Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia dakika tano ili niweze kuwasemea wananchi wa Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Spika, kimsingi nieleze, nimekuwa mara nyingi nikiongelea changamoto ya miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Kagera hususan Wilaya za Kyerwa na Karagwe. Nimeuliza maswali mengi nikiongelea barabara na nikihusianisha Wilaya ya Karagwe na Kyerwa na kupakana na nchi ya Rwanda na Burundi. Maelezo yangu yalijikita kuonesha ni potential kiasi gani nchi inaweza kupata kama ikiunganisha Kyerwa na Karagwe na nchi hizi nyingine kwa kupitia lami.
Mheshimiwa Spika, hizi ni wilaya ambazo zinafanya vizuri katika mazao mbalimbali ya kilimo, lakini zinashindwa kufanya biashara na nchi nyingine na Mikoa mingine ya Tanzania Bara au Mikao mingine kwa sababu haina barabara.
Mheshimiwa Spika, nimeeleza mara nyingi sana barabara ya Mgakorongo - Kigarama na Murongo ambayo ina urefu wa kilometa 105. Mheshimiwa Waziri amejibu mara kadhaa, lakini nimesoma hotuba yake ya mwaka 2021, amesema barabara ipo kwenye mchakato, hakusema ipo kwenye upembuzi. Akaenda mbali zaidi, anasema, barabara wanaenda kulipa fidia. Nimesoma leo anasema, sasa ndiyo tunaenda kutangaza zabuni, lakini bado michakato haijafanyika, wananchi wamefanyiwa tathmini hawajalipwa fidia. Sasa je, tunaendaje hatua ya pili kabla bado hatujalipa hizi fidia na watu wameshindwa kuendeleza maeneo yao kwa sababu hawajalipwa fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nimekuwa nikiongelea barabara ya Bugene - Nkwenda hadi kwenda Murongo huko huko ambayo ni barabara mbili; ukichukua Wilaya ya Kyerwa inaunganishwa na barabara mbili, ambapo moja unapita Mgakorongo na nyingine unapita Nkwenda. Ina maana hii Wilaya tukiweza kui-link kwa barabara tutaweza ku-tap uchumi ulio kwenye hizi Wilaya.
Mheshimiwa Spika, kitu kingine, nimeeleza umuhimu wa barabara ya kutoka Benako kuja mpaka Karagwe Bugene. Hii barabara ni muhimu kwa sababu ya ulinzi. Pale ni pori, mara nyingi watu wamekuwa wanapita pale wanatekwa, wanauwawa. Hii barabara kama itaunganishwa, itakuwa ni kichocheo kikubwa cha biashara ya kutoka Karagwe, Kyerwa na Rwanda, na kuna magari mengi yanakwenda Rusumo yanahitaji kutumia hiyo barabara.
Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, ni wakati sasa wa Kyerwa na Karagwe kusikika, mmetuacha muda mrefu, hebu fungueni uchumi wa maeneo haya kwa kufungua hizi barabara. Ahadi za muda mrefu, ahadi tamu tamu, maelezo mengi; na kesho nina swali la msingi. Waheshimiwa Wabunge naomba mnisikilize kesho, watakuja watatudanganya vile vile. Sasa ifikie wakati na sisi tupewe hizo barabara ili Wilaya ziweze kuchangia kwenye uchumi wa nchi hii.
Mheshimiwa Spika, nakushukru sana. (Makofi)