Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu katika bajeti hii nyeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma na kupitia nafasi hii napenda nimpongeze sana Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuitazama na kuiongeza bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara Bwana Faraji Mnyepe na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeho, mzalendo, mchapakazi na wasaidizi wake, makamanda na wanajeshi wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi wana mgambo hawa ni wakubwa sana kwetu maana sisi wale ma-private soldier ndio wamekuwa wakitufundisha sisi wana mgambo. Kwa hiyo, leo nilipoona makamanda hawa nilikuwa nasema sasa sijui nitoe mchango wangu nikiwa nimebana mikono sasa, lakini kwa ujumla naonesha tu kwamba utii mkubwa sana kwa makamanda hawa ambao wanafanya kazi nzuri ya kizalendo kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitaanza na suala la doria kwenye mpaka wa maji wa DRC na Tanzania. Hali ya mipaka yetu kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Waziri ni nzuri, mpaka wetu sisi na Burundi ambao tuko kule Kigoma na mpaka wetu sisi na Kongo ni nzuri sana. Isipokuwa yamekuwepo matukio katika Ziwa Tanganyika ambayo yamekuwa yakijitokeza na haya sio matukio ambayo unaweza ukasema ni ya kivita, hapana, ni matukio ya maharamia tu wa ziwani ambao wengine wanatoka nchi jirani, wanakuja maharamia hawa wana silaha wengine walikuwa kwenye majeshi ya nchi hizo huko zamani basi wanakuja wanachukua nyavu, mashine za wavuvi wetu na wanaondoka nazo. (Makofi)
Kwa hiyo, katika nafasi hii ningependa kuomba kupitia bajeti hii kwamba jeshi letu liongeze doria katika Ziwa Tanganyika ili kusaidia wavuvi na wasafiri wengine katika mpaka wetu huu wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa niliseme ni suala la fidia. Nakumbuka eneo la Kibirizi kule Kigoma jeshi letu kupitia kikosi cha 24KJ kimeongeza eneo lake na katika kuongeza eneo lake, kimechukua maeneo ya raia na wale raia hawana tatizo wamekubali na wako tayari kulipwa fidia. Lakini sasa tunakwenda mwaka wa tatu hawajalipwa fidia na hawawezi kuendeleza maeneo yale, wanataka fidia ile ikawasaidie kujenga maeneo mengine na kupata makazi bora.
Mheshimiwa Spika, ningeomba katika bajeti hii muwatazame wananchi hawa waliotoa maeneo yao kwa ajili ya jeshi, ili waweze kulipwa fidia na kwenda kuendeleza maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninge…
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Naona mchangiaji kama anasikitika, nilishawaambia Wabunge taarifa muda unaohusika ni wa yule mchangiaji mwenzio, Mheshimiwa Saashisha Mafuwe.
T A A R I F A
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, mimi nilitaka kumpa taarifa ndogo tu kaka yangu pamoja na mchango mzuri, nchi hii kuna maeneo mengi sana yamechukuliwa na jeshi ikiwemo eneo la Kigamboni Amani Gomvu, wananchi wamechukuliwa eneo muda mrefu, lakini jeshi hawajasema chochote hawajalipa fidia na hawajatoa msimamo wao. Nilitaka kumpa hiyo tu. (Makofi)
SPIKA: Haya mafunzo mtakuwa mnapeana wenyewe mkikutana kantini. Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda. (Makofi/Kicheko)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwanza taarifa naipokea kwa manufaa ya Taifa sio kwa manufaa ya eneo nililokuwa nachangia.
Mheshimiwa Spika, nimalizie hoja yangu kwa jambo dogo sana ambalo ningependa ndugu zangu na hasa kwenye jeshi walielewe vizuri. Kuna vijana hawa wanaoingia katika jeshi iwe JKT, iwe Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, wanachukua mazoezi wanaimba nyimbo zao wakati wa mazoezi. Mimi ningeomba maana kuna nyimbo zingine tumekuwa tukizisikia sasa hivi ukisikia tu wimbo ule unawaambia mabinti zako ingieni ndani mkae mara sijui fulani wewe, nilikusubiri sana nikalala mlango wazi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwani hakuna nyimbo za kizalendo mimi naomba sana turudishe nyimbo za kizalendo kwenye jeshi. Nyimbo za kusifia waasisi wa Taifa letu, nyimbo za kumsifia Amiri Jeshi Mkuu, nyimbo za kumsifia Mkuu wa Majeshi kama Jenerali Mabeho anavyofanya kazi vizuri, nyimbo za kulinda mipaka yetu, tuachane na hizi nyimbo ambazo ukizisikia tu unaona hawa vijana… (Makofi/Kicheko)
SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: ... mawazo yao yote yako kwenye ngono. Ahsante sana, nashukuru sana. (Makofi)