Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie katika Bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Awali ya yote niunge mkono hoja ya bajeti hii kwamba tuipitishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile leo naweza nikawa siyo katika kiwango kikubwa sana kwa sababu leo mimi ni zamu yangu ya kuhudumu katika Kanisa letu la hapa Bungeni. Kwa hiyo, Roho wa Bwana ameniatamia tangu asubuhi. Sasa naomba niwakaribishe baadaye saa saba kwenye Ibada hapo Basement, kwa sababu watu watakuwa wengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiitazama Sura ya Viongozi wa Wizara hii unaweza kuona namna ambavyo Mheshimiwa Rais aliteua watu watulivu. Ukimtazama Waziri, tazama wasaidizi wake, Katibu Mkuu, unaweza kuona nini Rais anataka kwenye Wizara hii. Anataka umakini, anataka utulivu, nami nitakuwa Mbunge wa ajabu sana kuwaondolea utulivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunawapongeza sana na tunawaunga mkono, lakini tunataka wazidishe zaidi kusimamia taasisi ambazo ziko chini yao. Ukitazama taasisi ambazo ziko chini yao nazo ni kubwa. Unaweza kuona bandari, Mkurugenzi wa Bandari tunampongeza sana Ndugu yangu Erick Hamisi, pia Masanja Kadogosa tunampongeza kwa kazi nzuri. Hata ule wizi wa kijinga jinga ulikuwa pale wa kuibaiba sijui redio za magari bandarini siku hizi ni hadithi. Kwa hiyo, unaweza ukaona namna ambavyo jamaa wako serious.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Mkurugenzi wa ATCL tunampongeza sana Eng.Matinde, lakini yeye kwa kweli amelemewa sana na madeni. Mimi nilikuwa nashauri Serikali ingeyachukua haya madeni, tungeweza kuona ufanisi wa ATCL.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa nje hapo wakati naingia nimepewa message na mama mmoja mtu mzima sana, aitwa Sauda Fundi, unajua mimi ni Mbunge wa Taifa, siyo wa Jimbo peke yake; huyu mama amestaafu kazi mwaka 2015, amefanya kazi miaka 32, mpaka sasa hivi hajalipwa mafao yake. Kwa hiyo, mwangalie wastaafu wa ATCL, wanapata taabu sana, ni watu wazima, ukimwona huyo Bi. Mkubwa yuko hapo nje, hebu angalieni maslahi yao ili nao waweze kuishi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza habari ya barabara, Wabunge wanajitahidi sana kuzungumza pengine thamani ya barabara inayoelekea sehemu fulani, lakini ukweli ukimsikiliza Hayati Mwalimu Nyerere, namnukuu, anasema: “Kwa kuwa sisi ni viongozi wa watu, basi isiwepo shida yoyote ya watu tunayoweza kusema shida hiyo haituhusu.” Yaani tunapotaja barabara, ni barabara kwenda kwa watu, kwenda kwa wananchi, hakuna barabara ambayo siyo muhimu. Barabara zote zinazoenda kwa wananchi ni za muhimu. Kinachotofautiana hapa ni ufundi tu wa namna ya kusema Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuiombe Serikali iongeze kasi ya kutafuta fedha ya kujenga barabara za lami kwenda kwa Watanzania kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inavyosema. Kwa mfano, chukulia barabara ya Dodoma Mjini – Ntyuka - Mvumi Makulu - Mvumi Mission inakuja kutokea Handali, inakuja kutokea Kikombo Makao Makuu ya Jeshi, inaunganisha na Ikulu. Hii barabara imezungumzwa sana na mwaka huu tumeiweka kwenye Ilani ya Uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wizara hii lazima iwe na vipaumbele. Mwanzo nimesema kuna barabara za service na za investment. Kwa sasa hivi zianze barabara za investment, hasa ukanda wa mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeitaja Bandari ya Kabwe. Bandari ya Kabwe ndio inakuja kubeba uchumi wa Bonde la Rukwa kwa Mheshimiwa Geofrey Pinda, Mkoa wa Rukwa, kupeleka soko Congo. Bandari zote zimejengwa kwa lengo la kufanya fursa ya uwekezaji kwa nchi jirani Rwanda, Burundi, Zambia na Congo. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri na Wizara nzima ije na mpango mkakati wa barabara zitakazojengwa na TANROADS. Kupitia Wizara barabara zijengwe kwa ajili ya kuelekea ukanda wa Ziwa Tanganyika ambako ndio kuna uchumi, kwa hiyo, maziwa yote mawili tutakuwa tunalisha Congo kutokana na juhudi za Mheshimiwa Rais za kufungua fursa kupitia diplomasia ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)