Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika sekta hii nyeti kabisa ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana sana Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo Tanzania. Tumeona Royal Tour ikitikisa Tanzania nzima, tumeona mishahara ya wafanyakazi inazungumziwa kila mahali hapa Tanzania. Lakini kubwa zaidi ni katika bajeti ya kilimo ya mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu ni maajabu makubwa sana na haijawahi kupatakutokea kwa kuwa bajeti ya kilimo imeongezwa kutoka Shilingi bilioni 294 hadi kufikia Shilingi bilioni 751, sawa na asilimia 155. Kwa kweli Mama yetu anafanya kazi kubwa, wote tunapaswa kumpongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nichukue pia nafasi hii kumpongeza kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo pamoja na Mheshimiwa Mavunde kwa kazi kubwa sana wanayoifanya katika sekta hii ya kilimo. Wamekuwa ni wachapakazi lakini si hivyo tu, wamekuwa na ubunifu mkubwa katika kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo. Ninawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nijikite kuchangia katika zao la kahawa. Zao la kahawa limekuwa ni uti wa mgongo kwa Mkoa wa Kilimanjaro. Mkoa wa Kilimanjaro unalima zao la kahawa tangu kabla ya uhuru. Lakini si Kilimanjaro tu, takribani mikoa 15 katika Tanzania inalima kahawa. Ni sawasawa na kwamba nusu ya Watanzania wanalima kahawa. Hivyo ukigusa kahawa umegusa nusu ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha sana kahawa hii ambayo ilikuwa inaiingizia Tanzania pato kubwa kabisa kuliko mazao mengine yoyote limeachwa nyuma na kwa sasa hata ruzuku halipati. Mazao ya korosho, tumbaku na pamba yanapata ruzuku, lakini tunajiuliza ni kwa nini kahawa haipati ruzuku?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ni rafiki yangu sana, lakini leo bila kupepesa macho, nimepanga kuondoka na Shilingi kwenye mshahara wa Mheshimiwa Waziri kama hatatoa majibu ya kujitosheleza ya kwa nini kahawa haipati ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limekuwa ni changamoto kwenye kahawa ni suala la miche. Wananchi hasa wa Kilimanjaro wanahitaji miche bora ya kahawa; ile miche ambayo inaweza kustahimili hali ya hewa ya sasa lakini pia inayoweza kustahimili magonjwa huku ikiendelea kutoa mazao mengi tofauti na ile ya zamani. Mibuni mingi iliyopo katika Mkoa wetu wa Kilimanjaro imezeeka. Leo tunahitaji miche mingine ili tuweze kupata kahawa iliyobora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana Wizara kwa kuwa bajeti ya sasa kwenye uzalishaji wa mbegu imetoka kuanzia Shilingi bilioni 10.58 hadi Shilingi bilioni 43.03, haya ni mapinduzi makubwa sana. kwa hivyo, ninaamini wananchi wa Kilimanjaro Watanzania wote wanaolima kahawa watapata miche bora itakayosaidia zao hili kufika pale lilipokuwa zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la taifa lilikuwa ni kufikia kuvuna tani 300,000 ifikapo mwaka 2025. Lakini mpaka sasa mwaka 2021/2022 tumeweza kuzalisha tani 65,235 ilhali tulikuwa tunalengo la kuzalisha tani 72,000. Hatuwezi kwenda kwa staili hii tukaweza kufika huko tulikokuwa tunataka kwa 300,000. Kwa sababu leo tuko tani 65,235 mpaka tufike tani 300,000 itachukua muda mrefu sana. Kwa hiyo, ninaomba zao hili lipewe kipaumbele, zao hili lipewe ruzuku. Leo tuna maafisa ugani ambao tumeona mmewapa mapikipiki wakafanye kazi kubwa kwenye zao hili pia… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naunga mkono hoja. Ahsante.