Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi kuchangia katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya na hasa katika uendeleza sekta hii ya ujenzi na uchukuzi na kuhakikisha kwamba miradi yetu yote inaendelea kutekelezwa kwa speed kubwa na kuhakikisha kwamba hakuna mradi unaosimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite katika maeneo kama manne; nitaongelea barabara katika Jimbo langu la Nkenge, Wilaya ya Misenyi, nitaongelea uwanja wa ndege wa Kajunguti, lakini nitaongelea maboresho ya TPA na mwisho nitamalizia na TRC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri Profesa Makame Mbarawa kwa ziara za mara kwa mara katika Jimbo la Nkenge, Wilaya ya Misenyi. Si muda mrefu ulikuwa kule kukagua ujenzi au maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Kitengule, lakini si wewe peke yako umetuma wasaidizi wako Engineer Kasekenya amekuja na ninafikiri na Mheshimiwa Mwakibete yuko safarini kuja tena. Lakini Mheshimiwa Waziri nikushukuru pia ulipotembelea pale ulituahidi kilometa 25 kutoka pale Kibaoni Bunazi kwenda mpaka pale Kagera Sugar. Mimi nakupongeza sana na wana Misenyi wanakushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Misenyi inazo barabara sita ambazo zinahudumiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na zenyewe barabara ya kwanza ni Katoma - Bukwali ambayo inatuunganisha na nchi ya Uganda, lakini barabara ya pili ni Mutukura kwenda Minziro ambayo ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, lakini barabara ya tatu ni Kasambia - Nyabihanga kwenda mpaka Minziro tena, lakini barabara ya nne ni Kibaoni kwenda Kagera Sugar mpaka Kakunyu, lakini tunayo barabara ya tano ambayo ni Kyaka kupitia Katoro kwenda Ibwera kwenda mpaka Kanazi hiyo ni barabara ambayo inaunganisha Jimbo la Nkenge na Jimbo la Bukoba Mjini kwa wajomba wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi nishukuru kwamba zimekuwa zikitengenezwa katika kipindi cha mwaka kwa utaratibu wa periodic maintenance ambazo zimekuwa zikipitika, lakini niombe kusema katika eneo la barabara ya Kyaka - Katoro kwenda Ibwera mpaka Kihetema imekuwa ikifanyiwa usanifu na nimeambiwa kwamba usanifu umekamilika, lakini nimwombe Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake hii barabara sasa imefikia wakati kuanza kutengenezwa kama ahadi inavyosema ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunayo barabara ambayo aliahidi Mheshimiwa Rais ya Mutukura kwenda mpaka Minziro, nisikitike kusema kwamba kila siku tulikuwa tukiahidiwa kwamba barabara itaanza kutengenezwa na Mheshimiwa Waziri umetuma msaidizi wako Engineer Kasekenya amefika pale na nafikiri alifungashiwa na senene akaja nazo, lakini mpaka leo hatuoni matokeo yanayoendelea pale. Wananchi kule hawaelewi, wanasema viongozi wetu ni kweli wanatupenda wanakuja kwenye ziara lakini mbona hatuoni matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msisitizo mkubwa niongelee barabara ya Katoma kwenda Bukwaya, barabara hiyo ilianza kujengwa kwa kiwango cha lami mwaka 2011. Mpaka leo ni kilometa saba tu ambazo zimejengwa barabara hiyo ina urefu wa kilometa 39.8 kila mwaka tunapata mita 500, mita 800 nikangalia hesabu za mita 500, mita 800 maana yake tunachukua miaka 50 kukamilisha hiyo barabara.

Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wako tunaomba Wanamisenyi muwaangalie kwa jicho la pekee, barabara ziko nyingi ambazo tungeomba ziendelee kujengwa kwa kiwango cha lami lakini hata moja ambayo imeanza mwaka 2011 miaka karibu 12 kilometa saba. Mimi naomba kwa kweli Serikali sikivu ya Mheshimiwa Mama Samia ione kwamba Wanamisenyi wanahitaji hiyo barabara, imalizike sasa ili tuweze kwenda katika barabara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi kubwa wanazozifanya wataalam wetu wa mkoa tunaye Meneja wetu wa Mkoa Engineer Sanga Msangi, lakini na msaidizi wake Engineer Ntuli, wanafanya kazi nzuri, wanawasiliana na mimi vizuri, lakini shida ni uwezeshaji. Leo katika mwaka huu katika bajeti tunazo mita 800, na nimeona katika ukurasa wa 352 umeniwekea kilometa 1.5; Mheshimiwa Waziri wewe unatengeneza mabarabara makubwa kilometa nyingi sana kwa nini hiyo kilometa 1.5 mita 800 mpaka miaka 50 wote hatutakwepo mimi na wewe ndio barabara itakamilika. Nikuombe sasa leo katika bajeti hii angalau tenga nusu kilometa 17 mwaka ule unaokuja kilometa 17 tunamaliza tunahamia barabara nyingine. Mimi nakuamia Profesa na haujawahi kushindwa kwa hiyo naamini utalitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niongelee ujenzi wa uwanja wa Omukajunguti; kwa nia njema Serikali iliona kuna haja ya kujenga Kajunguti International Airport na uwanja huu mahususi ulikuwa ni kwa ajili ya kuhudumia nchi za Maziwa Makuu ya Afrika nchi kumi, tunayo Malawi, Zambia