Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyang'hwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha mimi kunipa afya njema na uhai kwa siku ya leo na kuweza kusimama kwenye Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia nizidi kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo anaendelea kuzifanya hususani pia kwenye miundombinu ya barabara na usafirishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumpongeza Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Profesa Mbarawa pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Kasekenya, Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na timu yote. Pia nichukue nafasi hii ya kuwapongeza wafuatao kabla ya mchango wangu; nimpongeze Meneja wa TANROADS Mkoa wa Geita, lakini pia Meneja wa TARURA Mkoa wa Geita na Meneja wangu wa Wilaya ya Nyang’hwale wa TARURA. Meneji wa TARURA Wilaya ya Nyang’hwale anafanya kazi vizuri sana kwa kushirikiana na Mameneja wa Mkoa wa Geita kwa sababu watu hawa wako karibu sana na Ofisi za Wabunge hususani Mbunge wa Mkoa wa Nyang’hwale kwa kweli wananipa ushirikiano mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuipongeza Serikali kwa kuweza kututengea bajeti kwa barabara ambayo niliuliza swali asubuhi na sasa hivi nizidi kuipongeza Serikali kwa kutenga pesa kwa ajili ya upembuzi yakinifu barabara yetu ya kutokea Nyamkumbu - Nyang’hwale – Bukwimba – Karumwa – Nyangorongo; naipongeza sana Serikali. Lakini pia Serikali imeweza kutenga bajeti kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa kilometa mbili katikati ya Mji wa Karumwa ili kuweza kupunguza vumbi na adha ya wananchi ambao wanaweza kupata madhara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua ni lini ahadi za viongozi ambao waliofanya ziara katika Jimbo la Nyang’hwale tangu mwaka 2010 wameweza kuahidi ahadi ya ujenzi wa barabara ya lami kutokea Kahama Jimbo la Msalala, Nyang’olongo – Bukwimba – Karumwa – Ijundu – Busolwa - Ngoma hadi Busisi. Viongozi hawa wakuu wa nchi wameanza kutoa ahadi hizi tangu mwaka 2010 viongozi hawa nitapenda niwataje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi hawa kwanza alianza ziara yake Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete - Rais wa Awamu ya Nne alikuja mwaka 2010 akatoa ahadi hiyo, lakini alikuja pia mwaka 2012 akatoa ahadi hiyo, lakini Mama yetu Samia Suluhu Hassan wakati anazunguka katika kuomba kura akiwa kama Makamu wa Rais na yeye aliahidi, lakini pia Rais wa Awamu ya Tano naye aliahidi ujenzi wa barabara wa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu wamekuja viongozi mbalimbali wa chama akiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi kipindi kile Abdulrahman Kinana naye aliahidi barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami.
Sasa napenda kujua ni lini utekelezaji huu wa ahadi za viongozi utaanza kwa sababu imekuwa ni hadithi leo miaka 12 nazungumzia jambo hili, viongozi hawa walituahidi sisi kama wananchi wa Nyang’hwale tunamakosa gani? Kwa sababu tumekuwa tukiahidiwa fedha zikipatikana, leo hii miaka 12 hata kwenye upembuzi yakinifu hatujaingizwa; je, ni lini tutaingizwa kwenye upembuzi yakinifu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2012 Mheshimiwa Rais Awamu ya Tano wakati ule alikuwa Waziri wa Ujenzi aliahidi pia, lakini siyo hivyo tu viongozi wengi wamepita na kuahidi, sasa leo mimi sitakubaliana mpaka hapo utakapokuwa umenipa majibu yaliyo sahihi, nitashika shilingi yako leo, sijawahi kushika shilingi, lakini Mheshimiwa Mbarawa leo nataka nishike shilingi ili utoe majibu yaliyo sahihi ili wananchi wangu waweze kuelewa umeahidi kitu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukizingatia barabara hii ambayo mimi naipigia kelele miaka 12 imeunganisha mikoa mitatu, imeunganisha Shinyanga, imeunganisha Geita na imeunganisha Mwanza, lakini pia imeunganisha Wilaya tatu. Hii barabara ina umuhimu sana kwa kuchangia ama kuchochea maendeleo katika Wilaya ya Nyang’hwale. Leo hii wananchi wanaotoka ama wanaotumia barabara ya kutoka Kahama kwenda Mwanza kwa kupita njia ya Shinyanga wanatumia kilometa 280 lakini ukitoka Kahama, ukapita Jimbo la Msalala, ukapita Kalumwa Wilaya Shinyanga ukaenda Mwanza ni kilometa 160 tu kilometa zaidi ya mia moja na kitu wanakuwa wame-save. Kwa hiyo, ninaomba barabara hii muiangalie kwa umuhimu wake ili iweze kutengewa fedha kwa ajili ya kujengewa lami ili kuokoa gharama ambazo zinaweza kuepukika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ambalo inaitwa Mamang’ombe; barabara ile inaitwa Mamang’ombe ilikuwa ni barabara kuu ambayo ilikuwa ikiunganisha Kagera, Geita na Shinyanga. Barabara hii sasa hivi tuliambiwa itafunguliwa kuanzia Mbogwe itapita Bukoli, itapita Bujura, itapita Nyamigogo, itapita Nyashilanga, itapita Bumanda, itapita Kalumwa, itapita Nyungwa na kuunganisha Wilaya ya Vijijini Shinyanga, Salawi. Barabara hii tulishaambiwa na tayari kwamba ipo ndani ya mpango. Ninaomba kukuuliza Mheshimiwa Waziri mpango huo ulishafutwa au umewekwa kando kwanza? Nitapenda nijue ni lini sasa mpango huo wa kufungua barabara hiyo inaitwa Mamang’ombe ili iweze kufunguka wananchi niliowataja wa maeneo haya na vijiji vile waweze kupata maendeleo kwa sababu barabara ile imefungika. Mimi nikiwa mdogo kipindi kile kuna mabasi na malori yalikuwa yakipita kutoka Salawi kwenda Uganda kwa kupitia njia hiyo barabara hiyo imefungika tunaomba barabara hiyo iweze kufunguliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu ni hayo machache sitaunga mkono hoja mpaka hapo Mheshimiwa Waziri atakaponiambia barabara yangu ya kutoka Kahama - Nyangolongo - Kalumwa kwenda Busisi itaingizwa lini kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante sana. (Makofi)