Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kupata nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, niungane na wenzangu wote kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya kwa ajili ya nchi yetu. Tanzania inaona na dunia inaona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake, kazi yao ni nzuri na wametuletea bajeti yenye matumaini makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yuko mdau mmoja wa mambo ya uchumi alikuwa akizungumza juzi juzi kwamba utajiri uliyoko juu ya ardhi ni mkubwa kuliko ulioko chini ya ardhi. Utajiri ulioko juu ya ardhi ni katika maana ya kilimo na ulioko chini ya ardhi katika maana ya madini. Kinachokosekana tu ni uwekezaji. Kwa uchumi kama wa kwetu ambao unategemea wakulima wadogo, kilichokuwa kinakosekama ni kile ambacho kipo kwenye ukurasa wa 14 wa Hotuba ya Bajeti ya Waziri kuongeza nguvu kwenye utafiti, kuongeza nguvu kwenye ugani, umwagiliaji na ubora wa mbegu. Yakitekelezwa haya kama Mheshimiwa Waziri alivyotuletea, basi nadhani maneno haya ya mdau huyu yatatimia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Mwanga maeneo yote ya milimani yalikuwa yakitegemea zaidi uchumi wa kahawa ambao hapo katika ulidorora kidogo kutokana na matatizo haya ya ugani pengine na masoko, lakini sasa hivi ari kubwa ya kahawa imerudi. Tunachoiomba Serikali ni kupatiwa mbegu tu, yaani miche ambayo inahimili hali ya kule milimani ambayo pia haihitaji dawa nyingi kwa ajili ya kukua na kustawi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninazo skimu tatu kubwa za umwagiliaji. Kwanza ni Skimu ya Kirya ambayo nashukuru sana kwamba tulipata fedha inaendelea. Potential ya ile skimu ni hekta 1,600, lakini Mkandarasi aliyeko site akikamilisha tutaweza kutumia hekta 950. Tunashukuru na tunaamini tutaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, skimu ya pili ni ya Kivulini Kileo ambayo ina potential ya hekta 1,550, lakini zinazotumika ni hekta 712. Tunaomba tupatiwe fedha ya kumalizia ili skimu hii ifanye kazi kwa asilimia 100. Pia tupatiwe maghala na mashine za kukaushia mpunga. Kwa sasa hivi wanaanika nje, hali ambayo haileti ubora mzuri wa mpunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, skimu yetu ya tatu ni Skimu ya Kigonigoni. Mheshimiwa Waziri nakushukuru, ulipokuwa Naibu Waziri ulikuja Kilimanjaro ukanipa breakfast pale Kili Wanders, nami sikulipa, ni wewe ulilipa, nakushukuru sana. Ukanishauri juu ya Skimu hii ya Kigonigoni kwamba tutafute fedha tufanye upembuzi yakinifu. Tulifanya hivyo na hiyo kazi imefanyika, sasa hivi wako kwenye designing. Ile skimu ina potential kubwa sana ya hekta 2,300.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba Mheshimiwa Waziri ni kwamba tutakapokamilisha upembuzi yakinifu hivi karibuni, basi tusaidiwe fedha kupitia kwa wadau wa maendeleo kama IDF na JICA tusije tukasubiri tena bajeti ijayo. Naamini kabisa tutakamilisha upembuzi yakinifu ndani ya muda kwa sababu umetupa kijana mzuri sana, Eng. Said pale Mkoa wa Kilimanjaro. Tunachoomba tu ni kwamba aongezewe nguvu hasa manpower kwa sababu wataalam pale ni wachache na wanakimbiza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili ya muda, naomba nimalizie mchango wangu hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja.