Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba nichukue nafasi hii nikushukuru kunipatia nafasi kwa ajili ya uchangiaji; lakini nianze kwa kuwapongeza sana Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi, hususan Mheshimiwa Waziri, watendaji wake wote akiwemo Katibu Mkuu bila ya kuwasahau watendaji waliopo chini yake kwa maana ya wale Wakurugenzi wa Mashirika yetu ya Reli, TBA na mambo ya anga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimesimama hapa kutoa pongezi na shukrani; hivi juzi tu mliweza kuona Mheshimiwa Rais akiwa katika Mkoa wetu wa Tabora na mambo aliyoyafanya katika Mkoa wa Tabora ni mambo makubwa sana, ndiyo maana nimewiwa nakuona kwamba ni vizuri nikisimama na kutoa pongezi kwenye Wizara hii ambayo inafanya mambo mazuri na mambo ya kufurahisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa napenda nikumbushe Wizara kwenye barabara baadhi ambazo zinapita katika mikoa minne. Katika Jimbo la Kaliua, tuna barabara ambayo inatokea Mpanda; barabara hii inaingia Wilaya yetu ya Kaliua, inapita Jimbo la Ulyankulu, Ushetu inaingia Kahama, inapita Msalala mpaka Geita. Barabara hii kwetu sisi ni barabara ya kiuchumi. Barabara ya Mpanda – Kaliua - Kahama mpaka Geita ni barabara ya kiuchumi kwa sababu kwanza mazao mengi sana yanategemewa kiuchumi yanatokea Mpanda na Kaliua. Lakini gari nyingi sana kwa mfano Kaliua tu kwa siku tunalaza mabasi karibu 28 ambayo yanakwenda Kahama. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, lakini tunazo hifadhi zetu kule Katavi, tunahifadhi ya Ugala, lakini bado tuna hifadhi ya Kigosi zote hizi ni National Parks. Uwepo wa barabara hii kiuchumi kwetu sisi bado itatusaidia kuinua uchumi wetu na mpaka sasa ninavyokwambia kwa mfano, Wilaya ya Kaliua ni Wilaya ambayo inafanya vizuri sana kwenye mapato ya ndani. sisi mpaka Disemba tumekusanya kwa asilimia 91; sasa haya mazao yote ambayo tumekusanya tulitegemea kabisa tungekuwa na usafiri bora na imara ingetusaidia sisi kuendelea kuinua uchumi wa wananchi wa Kaliua, Mpanda, Kahama na Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, mwaka jana katika bajeti wakiangalia pale waliweka ujenzi wa daraja la Ugala shilingi bilioni 3.5 na mimi kama Mbunge nikasimama nikasema bajeti imepitishwa na Bunge kuna shilingi bilioni 3.5 ya kujenga daraja la Ugala. Lakini mwaka huu wakasema, sasa tulifanya upembuzi wa awali, sasa tunakwenda kwenye upembuzi wa kina, sasa huku mliweka bajeti ya kujenga daraja leo mnatuambia mmekwenda kwenye upembuzi wa kina inamaana hili daraja mlikuwa mmeliweka kwenye bajeti na mkaweka ile fedha bila kuangalia hayo yote? Lakini hiyo fedha imekwenda wapi hiyo shilingi bilioni 3.5?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba tushauriane kiuchumi na tushauriane ili kujenga nchi yetu hii, tunaposhauri barabara ambayo ina cut across mikoa minne ni barabara ya kiuchumi, ni barabara ya msingi sana. lakini kule sisi tumepakana na nchi mbalimbali kama Burundi Rwanda, Congo tumepakana nazo kule, sasa huoni kama hii ni corridor nzuri sana na ukuangalia ndiyo maana Mheshimiwa Rais amefanya jambo la maana, unasikia kuna lot inakwenda kujengwa reli ile ya kutokea Tabora kwenda Kigoma lakini njia panda ni Kaliua. Kuna reli nyingine inatoka Kaliua inakwenda Mpanda kwa maana joint ya Kalema kule ili tuweze kusafirisha mizigo kwenda Congo. Kwa hiyo, mimi nilikuwa naomba ushauri wa kiuchumi, ushauri wa kitaalam huu ndiyo ushauri ambao tunatakiwa kuuzingatia kwa faida ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi ninalo jambo pia ningependa kushauri. Jambo hili linahusiana sana na barabara ambayo inajengwa, nawashukuru sana kwenye barabara ambayo inajengwa ya kwenda Kigoma. Barabara hiyo kile kipande cha Kazilambwa alikuja Naibu Waziri pale na nadhani ni kilometa 36 ambayo ni karibu shilingi bilioni 38 tunawashukuru sana. Lakini kwenye ile barabara tulikuwa tunaushauri, kuna kijiji kinaitwa Ugansa ambako inajengwa hapo kuingia katika mji mkubwa sana wa Usinge, ile Usinge peke yake ni kata ina watu karibu 80,000 na nina Imani kwa sensa ambayo tunakwenda kuitekeleza sasa hivi sisi kule tunajua kuzaa, idadi ni kubwa sana ya watu kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale tumeweka kilometa tisa ambazo zinaingia mpaka katika