Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngorongoro
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru pia kwa kunipa nafasi kuchangia kwenye Wizara hii ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika na Mheshimiwa Waziri, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa upendo wake kwa Watanzania kwa kukubali kutenga fedha nyingi kwa ajili ya Wizara hii ya Kilimo. Kama tunavyojua, kilimo kimewaajiri Watanzania wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na watendaji wote kwenye Wizara hii. Ni wasikivu sana. Jana tu nilikuwa na tatizo kwenye Jimbo langu lakini nimemplekea Mheshimiwa Waziri na watendaji wake, wameshafanyia kazi. Hawa ni watendaji, ni watumishi wa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana bajeti hii, kutoka Shilingi bilioni 294 mpaka Shilingi bilioni 751 ni ishara kwamba tumeamua sasa kuwakwamua wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kitu kimoja. Kwenye Wilaya ya Ngorongoro kuna maeneo mengine ambayo sasa hivi tunatafuta namna ya kupata maji, lakini sisi kwenye Kata za Pinyinyi, Oldonyosambu, Digodigo na maeneo mengine kama Engaresero, Enguserosambu kuna maji ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotakiwa ni kuweka miundombinu kwa ajili ya wananchi wetu kuanza kunufaika na mfumo wa umwagiliaji. Tukijaribu kuangalia kwa mfumo wa sasa hivi wa dunia, watu wengi wamekwenda kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kwa nini, na nchi nyingi, kwa nini wameamua kwenda? Ni kwa sababu kilimo cha umwagiliaji ndicho kilimo cha uhakika kuliko kilimo cha kutegemea mvua. Tukichukulia mfano mwaka huu, watu gani wana uhakika wa kuvuna ni watu wanaotegemea kilimo cha umwagiliaji. Kwa sababu kwa wale wanaotegemea kilimo cha mvua wengi wamepata hasara hakuna mvua za kutosha. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuamua sasa kuangalia katika mfumo huu wa irrigation system ambao utakwenda kuwakwamua Watanzania wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri, kwenye Wilaya yetu ya Ngorongoro wananchi wanapata hasara sana kwa sababu hawana hata ghala moja kwa ajili ya kuhifadhi chakula kipindi cha mavuno. Inawabidi wauze mazao yao kwa bei ya hasara; kwa sababu hawana namna ya kuhifadhi. Kwa hiyo, nikuombe kwenye Wilaya yetu ya Ngorongoro kaangalie kwenye mifuko yako yote, chonde chonde utupe angalau ghala moja kwa ajili ya wananchi kuhifadhi chakula chao. Kila mwaka sisi tumekuwa tukiuza chakula, mahindi kwa Wakenya kwa sababu hatuna maeneo ya kuhifadhi, na wao wanatumia opportunity hiyo kuja kununua chakula mpaka mashambani; ni lazima tuwalinde wakulima wetu namna ya kunufaika na kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine niombe tupeleke mbolea pia. Ukienda leo Kata ya Pinyinyi, ni eneo ambalo tukiamua kuwekeza tutazalisha mbegu nyingi sana. Sasa hivi Kampuni ya Kibo Seeds wanawapa wakulima mbegu za alizeti na bamia wanazalisha halafu wanawapa bei wanayotaka wao. Lakini Serikali pia tunaweza kuzalisha mbegu katika eneo lile, ukienda kwenye Kata ya Oldonyosambu tunaweza tukatumia maji yaliyopo kwaajili ya wananchi kunufaika. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri tuwasaidie wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niomba kitu kingine, kuna tatizo la emergence services kwenye Wizara ya Kilimo pia. Mwaka huu mwanzoni mwezi wa tatu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: …wananchi walipata shida sana. Nashukuru sana niunge mkono hoja.