Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na mimi nianze kwa kuishukuru sana Wizara hii ya Kilimo kwa mambo kadhaa ambayo yanaendelea kufanyika pia ninaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa nia na dhamira ya dhati ya kuimarisha kilimo tunaiona kwenye bajeti hii na ninaamini tutaona makubwa katika kipindi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani zangu nazielekeza kwa Waziri na Wizara nzima kwa jinsi wanavyoshughulikia suala la chai la Kilolo na ninawataarifu tu wananchi wa Kilolo kupitia Bunge lako kwamba muda siyo mrefu suala la Chai Kilolo litakamilika kwa jinsi ambavyo Wizara hii inalishughulikia na nina imani tutakamilisha suala hilo kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili niendelee kushukuru sana Wizara hii kwa jinsi inavyoshughulikia suala la kilimo cha parachichi na uanzishwaji wa kitalu cha miche ya parachichi katika Wilaya ya Kilolo. Hapa nimtaje Dkt. Mkamilo wa TARI ambaye amefika kule na tayari kitalu kile kimeshaanzishwa na tunatarajia kupata miche ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapokuwa hapa kwenye eneo la parachichi watu wa Kilolo tumejipanga na tunajua sasa Kilimo kinaendelea lakini changamoto ndogo tuliyonayo wanaolima sasa hivi siyo wananchi wakawaida wengi wanaolima ni wakulima wenye mashamba makubwa kidogo. Sasa hapa ninapendekezo la block farming kwa wakulima wadogo nitakuomba sana Mheshimiwa Waziri upokee pendekezo hili la Vijiji 25 ambavyo wakulima wadogo wadogo wataanza kulima eka moja moja na sisi tutafuta namna nzuri ni eka moja hadi tano lakini tutafuta namna nzuri ya wakulima hawa kuweza kupata farm input lakini kila block itakuwa na zaidi ya eka 50 mpaka 100 kwenye shamba moja. Kwa hiyo, tunalo hili pendekezo tutakukabidhi Vijiji 25 tuanze navyo kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo wa parachichi ili tusiwaache nyuma wananchi wa Kilolo halafu wawekezaji wengine wakaja wao wakabaki vibarua. Nitaomba nikukabidhi kwa ajili ya kulifanyia kazi na wewe nitakuomba unipe Afisa ambaye nitakuwa nafuatana naye ili hili liweze kutekelezeka na unaijua ufuatiliaji wangu na hili nalo nitakusumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba pia Mheshimiwa Waziri kuhusu skimu chache ambazo zimetajwa kwenye bajeti ya mwaka jana, skimu ya Mgambalenga imetengewa shilingi bilioni moja lakini mpaka leo kwenye Tume ya Umwagiliaji ukiangalia kwenye randama ukurasa wa 52 utaikuta, bilioni moja ilitengwa na mpaka leo haijatolewa hata shilingi, ninakuomba kwa kipindi hiki kilichobaki skimu hii ipate basi hela hata kidogo ili ianze kutengenezwa ianze kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru nimeona skimu ya Nyanzwa imetajwa kwa ajili ya tathmini ya mazingira. Nimesoma ukurasa wa 82 mpaka 84 wa randama nikaona chini kuna kujenga skimu 14 na hazijatajwa. Kwa hiyo, kwa sababu tathmini yamazingira inafanyika Nyanzwa na pale chini kuna skimu 14 zitafanyika ukurasa 82 hadi 83 wa randama, naomba Nyanzwa iwemo mojawapo kati ya zile 14 ambazo nimeziona pale kwenye randama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ambalo ningependa kuliongelea hapa, Mheshimiwa Waziri umesimama hapa mara nyingi sana kukemea suala la lumbesa, watu wa kule tunalima mboga mboga horticulture, nakukumbusha kwamba korosho inapimwa kwa kilo huwa aina lumbesa, kawaha inapimwa kwa kilo huwa aina rumbesa, pamba inapimwa kwa kilo huwa haina lumbesa. Sasa tuje kwetu vitunguu tunavyolima vina lumbesa, nyanya tunazolima wanajua wenyewe wananvyopanga, tuje viazi vina lumbesa, mazao yote ya mboga mboga yana lumbesa, umekemea mara nyingi hapa kama imeshindikana itungwe sheria mahsusi ya vipimo vya mazao ya kilimo ili wale wananchi waweze kunufaika na kilimo chao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni kulikuwa na zao la pears, matunda tu ya kawaida na nilifika kule Kijiji kimoja cha Ilamba, tenga moja ni kama matenga matatu, mtu anaweka mpaka atakapoamua mwenyewe ni Shilingi Elfu Kumi, lakini ni kwa sababu hakuna kipimo madhubuti kinachotumika kupima yale mazao. Ninakuomba sana pamoja na kukemea huko bado tatizo hili ni kubwa, ninakuomba tuangalie namna gani tutawakomboa wakulima wanaolima mazao ya mboga mboga ili na wao waweze kujikomboa kama haya mazao mengine yalivypata ufumbuzi kwenye suala zima la lumbesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)