Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa SGR, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali, Wizara na viongozi wote na watendaji wa Wizara kwa ujenzi wa SGR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia ujenzi huu wa SGR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro kilometa 300 tumeambiwa tumefikia asilimia 99.54; tunaipongeza sana Serikali kwa ujenzi huu na hii ilikuwa mwezi Aprili. Pia tumeambiwa majaribisho ya umeme tayari yameshafanywa.

Sasa kiu cha wananchi wa Morogoro wanauliza Mheshimiwa Waziri usafiri wa reli hii hasa kwa wasafiri wa wananchi ni lini utaanza kuanzia Dar es Salaam kuja mpaka Morogoro ili uweze kurahisisha usafiri. Naomba Waziri wakati anamalizia aweze kutueleza wananchi wa Morogoro tuweze kujua kwa sababu hii inasaidia katika mambo mengi ya uchumi, ya biashara pamoja na usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiongelea hapo kuna kipande cha kutoka Kihonda mpaka kwenye kituo kikubwa hicho cha SGR. Katika hotuba ya Waziri amesema kitajengwa kwa upande wa lami, nashukuru sana. Ombi langu, naomba kuwa mara kwa mara huwa naongelea barabara ya mzunguko ili kurahisisha na kupunguza foleni hapo ya Msamvu pale Manispaa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba badala ya kurudia hapo kwenye kituo iendelee mbele mpaka kwenye ofisi ya TAFORI kwa lami kusudi iweze kupunguza foleni ya hapo Msamvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea tena kuna baadhi ya wananchi wa Kihonda pale Manispaa na wananchi wa Kilosa ambao bado wanadai fidia zao ambao walihamishwa na walichukuliwa ardhi yao kutokana na ujenzi wa reli ya mwendokasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha sana hasa mimi mwenyewe na wananchi wa Mkoa wa Morogoro kuona sasa hivi Mkoa wa Morogoro umefikiriwa kwenye uwanja wa ndege, hiyo ni furaha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Morogoro wanausubiri kwa hamu ujenzi wa kiwanja cha ndege kusudi kurahisisha usafiri wa kusafiria kwani tulikuwa hatuna uwanja wa ndege kwenye Mkoa wetu wa Morogoro ambao utarahisha usafiri pamoja na ajira na uchumi. Kwa hiyo, tunashukuru sana kwa kuliangalia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, jambo lingine ujenzi wa barabara wa kutoka Bigwa kuelekea mpaka Mvuha, tumetengewa fedha nashukuru sana kwa sababu hii barabara ni muhimu inaelekea kwenye Bwawa la Julius Nyerere ambalo ni muhimu sana kwa kufua umeme. Kwa hiyo, kuanzia pale Mvuha kuelekea mpaka Kisaki mpaka kwenye Junction naomba na yenyewe ifikiriwe, tuweze kuona itafanyaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi ni kubwa kwa Serikali kuona pia barabara ya Ubena mpaka Ngerengere Jeshini na yenyewe imetengewa fedha, itajengwa kwa kiwango cha lami. Hapo hapo naomba kuwa kuanzia hapo kipande cha Ngerengere kuelekea mpaka Mvuha nacho kiangaliwe ili kusudi kiweze kujengwa kwa lami kufuatana na umuhimu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Magore kwenda mpaka Turiani ilitengewa fedha lakini tumeambiwa kuwa hizo fedha za kulipa makandarasi na ni madeni. Kwa hiyo, barabara ya kuanzia kipande cha Turiani mpaka Mziha pale kipo palepale wanasema wanafanya maandalizi. Namuuliza Mheshimiwa Waziri, hiki kipande cha Turiani mpaka Mziha ni lini kitajengwa na ni lini fedha zitapatikana, kwani kinaunganisha Handeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Dumila – Ludewa – Kilosa nashukuru inaendelea vizuri, lakini na yenyewe ilitengewa fedha lakini na zenyewe ni za kulipa madeni ya wakandarasi. Kipande cha Kilosa mpaka Mikumi wanasema maandalizi yanafanyika; je, hayo maandalizi yatafanyika mpaka lini Mheshimiwa Waziri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa barabara ya Kidatu – Ifakara - Lupilo mpaka kuelekea Malinyi mpaka kuelekea Songea ambayo inaendelea na ujenzi. Ni kweli barabara kuanzia Kidatu mpaka Ifakara inaonekana hata ukipita inaonekana kuwa ujenzi unaendelea. Kwa hiyo, kwa kweli tunaipongeza Serikali na tunaishukuru Serikali kuona ujenzi unaanza kuendelea. Ni barabara muda mrefu, ni barabara ambayo tumeiongelea humu Bungeni mara kwa mara, kwa hiyo naomba hata Ifakara kuendelea mpaka Malinyi mpaka Songea iweze kuonekana kuwa inajengwa kwa sababu upande wa Ruvuma ni kama walishamaliza upande wa Morogoro ndiyo bado. Kwa hiyo, naomba na yenyewe iweze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Chalinze – Magindu - Lukonge pamoja na Serengeti B mpaka Mziha kwa kweli nimeshukuru na nimefurahi sana kwa sababu barabara ya Mziha huwa ni mbaya sana kiasi kufika kwenda mpaka Mziha huwa ni kazi sana, lakini sasa hivi wamesema wanaiangalia. Nakuomba Mheshimiwa Waziri usiiangalie tu, naomba itengenezwe kwa kiwango cha lami kusudi wananchi waweze kupita kwa sababu inaanzia Mkoa wa Pwani mpaka inakuja kwenye Mkoa wa Morogoro. Kwa hiyo, nilikuwa naomba iendelee kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye madaraja; madaraja ya Chakwale pamoja na Nguyani sijayaona vizuri Mheshimiwa Waziri, haya madaraja ni muhimu sana kwa sababu wanafunzi wanapata shida, watu wanakufa humo kwenye maji wakati wa mafuriko inabidi usubiri kwa muda mrefu mpaka mafuriko yapite. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri unayajua hayo madaraja, naomba hayo madaraja yaweze kujengwa kwa uimara yaache kujengwa mwaka kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nilikuwa naona barabara ya Ifakara – Kihansi - Madeke mpaka Njombe na yenyewe imetengewa fedha lakini imetengewa fedha kidogo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba kwa sababu na hii inaunganisha Morogoro pamoja Njombe ni mikoa miwili totauti muiangalie vizuri kwa sababu ya uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambayo haikutajwa kabisa ambayo sikuiona labda ni macho yangu ni barabara ya Newala kuja mpaka Ulanga, Mkoa wa Morogoro. Inaanzia Mkoa wa Mtwara inaunganisha Mkoa wa Morogoro. Mheshimiwa Waziri naomba hiyo barabara iangaliwe na baada ya hapo kwa kweli mimi napongeza na ninashukuru na mawazo niliyoyatoa naomba yachukuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)