Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, niungane na wenzangu kuipongeza sana Wizara hii chini ya uongozi mahiri kabisa wa Mheshimiwa Nape Nnauye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada kubwa sana ambayo Wizara hii inafanya katika kuhakikisha kwamba inaimarisha upatikanaji wa huduma wa mtandao wa internet bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma ya internet hususani katika maeneo ya pembezoni kama vile Kigoma, Kagera, Mtwara, Lindi, Tanga pamoja na Mikoa ya Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kutambua hilo, napenda kuishauri Wizara itambue mbinu mbadala ya kufikisha huduma ya internet Vijijini ikiwemo na Mikoa yote ya pembezoni. Na njia hii ni kutumia community networks. Nchi za wenzetu kama Uganga, Kenya, Zimbabwe, Afrika Kusini wamenufaika sana kwa kutumia community networks kufikisha huduma ya internet kwenye shule pamoja na Vituo vya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu kabisa, ningependa kuiomba Wizara kufanya mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, chini ya TCRA Wizara itambue kundi hili la community networks.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, chini ya TCRA Wizara itambue kundi hili la community networks. Jambo la pili, Wizara ipunguze gharama za Bendipana kwa community networks (broadband costs). Jambo la tatu, Wizara iondoe co-location fee kwa community networks. Yaani unakuta community networks wakitaka kuweka vifaa vyao kwenye minara ya UCSAF wanachajiwa gharama. Kwa hiyo, Wizara iondoe gharama hiyo kabisa kwa ajili ya community networks pale ambapo watataka kuweka vifaa vyao kwenye minara ya UCSAF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, Wizara itoe msamaha kwa hizi community networks kuchangia katika kapu la Mfuko wa Mawasiliano yaani UCSAF kwa sababu kimsingi community networks hazifanyi biashara, kimsingi community networks zinatoa huduma ya kijamii ili kuwezesha shule pamoja na vituo vya afya vya vijijini na mikoa ya pembezoni iweze kuunganishwa na huduma ya internet. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la pili, naipongeza sana Wizara pamoja na UCSAF kwa kazi kubwa inayofanya ya kuimarisha mawasiliano hapa Tanzania. Pamoja na hayo, naomba niseme kwamba, wakazi wa Bukoba Mjini, Mkoani Kagera wanapata shida kubwa ya mawasiliano yasiyokuwa na uhakika hususan upatikanaji wa mtandao. Naweza nikasema katika kati ya Kata 14 za Bukoba Mjini, Kata nane za greenbelt zinapata changamoto kubwa ya mtandao wa uhakika; Kata hizi ni Buhembe, Nyanga, Kahororo, Nshambya, Ijuganyondo, Kagondo, Kibeta na Kitendagulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa kabisa, ningependa kumwomba Mheshimiwa Waziri, baada ya Bunge hili la Bajeti afike pale Bukoba Mjini ajionee kero kubwa ya mawasiliano ambayo tunaipata. Hapa ningeomba atakapokuja na dada yangu jembe kabisa Mkurugenzi Mtendaji wa UCSAF, dada Justina na yeye afike, aone namna gani ambavyo atatusaidia kuimarisha mawasiliano pale Bukoba Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka, naendelea kuipongeza Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye anuani ya makazi. Hata hivyo, jambo hilo la anuani ya makazi linaleta changamoto kubwa ya kiusalama, usalama wa taarifa zetu binafsi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aharakishe utaratibu wa kuleta Sheria ya Data Protection hapa Bungeni ili tuweze kuipitia na kuipitisha ili kulinda taarifa zetu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa natambua zipo Asasi za Kiraia ambazo zimeshaanza mchakato huu, kwa mfano, Jamii Forum na wengine na tayari ipo rasimu ambayo imeandaliwa. Kwa kazi iliyobaki ni ndogo, Wizara ichukue jitihada ambazo zimeshaanza ilete Sheria ya Data Protection hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni mtumiaji mkubwa sana wa mitandao ya kijamii, naamini anaona namna gani ambavyo wanawake wanasiasa hususan Wabunge wanawake tunavyopitia ukatili mkubwa wa kijinsia mtandaoni. Jambo hili lipo kwenye Wizara yake, nimwombe Mheshimiwa Waziri atafute namna ya kutulinda kwenye mitandao ya kijamii; kwanza kwa kuhakikisha kurasa zetu za mitandao zinapata verification ili kutuondoa katika hatari ya kudukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nashukuru sana. (Makofi)