Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii, nianze kwanza kwa kumpongeza Rais kwa kazi anazoendelea kulifanyia Taifa hili. Nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wake kwa kazi wanazoendelea kuifanyia Wizara yao, kazi za muhimu sana kwa Taifa hili. Lakini pia nimpongeze…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ungekuja kiti cha mbele uonekane vizuri ili wananchi wako wakuone. Hebu njoo ukae mbele hapa, fanya haraka lakini. (Makofi)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaomba unilindie dakika zangu. Basi naendelea kuwapongeza watendaji wa Wizara, nilimtaja Katibu Mkuu, Injinia na Balozi Aisha, Erick Hamis - Bandari, TRC - Kadogosa, Mr. Matindi – ATCL na wengine wote kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo machache nitajaribu kwenda kwa haraka. La kwanza kabisa ni barabara ya Tengeru – Moshi – Himo na baadae mpaka Holili ambayo ni kilomita 105. Barabara hii kutoka Moshi kwenda Arusha ilikuwa ni muda wa dakika 45 mpaka saa moja. Lakini kutokana na msongamano mkubwa wa magari sasa hivi ni masaa mawili mpaka mawili na nusu. Huu ni upotevu mkubwa wa hela na upotevu mkubwa wa muda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na ahadi ya kuipanua barabara hii imekuwepo kwa muda mrefu sana. Sasa nimeangalia kwenye Hotuba kwenye ukurasa wa 17 nimeona imetengwa Bilioni 8.4 lakini ni kilomita 105. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri wakati unapokuja kuhitimisha, watu wa upande ule wafahamu ni barabara yote inatengenezwa au ni vipande vipande. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye Mji wa Moshi peke yake naona mmeelekeza kwamba itatengenezwa kilomita 8.4. Lakini pale kwenye daraja la Kikavu mita 560. Pia nikaona kuna mkopo kutoka Japani kipande cha kutoka Tengeru mpaka USA. Sasa tunatengeneza vipande vipande au mtatusaidia tupate fedha itengenezwe yote ili hilo tatizo liweze kuisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hiyo ya Arusha pamoja na wingi wa watu pia tunahitaji bypass baadhi ya maeneo. Moshi ni Jiji linalotegemewa kukua muda wowote, sasa hatuna bypass pale. Tumekuwa tukiipigia kelele sana barabara ya Getifonga ambayo sasa iko chini ya TARURA inayokwenda mpaka Maboginikahe na baadae mpaka Chekereni. Nawaomba ni vizuri sana TARURA na TANROADS wakae pamoja. Kama Majiji yanatengenezewa bypass ile ni moja ya sehemu muhimu sana ya kutengeneza bypass waone ni nani ataifanyia kazi hiyo barabara. Lakini hata hivyo kwa sasa barabara hiyo ni muhimu sana kwa maendeleo ya watu wa Moshi Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la airport. Tulipewa airport mwaka jana, Moshi Airport kurekebishwa na nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba hiyo ilikuwa ni ahadi ya Rais pia alipokuwa kwenye Royal Tour aliondokea pale akaona ile hali ya uwanja. Lakini mpaka leo pamoja na kwamba tulipewa bajeti iliyopita kazi haijaanza, tunaomba kujua shida ni nini maana ikipita tena kwenye bajeti hii haipo, kwenye bajeti iliyopita mpaka sasa tunaenda mwezi wa sita haijaanza matokeo yake tuataambiwa hela zilirudi na kazi imeshindikana kufanyika. Naomba wakati wa kuhitimisha atufahamishe ni nini kinaendelea kwenye Moshi Airport. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye utengenezaji wa barabara kwenye Taasisi za Serikali, mwaka jana palikuwa pamewekwa Moshi Police School (Chuo cha Polisi Moshi) barabara zake za ndani mpaka sasa hazijatengenezwa, nimejaribu kuwasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye wakati ule alikuwa Naibu Waziri wa Fedha, hazijaweza kutengenezwa na kwenye ile randama eneo hilo sasa imewekwa Taasisi nyingine, sina haja ya kuitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha utufahamishe kama ile ya mwaka jana haijafanyika hii mpya inafanya nini pale ili ikiwezekana itolewe turudishe Chuo cha Polisi Moshi ili barabara zake za ndani zitengenezwe. Na nimejitahidi sana, nilikuwa Diwani wa Kata ile ya Kilimanjaro miaka 10 lakini kwa kutumia fedha za Halmashauri na za TARURA barabara za Taasisi hazitengenezwi. Sasa Chuo cha Polisi barabara zake ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la kuiwezesha Wizara. Ninaangalia haswa kwenye suala la bandari na position ya Tanzania kwa nchi hizi za Afrika Mashariki lakini na majirani wengine wengi wameongelea. Mimi nadhani tuna kazi ya kufanya na hatutakiwi kuogopa. Kuna nchi zingine wameweza kuwatumia DP World. DP World ni kampuni ya Dubai ya bandari ambayo imejiweka kibiashara na inaendesha bandari kwenye nchi nyingine. Hata Uingereza wanaendeshewa bandari zao baadhi, India, Australia, Argentina. Kama hatuna hela za ku-invest ili bandari zetu zifanye kazi vizuri tuweze kufanya majadiliano na watu kama hao wenye uwezo lakini pia wana connection ambazo zinaweza kutusaidia kuboresha bandari lakini tukaunganisha na reli ili tuweze kupata fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo mengine ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la wakandarasi wazawa, niseme tu tumeelezwa kwamba wakandarasi wa nje wanapokuwa na miradi na zile deadline wanakuwa wanapewa interest wakicheleweshewa malipo, wakandarasi wa ndani haiko hivyo. Sasa mfumo huu unasababisha Serikali inakuwa kama inaenda kuwaua wakandarasi wazawa, hawalipwi kwa wakati, wakicheleweshewa hawapewi interest lakini pia upataji wao wa kazi haswa hizi kubwa hata kwa kushirikiana unakuwa wa kusuasua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kama tunataka kujenga Taifa imara lazima tuwawezeshe wakandarasi wa ndani, waweze kutumia hizi hela ndani na wakizitumia ndani multiplication yake inaendelea kuwa kubwa kwa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie hapo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)