Kituo cha Afya, lakini sasa nilikuwa nawashauri, hebu fanyeni ushirikiano kati yenu na watoto ambao ni TARURA, barabara ile ni ya TARURA msipowashirikisha TARURA mkija kuondoka ulinzi na uhifadhi wa ile barabara utakuwa kwa nani. Kwa hiyo, ninaloliomba jambo kubwa sana hapa ni ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nawaomba TANROADS, TARURA hajasimama kama alivyo TANROADS. Nilikuwa nawaomba pale Kaliua kuna majengo mlipomaliza barabara ya kilometa 28 kutoka Urambo – Kaliua, yale majengo yote yaliyobaki Kaliua Mkurugenzi wangu Bwana Jerry Mwaga aliwaandikia barua akawaomba yale majengo yasiendelee kuchakaa Halmashauri tuyatumie, lakini mpaka sasa barua hiyo haijajibiwa. Amekuja Mkuu wangu wa Wilaya mpya Bwana Chacha Matiko, akakumbushia kwa barua. Sasa tulikuwa tunaomba majengo yale yamekaa kwetu, sisi tuna shida mbalimbali, tunahitaji vyuo, vituo vya afya, tunahitaji mambo mbalimbali, lakini majengo yamekaa pale jengo lisipokaliwa nadhani mnaelewa linashuka thamani. Sasa pale majengo yanaharibika kwa nini msitupatie, shinda ni nini mpaka msitupatie. Lakini hapo hapo kuna vifaa ambavyo vimeachwa na nyie TANROADS, mkandarasi amemaliza kazi yake, anapomaliza awa TARURA hawana uwezo wa vifaa kwa maana ya kupima barabara zetu, maabara hawana. Vile vifaa mngekuwa mnawakabidhi watu wa TARURA ili na wenyewe zile barabara zao waweze kufanya, kinyume cha kukaa wanamkodi mkandarasi, wanamkodi Mchina kwa ajili ya kuja kurekebisha barabara zetu; ule ubora wa barabara za TARURA unashuka kwa sababu ninyi hamjawaachia vifaa hivi ambavyo vinabaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo ningependa kushauri, na hili napenda nilishauri vizuri sana kwenye barabara zetu hizi; naomba nawaomba tuangalie kusisitiza uzito wa magari, maana yake kuna barabara zinaanza siku mbili unaiona kabisa hii sijui inazidiwa, sijui ni chini ya kiwango mimi sijaelewa hapo. Kwa hiyo, nilipenda mlifanyie utafiti muangalie tutasimamaje sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ushauri mwingine unakwenda kwenye Shirika la Reli sasa. Nafahamu Mheshimiwa Rais ana dhamira njema sana ya zile reli zile lots mbili ambazo zitakuja Ukanda wetu, lakini kwenye reli sasa hivi reli sisi inatumika Tabora – Kigoma treni inakwenda, lakini Tabora – Mpanda treni inakwenda.
Sasa treni inayokwenda Mpanda mmetuma mabehewa mawili tu, watu wanajaa kuliko kiwango mle. Lakini jambo lingine na Mtendaji Mkuu nikuombe kaka yangu Kadogosa pale engineer, yaani pale kuna wizi umeibuka sijui ni mfumuko wa bei hata sielewi shida ni nini? Yaani hizo hizo behewa mbili mnao polisi ambao wanatembea na zile behewa, lakini wananchi wangu wa Kaliua wanaibiwa kuliko kiwango.
Kwa hiyo, nilikuwa naomba wale polisi ambao wanafanya kazi pale wahakikishe wanalinda mali za wale wananchi ambao wanasafiri kwa kutumia treni. Lakini kwenye reli hiyo hiyo kwenye vituo, angalieni vile vituo ambavyo vina idadi kubwa ya watu ili mtupe muda mwingi wa kutosha kwa ajili ya kusimam,a kinyume cha kuwa inafika dakika moja tu paaa imeshaondoka mnaleta ajali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ikisimama kwa muda tayari mnatuinulia uchumi wetu sisi kwa sababu zipo bidhaa wajasiriamali wanafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba walichukue hili la kuimarisha reli yetu na kuimarisha usalama wa abiria ambao wanasafiri. Kwanza idadi ya mabehewa iongezwe kwa maana ya Tabora – Kigoma lakini Tabora – Mpanda ambayo ni mawili tulikuwa tunashauri hata mkitupa manne shida iko wapi, kinyume cha behewa moja linakweta unakuta hadi watu 300, siyo sawa. Kwa hiyo, mimi ushauri wangu mkubwa nilikuwa naomba niishauri Serikali kwenye jambo hilo mtupe kipaumbele sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilikuwa na ombi, juzi mlivyokuja mmeona Meneja wetu wa Mkoa wa Tabora anafanyakazi vizuri sana. Kijana anayejituma kabisa anakwenda na kazi yenu, lakini ninachokiona pale sisi kikao cha mwisho cha Road Board, yule bwana anajitambulisha bado ana kaimu tu, sasa nikawa napiga mahesabu yule marehemu ambaye ametufanyia kazi nzuri Mzee Ndabalinze amekuja kijana mwenye kasi tena hajathibitishwa kazini, hebu naomba mumthibitishe ninyi wenyewe mmefungua barabara nzuri mnaona. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)