Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa dhati kabisa nianze kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Taifa letu kutuletea maendelea Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nipongeze Wizara kwa maana ya kwanza Waziri lakini na watendaji wote wa Wizara mpaka Wakala wa Barabara kwa maana ya TANROADS, ndugu yangu Mativila, CEO wa TANROADS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye hoja yangu ya msingi na nianze kueleza kupanga ni kuchagua, rasilimali fedha ni chache lakini tunazitumiaje hizo rasilimali fedha kwenye mambo ya muhimu, wachumi wanasema opportunity cost you foregone for the best alternative. Sasa kuhusu Wakala wa Barabara yaani TANROADS ilianzishwa kwa kusudi kubwa moja, kuunganisha mikoa yote nchini kwa kiwango cha lami. Hiyo ndiyo ilikuwa jambo la msingi kwa Wakala wa Barabara yaani TANROADS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumze kwa habari ya Mkoa wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro, ipo mikoa ambayo haijaunganishwa kwa kiwango cha lami kwa mkoa mmoja, miwili, lakini kwa Morogoro ni mkoa pekee nchini ambao mpaka leo tunazungumza haujaunganishwa na mikoa mitatu. Ukizungumza upande wa Kusini unazungumzia wenzetu wa Lindi, leo hii Mkoa wa Morogoro haujaunganishwa na Lindi kwa kiwango cha lami; ukienda Ruvuma bado Mkoa wa Morogoro haujaunganishwa kwa kiwango cha lami, lakini ukienda Njombe kwa kupitia Ifakara – Mlimba – Madeke - Lupembe pale Kibena Junction kwa maana upande wa Njombe bado Mkoa wa Morogoro na Njombe haujaunganishwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimeshukuru hapa, ninashukuru tena kwa mara nyingine, Mheshimiwa Rais ametoa kibali kwa ajili ya kuanza ujenzi walau kwa kiwango cha lami kilometa 50 kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni, katika hili Mheshimiwa Rais wanasema ameupiga mwingi, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo kimsingi ningependa kulisisitiza hapa ambalo Waziri anisadie wakati anakuja kwenye majumuisho hizi kilometa 50 ambazo tayari tuna kibali za kuanza ujenzi, mwaka ule wa fedha uliyopita zilielezwa kwa habari za kilometa 50 kuanza ujenzi, lakini halikadhalika mwaka huu imejirudia ilikuwa shilingi bilioni saba mwaka huu kuna shilingi bilioni nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kwa Mheshimiwa Waziri Profesa kaka yangu nisaidie wakati unakuja kwenye majumuisho wananchi wa Mlimba wangependa kusikia ni lini mkandarasi atakabidhiwa site kwenye barabara hii. Maana ahadi ya mwaka wa fedha uliopita ilikuwa ni hivyo hivyo haikutekelezwa, mwaka huu pia tumeongezewa kutoka shilingi bilioni saba imekuja shilingi bilioni nane. Sasa hofu yao inaweza ikawa ahadi tu wakati wote. (Makofi)

Kwa hiyo, wanatamani kusikia unapokwenda kwenye majumuisho lini mkandarasi atakabidhiwa site kuanza ujenzi wa barabara hii walau kilometa 50 na zile kilometa 220 ambazo ADB imeonesha nia ya kutusaidia na nimeona imetengwa fedha shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi. Kwa hiyo, ninaendelea kusema naishukuru sana Serikali na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali eneo lingine na Mheshimiwa Waziri hili jambo tumechelewa sana. Nimesikia hapa pamoja na barabara zingine kuna barabara inayokwenda kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Ruvuma, mfumo sasa wa barabara huu itaenda kujengwa kwa njia ya ubia. Jambo hili tumechelewa sana, wenzetu nchi nyingine huko duniani walishafanya haya mambo. Mimi nadhani sasa umefika wakati tusimame kidete, tusimamie mambo, kwa sababu katika hali ya kawaida nchi yetu ni kubwa, hatuwezi kujenga barabara zetu kwa kiwango cha lami sisi wenyewe kama Serikali. Lakini kwa kutumia ubia ni mfumo mzuri sana ambao ukienda nchi zote duniani wanafanya haya. Sasa naomba jambo hili litekelezeke ili Mkoa wa Morogoro uungane na Mkoa wa Ruvuma kupitia ubia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende eneo la mwisho mchango wangu utaishia hapo; nafahamu lakini kwa sababu Serikali ipo hapa na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Uratibu wa Shughuli za Bunge yupo, hata kama Waziri wa Fedha hayupo hili ni muhimu nikalisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingi za miradi yetu ya barabara inachelewa sana pamoja na mambo mengine, upatikanaji wa rasilimali fedham lakini pia uwajibikaji wa watendaji wa Serikali na wakandarasi. Changamoto kubwa nyingine ni changamoto ya kisheria, changamoto ya kisera. Leo hii kuna suala la GN yaani Government Notice, sasa GN inatolewa makao makuu tu pale TRA, sasa nchi hii ina miradi mingapi ya maji, ya barabara yote inatoa Idara moja tu pale TRA. Sasa jambo hili linawezekana kwa nini Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa mujibu lakini mkashauriana na Waziri wa Ujenzi kuona namna bora zaidi ya GN ipatikane kwa wakati, inatuchelewesha sana GN, imekuwa kikwazo kikubwa sana GN. Na kuna wakati niliwahi uliza hapa hii GN niliuliza ni raia anapatikana nchi gani. Lakini ni kitu cha kuamua tu, cha kuamua tu tubadilishe sheria, lakini pia kwenye Sheria ya Kodi Waziri wa Fedha ana mamlaka ya kutengeneza kanuni sasa kama GN sawa wangeweza ku-decentralize kwa maana sasa GN wale Mameneja wa Mikoa wa TRA wakasimiwe majukumu haya ya kutoa GN katika level za mikoa ili fast track miradi. Ni jambo la kuamua tu. (Makofi)

Sasa leo mkandarasi GN, mwezi mmoja amesaini mkataba GN, miezi miwili GN, hapana tunamkwamisha Mheshimiwa Rais. Jambo hili ni la kuamua tu. Nadhani Serikali imesikia katika hili na kwa leo niseme tu kwa dhati sina mengi ya kusema nimehemewa na wananchi wa Mlimba wamefurahi sana.

Mwishoni Mheshimiwa Waziri tukimaliza Bunge wangependa kukusikia ni lini unakwenda pale kuzungumza na mkandarasi aanze kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naipongeza sana Wizara hii, Mungu awabariki sana, ahsanteni sana. (Makofi)