Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tumbatu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwako kwa kinipatia nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya Makadirio na Mapato ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, aidha nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wake wote kwa kutayarisha na hatimaye kuiwasilisha hotuba hii katika Bunge lako tukufu kwa ufasaha na umakini mkubwa.
Mheshimiwa Spika, katika kuchangia hotuba hii napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo; kwanza ni upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, kilimo ni uti wa mgongo kuelekea uchumi wa wakulima wetu. Serikali yetu inaendelea kutilia mkazo wananchi kujishughulisha na kilimo. Lakini kilimo chenye tija ni lazima kiandaliwe kwa kuwapatia wakulima wetu pembejeo za kilimo kwa wakati. Mpaka sasa kuna baadhi ya maeneo katika nchi yetu huwa wanasumbuka, aidha kutopata pembejeo kwa wakati au kukosa kabisa kwa baadhi ya miongo.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali katika jambo hili la pembejeo ni kuhakikisha wakulima wetu wanapata pembejeo hizi kwa wakati na kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Spika, pili kuwawezesha wakulima wadogo wadogo; wakulima wetu wengi katika nchi yetu ni wanyonge sana. Uwezo wao wa kujiendesha kiuchumi ni mdogo sana. Wakulima wetu wanashindwa hata kuanza kilimo kwa sababu ya unyonge. Hivyo basi ni lazima Serikali yetu iwaunge mkono katika kilimo chao. Wengi huwa wanakimbilia kwenye mikopo ambayo baadae huwa wanashindwa hata kurejesha mikopo hiyo kutokana na masharti magumu. Riba kwenye mikopo ni miongoni mwa vihatarishi vikubwa kwa wakulima wetu.
Ushauri wangu katika suala hili la riba kwa mikopo ya wakulima ni Serikali kudhibiti kabisa viwango vya riba kwenye mabenki yetu ili kuondoa kabisa vihatarishi vinavyopelekea kufilisiwa kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Spika, tatu ni kuhusu kilimo cha umwagiliaji; mabadiko ya hali ya hewa ulimwenguni yanaathiri mwenendo wa kilimo kwa kutegemea mvua. Nchi nyingi pamoja na Tanzania hivi sasa zinapata mazao hafifu kwa kutegemea mvua. Wengi wanaelekea kwenye matumizi ya kilimo cha umwagiliaji.
Ushauri wangu kwenye jambo hili ni Serikali iendeleze mikakati ya mpango wa kilimo cha umwagiliaji kwa kueneza scheme za kilimo kwenye maeneo yote nchini. Pia Serikali iendeleze zoezi la kuwa elimisha wakulima wetu faida za kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.