi kikubwa, tunajitahidi kushiriki. Hata hivyo, bado tuna changamoto, kuna vijana wako field wana mashamba makubwa, wana greenhouse, wamejiandaa, wako tayari kushiriki kwenye mnyororo wa thamani katika sekta nzima ya kilimo lakini hawapati mikopo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameongea Mheshimiwa Mariam Ditopile hapa, kuna watu kabisa wana kitu, yaani siyo kama labda anachukua mkopo ili akaanzishe, kuna wengine tayari walishaanza, wanatakiwa kuwa boosted tu, lakini ni hizo bureaucracy (urasimu) kupewa mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ili vijana washiriki kwenye kilimo, tulisema tunataka tufanye kilimo kiwe romantic. Nafikiri tunaelewana. Tukifanye kilimo kiwe rafiki, kwa sababu najua vijana ndio hao wa millennials, hutegemei aende akashike jembe la mkono alime. Sasa huwezi kuzungumza ku-romanticize kilimo halafu usizungumze kuhusiana na teknolojia na ubunifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kwenye Taifa letu tuna kituo cha kukuza ubunifu na zana za kilimo cha Arusha CAMARTEC. Hiki Kituo wametengeneza matrekta, mashine za kulimia, mashine za kupanda, wanajitahidi wametengeneza ziko pale, lakini kile Kituo hakina fedha. Hakijapewa fedha kwa ajili ya kuhamisha maarifa yao kupeleka kwa wakulima. Kwa hiyo, wametengeneza vitu vikubwa wamebaki navyo pale kituoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba anatenga fedha kwa ajili ya kuwapelekea kituo hiki waweze kuhamisha ujuzi kutoka kituoni kupeleka kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kumalizia… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia sentensi ya mwisho kabisa hiyo.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna fedha za Benki ya Kilimo zimechukuliwa Shilingi bilioni saba. Mheshimiwa Waziri kuna watu walizungumza, nami naomba nisisitize; tunaomba majibu ya hizo Shilingi bilioni saba kwa sababu zilikuwa za mikopo, vijana wangepata mikopo. (Makofi)