Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii ya Ujenzi. Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuweza kusimama kwenye Bunge lako tukufu ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi lakini pia ninampongeza sana Naibu Waziri kaka yangu Kasekenya kwa namna ambavyo amekuwa akijibu maswali hapa Bungeni, pia ninampongeza sana Mheshimiwa Mwakibete namna anavyojibu maswali hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru Serikali hii ya Mheshimiwa Rais ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo imeenda kuuona uwanja wa ndege wa Mbeya. Tunaishukuru sana Serikali hii kwa sababu wameweza kuweka taa ambapo sasa ndege zinaweza kutua usiku kwenye Mkoa wetu wa Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana nieleweke vizuri, ninaombi moja uwanja ule wa Mkoa wa Mbeya uwanja wa ndege unaitwa Songwe International Airport nilikuwa ninaomba sana ule uwanja ubadilishwe...

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. SUMA I. FYANDOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ule uwanja jina libadilike na uitwe Mbeya International Airport kwa sababu mara nyingi...

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma kuna taarifa, taarifa Mheshimiwa Neema.

T A A R I F A

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nimpe taarifa dada yangu Mheshimiwa Suma Fyandomo Ikenda kwamba suala la uwanja wa Songwe siyo uwanja wa Mkoa wa Mbeya, na ni uwanja wa kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Kwa hiyo, wanapotafakari na kusemea uwanja ule wakumbuke kwamba siyo wa kwao Mbeya, ni wa kwetu wote, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma Fyandomo unapokea hiyo taarifa?

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa siipokei, ule uwanja ni uwanja wa Mkoa wa Mbeya uko ndani ya Mkoa wa Mbeya na hauko Mkoa wa Songwe, sasa hivi Songwe ni Mkoa.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vile ambavyo mimi...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma subiri kidogo.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: ...naweza nikajidanganya kwamba mabasi ya Shabiby ni yangu mimi, badala ya kuanza kutafuta mabasi ya kwangu ambayo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma kuna Taarifa kidogo.

T A A R I F A

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi naomba tu kumpa taarifa mzungumzaji kwamba ule uwanja siyo wa Mkoa wa Songwe, siyo wa Mkoa wa Mbeya ni uwanja wa kanda, kwa hiyo kuuita ule uwanja kwamba jina liwe Mkoa wa Mbeya ni ubinafsi. Nakushukuru. (Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosikitika hapa hawa ndugu zangu wa Mkoa wa Songwe wanajichelewesha kwa sababu wanajidanganya, ule uwanja ninaomba uitwe Mbeya International.

MHE. CONDESTER M. SICHWALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taratibu, kama ni suala la uwanja naomba tumuachie Waziri atakapokuja atajibu kwa sababu limeshakuwa kubwa.

Mheshimiwa Suma endelea. (Makofi)

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, taarifa zao nazidi kutokuzipokea na hata ukiangalia hapa wanaelezea kwamba uwanja ule ni wa Kanda, lakini wanaokanusha hili ni Wabunge wa Mkoa wa Songwe. Hivyo, ninasisitiza ninaomba Serikali ule uwanja uandikwe Mbeya International Airport. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi tumekuwa na wageni…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu tafadhali maana nina mengi ya kuchangia, ahsante. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa tu taarifa maana yake ulizuia lakini nikaona anaendelea kuchakata kwamba uwe wa Mkoa wa Mbeya. Sasa kuondoa hii mikanganyiko na mgawanyiko na kuleta utofauti kwenye hii mikoa nilikuwa napendekeza huu uwanja ufikiriwe hata kupewa jina la kiongozi ili usiwe na majina ya mkoa ili kuleta umoja. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma taarifa hiyo unaipokea?

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa inaweza ikanikuna kidogo ya Mheshimiwa Esther Matiko. Uwanja ule ninaomba kama mtafikiria kwamba muupatie jina la kiongozi maalum ninaomba basi uitwe Tulia International Airport. (Makofi/Kicheko)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi wewe mbona unaongea sana?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma subiri kidogo.

T A A R I F A

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipingani na hoja ya dada yangu Mheshimiwa Suma, lakini concept iliyopo kwenye uwanja wa Songwe ni umetolewa kama ambavyo Mkoa wa Kilimanjaro unaitwa kwa jina la Mlima Kilimanjaro, Mkoa wa Rukwa unaitwa kwa sababu ya Ziwa la Rukwa, Mkoa Ruvuma unaitwa kwa sababu ya Mto wa Ruvuma. Kwa hiyo, hata ule uwanja uliitwa kwa sababu kuna mto ambao unaitwa Songwe kama sehemu ya kutangaza kivutio. Kwa hiyo, hatumaanishi sisi Wabunge ambao tunatoka Mkoa wa Songwe tunataka uendelee uitwe kwa mkoa wetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Umeeleweka, nimesema kwenye suala la jina la uwanja wa ndege hakuna tena taarifa. Tuendelee Mheshimiwa Suma.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ninaomba niseme hivi ninaongea haya kwa msisitizo, mimi binafsi nina wageni wangu walikuwa wanatoka Ulaya kuja kunitembelea, walibaki wanahangaika angani maana walikuwa hawaoni jina la Mbeya International Airport wanaona Songwe hawajui … (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba…

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ahmed Shabiby.

