Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze katika kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuona kwamba kilimo ndio kipaumbele katika nchi yetu, ukizingatia kwamba wananchi wetu wengi asilimia 60 wanajihusisha na shughuli nzima ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Wizara nimpongeze kaka yangu Hussein Bashe Waziri wa Kilimo pamoja na Naibu Waziri kwa kufanya kazi kubwa kuhakikisha kilimo kinaenda kusonga mbele. Kwa kupitia Mawaziri hawa tulionao nina uhakika kutakuwa na mapinduzi makubwa katika sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, usalama wa nchi yetu unategemea usalama wa chakula na usalama wa chakula unategemea kuwa na mbegu bora na mbegu bora upatikana kwa Serikali yetu kuamua tuzalishe mbegu hapa nchini. Asilimia 45 ya mbegu ya mahindi hutoka nchi za nje, lakini asilimia 95 mbegu ya mboga mboga inazalishwa nchi za nje. Hivyo basi inapelekea tunapokea mbegu ambazo si bora na wakulima wengi wanapopata zile mbegu na kwenda kufanya shughuli za kilimo uzalishaji unapungua siku hadi siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali iwekeze katika utafiti. Tukiwekeza katika utafiti tutawasaidia wakulima wadogowadogo. Sasa hivi wakulima wetu wanafanya kilimo kisichokuwa na tija. Wanalima bila ya kuelewa ardhi hii inastahili kuotesha nini, kwa sababu hawajui udongo ule unafaa kwa zao lipi. Kwa hiyo niombe sana Serikali iwekeze sana katika Vituo vyetu vya Utafiti ili wananchi wetu wapewe elimu kulingana na ardhi iliyopo. Wananchi wetu wapewe elimu kuangalia ni mbegu gani inastahili kuoteshwa katika eneo hilo, tukifanya hivi tutawasaidia wakulima wengi na hatimaye suala zima la kilimo kitakuwa kinapanda siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la utafiti, Vituo vyetu vya Utafiti havifanyi kazi vizuri hii ni kwa sababu kuna kodi kubwa katika vifaa vile vya utafiti. Niiombe Serikali ipunguze au iondoe kabisa kodi katika vifaa vile vya utafiti. Utashangaa sana katika Serikali yetu hata vifaa vinavyoletwa na taasisi za kiserikali vinatozwa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo linapelekea vituo vyetu vya utafiti vinashindwa kufanya kazi. Sasa ni muda muafaka tuelekeze kwenye suala zima la utafiti, nina uhakika tutafanya mapinduzi makubwa katika suala zima la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali kuwekeza katika kilimo cha mbogamboga na matunda (horticulture). Sasa hivi kuna mwamko mkubwa sana kwa wananchi hasa vijana wengi na akinamama, wamepata mwamko mkubwa wa kujishughulisha na shughuli nzima ya kilimo cha horticulture, kwa sababu ni kilimo pekee ambaye unapata matokeo kwa muda mfupi, ni miezi mitatu hadi miezi sita unapata mavuno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwekeza kule, tatizo kubwa lililopo ni kwamba hawana mitaji na hawana vitendea kazi. Naiomba Serikali iwekeze kule ili angalau vijana wengi na akinamama wengi waweze kujiajiri na kukuza mapato yao ili kuendeleza maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niendelee kuipongeza Serikali kwa kuweka msukumo mkubwa katika kilimo cha umwagiliaji. Hii hapa itasaidia sana wananchi kujikwamua kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, si kila jambo litafanywa na Serikali, niiombe Serikali iweze kuondoa kodi katika mitambo ya uchimbaji wa mabwawa ili wananchi wenyewe au wakulima waweze kununua hiyo mitambo na kuweza kujishughulisha na shughuli za umwagiliaji. Ukiondoa kodi katika mitambo ya uchimbaji itapunguza bei kwa asilimia 30 hadi 40. Kwa hiyo tuwasaidie wakulima wetu ili waweze kununua mitambo hiyo na kujishughulisha na shughuli nzima kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufikia hapa naomba niunge mkono hoja. Nashukuru. (Makofi)