Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata dakika 10 na kwa kuwa ni mchango wangu wa kwanza ndani ya Bunge hili naomba niwasemee wananchi wa Kigamboni. Wananchi wa Kigamboni ili waweze kufika Mjini ni lazima wavuke maji. It is whether wapitie kwenye feri au wapitie kwenye daraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna changamoto kubwa sana sasa hivi kwa wananchi wa Kigamboni kutokuwa na uhakika especially pale panapokuwa na mahitaji yao kwenda Mjini. Vivuko vyote ambavyo vinafanya kazi pale MV- Magogoni, MV - Kazi na MV - Kigamboni vyote ni vibovu. MV - Kazi ambacho ni kivuko kipya kuliko vyote hivi sasa hivi kimetolewa kimepelekwa doc kwa ajili ya matengenezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetoka Dar es Salaam hivi karibuni, juzi tu mimi mwenyewe nimejithibitishia nimekaa ndani ya maji zaidi ya nusu saa, kivuko kilikuwa kinazunguka, geti ya kufunguka haishuki, imebidi tutoe magari kwa kurudi reverse.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri alitembelea kivuko hiki cha MV - Kazi na aliahidi wananchi wa Kigamboni kwamba ndani ya muda wa miezi minne kivuko kile kitakamilika, hivi ninavyoongea matengenezo ya MV - Kazi hayajaanza, Serikali haijatoa fedha, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya hitimisho lake atuambie MV - Kazi inaanza kufanya kazi lini, fedha hizo zinatolewa lini, na ni lini wananchi wa Kigamboni wategemee kivuko kile kitaanza kufanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo usimamizi wa vivuko kwakweli ni mbovu sana, TEMESA wameshindwa majukumu yao. Ninaliomba Bunge lako kwamba sasa hivi wananchi wa Kigamboni pale ukiwahi sana kuvuka, ukifika pale ili uvuke ni dakika 45 hadi Saa Moja, leo hii asubuhi Nahodha wa MV - Kigamboni amekunjwa na abiria ambao walikuwa na jazba, kwa sababu amefika pale ameiweka Pantoni muda mrefu, wananchi wamekasirika wamemfuata kule kule kwenye Deck wameanza kupigana. Vivuko hivi vitakuja kuleta maafa, Mimi ninaomba kama TEMESA wameshindwa kazi tuvibinafsishe, wapewe watu wenye uwezo, waweze kuendesha vivuko hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya pili ni suala la daraja. Ninampongeza Waziri kidogo katika hili amewafuta machozi wananchi wa Kigamboni, lakini hoja ya wananchi wa Kigamboni ni kufuta tozo ya daraja. Daraja lile ni kiunganishi cha barabara ni sawasawa na madaraja mengine, inawezekana njia ambayo inatumika pale ni ya PPP hilo tunalielewa, lakini kuweka tozo pale inaongeza gharama sana kwa wananchi wa Kigamboni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa wa Kigamboni wanachangia katika ujenzi wa madaraja mengine nchini na wanachangia kulipa madaraja mengine nchini, iweje wananchi wa Kigamboni katika daraja linalowahusu wao walipe na Tanzania wengine wasichangie katika hili? Kwa hiyo nikuombe na Waziri hapa ananisikia, tumeanza hili la mwanzo bado tunahitaji tozo ya daraja la Kigamboni ifutwe ili kuwe na uwiano na madaraja mengine. Wananchi wa Kigamboni wanasema hawahitaji daraja la Tanzanite liwekewe tozo, tukiweka tozo katika daraja la Tanzanite tunajenga presidency mbaya, tutajenga presidency kwamba Kigongo Busisi ambalo linakamilika nalo tuweke tozo, tujaweka presidency kwamba daraja la mto Wami nalo tuweke tozo na tutarudi katika madaraja yote Tanzania tuweke tozo, tunasema kwamba madaraja ni viunganishi na Serikali ibebe gharama ya madaraja yote nchini (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu namba tatu ni suala la miundombinu ya barabara, Naibu Spika nawe ni Mbunge wa Dar es Salaam tunayo changamoto kubwa sana ya miundombinu ya barabara katika Wilaya za Dar es Salaam. Wilaya yangu ya Kigamboni ni moja ya Wilaya ambayo imekuwa na changamoto kubwa sana ya miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua katika bajeti hii tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kibada - Mwasonga kwenda Tutisongani kwa kilometa 41 tunalipokea kama wananchi wa Kigamboni, lakini rai yangu kwa Wizara ya Ujenzi pamoja na TANROADS ni kuhakikisha kwamba hiyo barabara ambayo ni barabara ya kimkakati ambayo inakwenda kuchechemua uchumi wa Wilaya ya Kigamboni na Industrial Hub ambayo Mheshimiwa Rais alikuja kuizindua, basi hiyo barabara iweze kutengenezwa na tuweze kuijenga kwa ukamilifu wake wa kilometa zote 41. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ninawaomba tena Wizara ya Ujenzi kuna barabara pacha ya kutoka Feri - Mji Mwema kwenda Pemba - Mnazi nayo tumekuwa tunaijenga kwa kilometa moja moja ingependeza hii barabara nayo kwa sababu inakwenda kuunganisha eneo la Pemba Mnazi ambako tumeweka ekari zaidi ya 1,000 za uwekezaji ili sasa na hilo eneo tuanze kulitumia katika masuala ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo niongelee changamoto ambayo wanaipata watumiaji wa barabara au watumiaji wa daraja la Nyerere. Katika barabara ya kutoka Bendera Tatu kwenda Darajani kuna mizani ambayo mmeiweka pale ambayo magari yakitoka bandarini yanapita kuangalia uzito kabla hayajaendelea. Ile mizani haitumiki kwa ajili ya kutoza faini au vitu vingine lakini inaleta msongamano usiokuwa wa lazima. Ninaishauri Wizara ya Ujenzi ule mzani muuondoe pale kwa sababu unaondoa maana nzima ya daraja ambalo lipo pale na kuongeza msongamano usiokuwa wa lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo mnafanya ujenzi wa mwendokasi, mnafanya ujenzi wa flyover pale karibu na Uwanja wa Taifa lakini Wakandarasi wale hawajaweka miundombinu mizuri ya michepuo hali ambayo inapelekea kuwa na foleni kubwa sana. Watumiaji wa Mbagala, wote wa Mkuranga sasa hivi wanapita Kigamboni, ninawaomba sana Wizara ya Ujenzi hakikisheni tunakuwa na barabara nzuri za michepuo na kuondoa ule mzani pale karibu na bandarini ili njia za kwenda na kutoka darajani ziweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ninaomba LATRA ipo chini ya Wizara ya Ujenzi, mwananchi wa Kigamboni ili afike mjini anahitaji nauli tatu hadi nne. Akipitia kwenye kivuko anatoka kule alikotoka anavuka nauli ya pili anatoka pale anakwenda posta nauli ya tatu anakwenda sehemu ambayo anataka kwenda hiyo nauli ya nne, akipitia darajani anahitaji nauli tatu, ninawaomba LATRA kwa kuwa tozo za daraja zimepungua kwa kipindi hiki, tunatarajia kuona kwamba tutakuwa na route ndefu kama maeneo mengine ya Mkoa wa Dar es Salam, ambapo wananchi wanaweza kusafiri kwa kutumia nauli moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba Waziri wa Ujenzi atakapokuja kufanya hitimisho aje na majibu ya hoja ambazo nimezieleza la sivyo nitasimama na kukamata Shilingi, kwa kipindi hiki naomba aje na hayo majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)