T A A R I F A

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa huko wanang’ang’ani uwanja uitwe Songwe na Songwe nao watakapopata uwanja wao utaitwa nani? (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma unaipokea taarifa hiyo?

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa ya Mheshimiwa Shabiby kwa kukupiga magoti, ahsante sana. Nadhani nimeeleweka namna ambavyo wageni wetu wanakuwa wanasumbuka wanavyotaka kutua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitashukuru sana endapo Serikali italichukua hili kwa maana ya kuandika ule uwanja jina stahili Mbeya International Airport kama mnaona kwamba inafaa kuandikwa jina kwa sababu Mheshimiwa Tulia Ackson ni mwenyeji wa Mkoa wa Mbeya basi uitwe Tulia International Airport. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana pale Mbeya sisi tuna tatizo kidogo. Tuna tatizo la usafiri…

MBUNGE FULANI: Toa hoja kuhusu jina la uwanja.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa hoja, naomba uwanja uitwe Tulia International Airport, nimetoa hoja. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Waheshimiwa naomba mkae. Mheshimiwa Suma endelea. (Kicheko)

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Mbeya namna ya kusafiri kufika Dodoma tunazunguka sana, nilikuwa naomba nishauri Serikali watupatie ndege ambayo itatoka Mbeya kuja moja kwa moja Dodoma, maana sasa hivi tunazunguka ukitaka kupanda ndege upande ndege utue Dar es Salaam halafu Dar es Salaam ufike Dodoma. Nilikuwa naomba sana mlichukue hili ili mtuone na sisi wananchi wa Mkoa wa Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa suala la airport nilikuwa naomba jambo moja ambalo hili jambo halihusu ndege za local kwa maana ndege za ndani ya nchi yetu sisi. Nilikuwa ninaomba sana uwanja wa ndege kwa maana ya ndege zinazotoka nje ya nchi ambazo zinashushia abiria terminal three nilikuwa naomba sana kule tuweke tozo la trolley kwa maana kwamba sisi tunaposafiri kwenda nchi za nje hasa Marekani ukitua pale kwa maana kwamba yaani ndiyo upo immigration huwezi kuruhusiwa kuchukua trolley bila kulipia na trolley lile ukilivuta halitoki mpaka uweke fedha. Kwa hiyo, sisi hii itatusaidia kama chanzo cha mapato ya ndani ya nchi yetu. Narudia kwamba naomba nieleweke ndege zetu za ndani hizi zisiingizwe kwenye hizo tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachangia barabara ya Wilaya ya Rungwe ambayo hii ni ya ahadi ya tangu kipindi cha Awamu ya Nne. Ile barabara ni barabara ya Masoko Road kwa maana inaanzia pale Tukuyu Mjini kwenda Luhangwa kupita Mwakareli kupitia Suma kuja kutokea Katumba; ile barabara niyamuda mrefu sana, ile barabara alipatikana mkandarasi, lakini mkandarasi yule anasuasua sana, anakwenda taratibu sana, sijajua tatizo lipo wapi! Sijajua tatizo ni fedha ama tatizo limekaa upande gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Wilaya ya Rungwe wanahamu sana kuhakikisha ile barabara imekamilika ili waweze kujikwamua na kukwama kwama kwa magari, maana mvua ikinyesha ni tatizo kubwa sana. Nitashukuru sana endapo Serikali italichukua hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa dhati niliongea kwa uchungu sana kuhusu barabara ya kutoka Igawa mpaka Tunduma. Sasa basi ninaingia kwenye ombi maalum, nilielezwa hapa na Naibu Waziri kwamba tatizo ni mkandarasi hajapatikana, kwa maana hiyo fedha zipo. Nilisisitiza kumuomba mkandarasi apatikane mara moja. Ninaomba mnapokuja kuwasilisha hapa naomba sana nipate majibu kwamba mmeshampata mkandarasi wa kuijenga ile barabara ya kutoka Igawa mpaka Tunduma na kazi itaanza lini ya kujenga ile barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana namna ambavyo Serikali inaendelea kufanyakazi yake, lakini watu wa TANROADS hawa wanafanyakazi nzuri, lakini wanakuwa wanajisahau wakati fulani. Madaraja haya zile kingo za pembezeni mwa barabara kukiwa na daraja zinakuwa zimebomoka, zinakuwa hazipo, wanajisahau sana kurudishia kiasi ambacho kule kwetu kwenye barabara ya uwanja wa ndege ukitokea Ntokela unakuja uwanja wa ndege ule uwanja wa ndege umeitwa uwanja wa ndege kwa sababu gari zinashindwa kukata kona zinapaa, zinapitiliza, zinadodondoka, lakini mbele yake kuna daraja lile daraja kingo ya upande mmoja imevunjika siku nyingi na juzi kati gari ilitumbukia ….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma, nakuongeza dakika moja kwa sababu ya taarifa zile. Nakuongezea dakika moja, malizia.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ile kingo haipo tena, gari ilitumbukia matokeo yake ikalipuka ikawaka moto na watu waliteketea pale. Ninaomba sana hawa watu wa TANROADS wanapoona kwamba kwenye barabara ambako kuna madaraja kama kingo za daraja lile zimebomoka naomba wawe wepesi wakurudishia ili tuweze kuponya maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)