Msumbiji, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania lakini katika eneo hili ilikuja likaainishwa eneo, wananchi wakazuia kuendeleza na wananchi wakatulia kwa upendo mkubwa wakijua kwamba tunaletewa uwanja wa ndege, uwanja wa ndege huu ukainue uchumi wa Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mkoa wa Kagera tukiangalia GDP yetu tuko wa mwisho katika mikoa yote 26 ni kwa sababu hatuna miundombinu na mawasiliano ya kuweza kusafirisha bidhaa zetu, kuuza ndani ya nchi na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Waziri hata jirani yako Mheshimiwa Waziri Ndaki hapa anajua kwamba Mkoa wa Kagera ndio una ranchi kubwa za mifugo. Kwa hiyo tunao ng’ombe, lakini ng’ombe hao hawana thamani leo kwa sababu hatuwezi kufanya export, hatuwezi kuanzisha viwanda, hata mwekezaji wetu wa kiwanda aliyepo pale Karagwe kwa ndugu yangu Bashungwa ameshindwa kuendelea kwa sababu hana jinsi ya kusafirisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana uwanja huu ni wa muhimu sana kwa ajili ya kuhakikisha unainua uchumi wa Mkoa wa Kagera; tuuze, tuanzishe viwanda vya kusindika mazao mbalimbali, tunalima vanilla, tunalima maparachichi, lakini wananchi wanakata tamaa kwa sababu hawana jinsi ya kusafirisha maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo niombe kusema kwamba tunao uwanja kweli wa Bukoba ambao unaendelea sasa hivi, lakini uwanja huo ukiangalia runway ile ni kilometa moja na nusu, na ninyi ni mashahidi mnajua specification za ndege; Bombadier Q400 minimum runway ni kilometa 2.2 watu wote shuhudia na Mheshimiwa Waziri ukitua Bukoba rubani wako anavyoshika break ni tofauti anaposhika kwenye sehemu nyingine ila tunaendelea kuvumilia tukiwa na tumaini sasa Omukajunguti inakuja kujengwa ili sasa iwe ni suluhisho kwa wananchi wa Misenyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuponge juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali hasa upande wa uboreshaji wa bandari yetu, tumeona kwa kweli gati zimejengwa sana meli zinaendelea kuja kushusha mizigo, ni maendeleo makubwa na lazima tusifie Serikali yetu kwa sababu yanayofanyika tunayaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hayo tu niipongeze Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kuna eneo ambalo lilikuwa pale karibu na bandari yetu la EPZA ambalo lilikuwa linasababisha magari yanayoingia bandarini na kuzuia wananchi wanaoenda Kigamboni, huwa inaleta foleni kubwa na kudololesha huduma zinazotolewa pale bandarini, lakini Serikali ya Mama Samia imetoa eneo hilo kwenda katika uongozi wa bandari yetu na hivyo limetengwa katika umahususi kuweza kutunza baadhi ya makontena na shughuli zingine. Kwa hiyo niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini pia nimpongeze Mkurugenzi Erick kwa kazi nzuri pamoja na timu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi niongelee pia TRC nimpongeze Mheshimiwa Rais, wakati anaingia katika Awamu yake ya Sita alikuta kuna lots mbili ambazo zimeanza kutengenezwa, lakini leo tunaongelea lots tano zimeongezeka lots nyingine tatu, tumeongezeka Makutupola – Tabora; Tabora – Isaka; na Isaka - Mwanza, na Tabora - Kigoma iko katika hatua mbalimbali za manunuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala la kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa hiyo na hii nimpongeze Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake kazi nzuri mnaifanya. Kwa hiyo niwaombe sana muunganiko wa hizi lots zote zikikamilika tukienda Tabora - Kigoma maana yake tuna uwezo wa kufanya biashara na DRC Congo na Burundi na hivyo uchumi wa nchi utaendelea kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kwamba tumeona maboresho ya reli ya zamani, Mheshimiwa Waziri lazima tukupongeze na hilo, kuna reli ambazo zililala muda mrefu lakini zilifufuliwa kuanzia Serikali ya awamu ya tano mpaka leo tunaona Dar - Moshi, Moshi - Kilimanjaro na sehemu zingine na hizo zimeweza kuongeza pia na mapato ndani ya taasisi yetu ya TRC. Kwa hiyo nimpongeze na ndugu yetu Bwana Kadogosa kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali katika maeneo ya mikataba na hasa Serikali katika kuingia katika mkataba wa Fixed Lump Sum Contract, huu ni mkataba wa jumla usiobadilika katika mabadiliko ya corona, katika bei za mafuta, kama tusingekuwa na mikataba ya namna hii maana yake tungetengeneza hasara kubwa zaidi ya matrilioni ya pesa, lakini Serikali yenye maono na wataalam na wazalendo wameweza kuliona hili kwa mbali na kuweza kuzuia hasara ambayo ingeweza kutokea.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele yako ya pili ilikuwa imelia.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuunga mkono hoja naomba sana Mheshimiwa Waziri hasa kwa Wilaya ya Misenyi paangalie, ahsante sana na nakushukuru. (Makofi)