Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii nami nichangie katika Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ambayo kwa kiasi fulani tumekuwa tukiilalamikia, lakini hata jirani yangu hapa jana alifanya vurugu sana kidogo anipige mateke, lakini nilikwepa na bahati nzuri nilikuwa na bakora, ningemchapa kweli kweli. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Mheshimiwa Prof. Mbarawa Mnyaa kwa weledi wake mkubwa katika utendaji kazi na Manaibu Mawaziri wake wote wawili ambao kwa kweli wanatuhakikishia kwamba wamedhamiria kuifungua nchi hii kwa barabara za lami.
Mheshimiwa Spika, Bunge lililokwisha tulilalamika sana hapa, zilikuwa zinawekwa barabara kilometa 20 na 25, lakini Mawaziri hawa walipokuja hasa Prof. Mbarawa ameanza kuonesha dhamira ya kuongeza angalau badala ya 20 zikawa 50, badala ya 25 zikawa 60, basi hii ni dhamira nzuri ambayo tunaamini kwamba muda mfupi tutaenda kuunganisha Mikoa yetu kwa barabara za lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mikoa ambayo inataka kuunganishwa kwa lami sasa na ambayo bado na haitajwi ni Mkoa wa Singida na Mkoa wa Mbeya kupitia barabara ya Itigi - Rungwa hadi Makorongosi ambako kule ndiko kuna Mkandarasi. Hata hivyo namshukuru sana Mheshimiwa Mbarawa, leo tunaenda kuanza ujenzi upande wa Mkoa wa Singida. Ni jambo la faraja sana kwa wananchi ambao wametutuma humu ndani.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuridhia nasi tujenge barabara katika eneo letu, lakini Mheshimiwa Mbarawa kumpelekea hoja hii mezani kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lipo jambo ambalo halijajadiliwa sana katika Bunge lako hili Tukufu upande wa Uchukuzi. Wengi tumejikita katika barabara na kwa kweli ni changamoto kubwa. Pia upande wa uchukuzi nako kuna changamoto kubwa sana. Ajali za barabarani zimekuwa zikitesa watu wetu na zimekuwa zikiua watu wengi sana. Kipindi cha nyuma sana kulikuwa na magari ya kizamani sana; sisi tuliozaliwa zamani kidogo tulipanda yale magari ya Leyland, kulikuwa na barabara za vumbi lakini ajali zilikuwa chache.
Mheshimiwa Spika, miaka ya katikati hapa barabara za lami zilipoanza kuja, ndiyo ikatokea ajali moja kubwa sana hapa Dodoma, basi la Yarabi Salama liliua watu wengi sana, ikapelekea Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati huo Mheshimiwa John Samweli Malecela akazuia magari kutembea usiku.
Mheshimiwa Spika, yalipozuiwa kutembea usiku, baadaye sasa kila Mkoa mabasi yanatoa asubuhi kwa kushindana saa 12. Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa alipokutana na wadau mwaka 2019 katika Ukumbi wa Hazina, alishauri mamlaka ambayo inasimamia vyombo hivi vya usafiri, kwamba kweli kuna sababu hadi leo magari yaendelee kutokutembea usiku? Kama haipo sababu, na kama ipo, basi ni maeneo gani? Bahati nzuri waliyaainisha na baadhi ya magari yakaruhusiwa.
Mheshimiwa Spika, ilikuwa gari ikitoka Bukoba inafika Dumila au Gairo inazuiwa, halafu wale watu wanapanda kwenye Noah. Yaani mtu ametoka kwenye basi kubwa, kwa sababu ana haraka na kwa sababu Coaster hazizuiwi usiku, wakawa wanapanda Coaster na Noah kwenda Dar es Salaam. Ajali zikawa nyingi zaidi. Waliporuhusu magari haya kutembea hadi kufika mwisho wa safari kwa maeneo ambayo nisalama, ajali zimepungua.
Mheshimiwa Spika, changamoto iko wapi? Changamoto ilipo sasa ni vile ving’amuzi ambavyo wameweka kwenye mabasi, havizuii ajali, ni vitu ambavyo vinaonesha gari linatembea namna gani? Ni mtu ambaye anaweza kuweka mwenyewe na aka-track gari yake na kuiona inakwenda mwendo gani, lakini imekuwa ni sharti la leseni; na ili upate leseni lazima uwe na kile king’amuzi.
Mheshimiwa Spika, leo ni zaidi ya miaka mitano vile vidude hata mamlaka ya kudhibiti ubora wa vitu vyetu haivitambui, lakini taasisi kubwa ya Serikali ndiyo imeweka kuwa sharti la leseni. Naiomba sana Serikali izingatie na kuona, kama kitu hata Mamlaka ya Udhibiti Ubora (TBS) haikitambui, inakuwaje ni sharti la leseni ya usafirishaji? Maana yake havizuii speed, vinaangalia tu unaendaje?
Mheshimiwa Spika, hoja inakuja eti zikiwekwa speed governor, gari zitashindwa ku-overtake. Gari zinatofautiana nguvu. Dpeed governor ni mwisho wa speed. Kuna gari lina uwezo wa kupanda mlima na nyingine haina uwezo. Kwa hiyo, tukiweka speed governor maana yake tutazuia ajali.
Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ije na mfumo huo kwenye mabasi. Tracking system ni system ambayo mtu anaweza kuiweka hata mwenyewe. Watu wanaosafirisha mizigo nje ya nchi wanaweka kwenye malori yao ili aone gari lake linakwenda upande gani? Labda limetoka nje ya barabara, ili aweze kujua, lakini leo eti tracking system imekuwa ni sharti la kupata leseni ya usafirishaji. Hiki kitu hakitendi haki na siyo sawa, kwa sababu ni kitu ambacho hata Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Bidhaa zinazoingizwa nchini (TBS) haikitambui.
Mheshimiwa Spika, sasa leo nilikuwa nashauri jambo hili tulifanyie kazi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, mwisho, mabasi yanatoka saa 12.00 Magufuli Stand yanafukuzana…
SPIKA: Kengele imeshagonga.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, naomba sekunde 30 tu nijazie hii hoja.
Mheshimiwa Spika, mabasi yanafukuzana kwenda Mbeya saa 12.00, ya kwenda Mwanza yanatoka saa 12.00, ya kwenda Musoma yanatoka saa 12.00, za kwenda Arusha yanatoka saa 12.00; hatuwezi kubadilisha mfumo huu. Mabasi yanaweza kutoka saa 11.00, saa 1.00, saa 2.00, ule muda wa mafukuzano ndiyo unasababisha ajali.
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Massare.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Naam Mheshimiwa.
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)