Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yangu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, pia ninampongeza Waziri Kaka yangu Mheshimiwa Nape Nnauye kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, bila kusahau Naibu Waziri ambaye kimsingi mimi kama Mbunge wa Jimbo la Msalala kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala na hasa Kata ya Jana, Kata ya Mwaruguru ndio Naibu Waziri wa kwanza kufika kwenye maeneo haya. Kwa hiyo, nakupongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo umekuja kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani nizungumzie habari ya mawasiliano katika Jimbo langu la Msalala na Naibu Waziri nadhani kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, alifanya ziara kwenye Jimbo langu la Msalala kuona hali ya mawasiliano katika maeneo yale. Ni kwamba katika Jimbo la Msalala hali ya mawasiliano ni mbovu sana, minara hakuna, hata kwenye Makao Makuu yetu ya Halmashauri bado Watendaji wanapata taabu sana wnapoenda ku-load document inabidi sasa wasafiri waende Manispaa ya Mji ili kuweza kufanya kazi zao za kimawasiliano. Naibu Waziri aliagiza na akaahidi kwamba atatupatia minara Saba na wananchi wanasubiri na niombe sasa Mheshimiwa Waziri unapokuja kufanya winding up hapa, utueleze ni lini sasa hiyo minara saba ambayo mlitupatia ambayo itakwenda kujengwa kwenye Kata ya Jana, Kata ya Mwaruguru, Kata ya Mwanase bila kusahau Kata ya Lunguye, Kijiji cha Nyangarasa na Kijiji cha Busolega na Kijiji cha Nyamishiga. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
T A A R I F A
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampa taarifa mwongeaji kwamba eneo la Halmashauri ya Msalala pia linafanana sana na Halmashauri ya Ushetu, hata Makao Makuu ya Halmashauri ya Ushetu hakuna mawasiliano kabisa. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Iddi, unapokea taarifa?
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa hiyo basi nimuombe Waziri tu aweze kuona aipe kipaumbele Wilaya ya Kahama katika Halmashauri hizi, kwa maana ya Halmashauri ya Ushetu lakini special kwenye Halmashauri ya Msalala kwa sababu Halmashauri ya Msalala ndiyo key ya Majimbo yote haya mawili kwa maana ya Jimbo la Ushetu na Jimbo la Kahama Mji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninakuomba utakapokuwa unafanya winding up hapa uje utueleze ni lini sasa hawa Wakandarasi watakwenda kuanza kazi ya kujenga minara katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu ili uchumi uweze kukua na hasa katika maeneo yetu ambayo tunatoka katika maeneo ya madini, watu wanahitaji kufanya biashara kila siku hivyo wanahitaji mawasiliano, jana nili-share picha moja nikimuonesha bwana mmoja katika Mgodi wa Nyamishiga Kata ya Runguya, ametengeneza kiti kimoja kirefu sana na amekaa juu na watu wamepanga foleni akiwahudumia kupitia simu yake. Hivyo ni kuonesha dhahiri kwamba bado huduma za mawasiliano katika maeneo hayo hazijafika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kuzungumzia habari nzima ya maslahi ya Waandishi wa Habari. Kila mmoja wetu hapa anafahamu kwamba kazi kubwa ambayo inafanywa na waandishi wetu hawa wa Habari; na sisi kama Waheshimiwa Wabunge lakini Viongozi mbalimbali huwatumia hawa waandishi wa habari katika kufanya kazi zetu katika maeneo yale, lakini bado Waandishi wa Habari hawa wamekuwa hawana mikataba ya kudumu. Mheshimiwa Waziri ninakuomba nenda kawalinde waandishi wetu wa habari wanafanya kazi kubwa sana, maslahi yao bado ni madogo mno Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kwamba kwenye msafara mmoja unaweza kukuta una Waandishi wa Habari mathalani 20 na wanafanya kazi kubwa kweli, kila unapokwenda wao ndiyo wa kwanza kushuka na wao ndiyo wa kwanza kukimbia kurudi kwenye magari na mwisho wa siku baada ya hapo Mheshimiwa Waziri wanaishia kupewa Shilingi 20,000, Shilingi 30,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri hebu nenda sasa mkaweke mfumo wa kuwalinda hawa Waandishi wetu wa Habari waweze kuwa na mikataba ya kudumu lakini pia waweze kulipwa stahiki zao kwa muda. Nilikufuatilia siku moja alipofariki Mwandishi mmoja wa Habari, ulitoa maelekezo aweze kulipwa haki zake, lakini mpaka ninapozungumza hivi bado hajalipwa haki zake. Kwa hiyo, ninakuomba Mheshimiwa Waziri Waandishi wa Habari hawa ndiyo wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba, wanatangaza mema yote yanayofanywa na Serikali yetu hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie nizungumzie suala zima la bando. Kuna wizi unaendelea kwenye suala zima la bando, ni kwa nini Mheshimiwa Waziri msitusaidie kwa sababu ukiangalia kilio kikubwa cha wananchi kwa sasa ni bando. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii unakwenda kujiunga bando mathalani ya Shilingi 30,000 na wanakuambia kabisa utapata dakika kwa mfano, 2,500 lakini utapata GB 12, lakini kutokana na hali ya uchumi unajitahidi sasa kujibana uweze kutumia dakika zile vizuri lakini hivyo hivyo unajitahidi kubana utumie MB vizuri, lakini mwisho wa siku inapofika siku 30 hujui zile dakika zimekwenda wapi? Sasa nikuombe utakapokuja kufanya winding up hapo utueleze, hizi dakika ambazo tunazilipia ambayo ni haki yetu ya msingi tumezilipia huwa zinakwenda wapi? Either ni Serikalini au zinakwenda wapi, tufahamu sasa hizi dakika zinazochukuliwa zinakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo ahsante sana, mchango wangu mimi ni mfupi sana kwa siku ya leo. (Makofi)