Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana tarehe 18 ya mwezi huu Rais wetu alifanya kitendo ambacho kwa sisi wana Katavi ilikuwa ni mkombozi, kwa maana ya Katavi, Tabora lakini na mikoa mingine ya uzinduzi wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kubwa ninalolikumbuka nikiacha kusema ahsante nitakuwa ni kiumbe wa ajabu, nashukuru sana kwa kitendo kile lakini bahati nzuri Waziri alikuwepo na Waziri anakumbuka sisi wana Katavi tulinufaika ile chenji itakayobaki kwenye ujenzi wa barabara ya Mpanda, Tabora imeombwa ielekezwe kwenye barabara ya kwenda Kigoma. Kwa hiyo, nilikuwa napenda nishukuru kwa suala hilo muhimu. Mkuu wa Nchi aliongea na yule kiongozi wa Benki ya Afrika kwamba chenji itakayotoka pale itusaidie wana Katavi kwa barabara ya kwenda Kigoma. Nashukuru sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutokana na hayo ya kwangu yatakuwa machache sehemu kubwa nikijikita kwenye kusema ahsante, lakini ahsante ni namna ya kistaarabu ya kuomba tena, ahsante kwa barabara ya Mpanda Tabora. Lakini tunayo barabara muhimu sana kwa maana ya Mpanda, Ugala, Kaliua, Ulyankulu kwenda Kahama. Barabara hii najua wataalamu wapo wanafanyia kazi suala hili lakini barabara ile na hii niliombe liwe katika sura ya nchi kwa ujumla wake kwa sababu zifuatazo;

Mheshimiwa Spika, inapotokezea mnabarabara moja tu ikipata dharura yoyote namna ya kutoka hapo inakuwa ngumu. Kwa hiyo, unapokuwa na barabara nyingine ambayo inaweza ikasaidia wakati wa dharura hilo jambo lisiwe tu kwa ajili ya Mkoa wa Katavi lipate sura ya kitaifa mnakuwa na barabara moja ikikatika matatizo uchumi unayumba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo kwa maana ya kufungamanisha fursa mbalimbali na suala zima la uchumi tumeongelea Ziwa Tanganyika. Tunayo meli moja ya Liemba labda kwa manufaa ya Bunge hili ile meli ilizinduliwa Februari 5, 1915 meli hiyo lakini ilianza kutengenezwa 1913 meli ya Liemba na ndiyo meli ambayo wanatuambia meli pekee duniani ambayo ilitumika katika vita vya kwanza vya dunia na inaendelea kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, sasa tafsiri yake nini tunaweza tukafungamanisha hata wenzetu wa utalii kama meli hii kwa siku zote hizo na watu huko duniani wanaifahamu hivyo inaweza ikawa ni chanzo cha utalii pia lakini watanzania angalia tunavyokalia fursa. Mbali ya kufanya kazi katika Ziwa Tanganyika lakini ingeweza kuwasaidia na wenzetu wa utalii kufungamanisha fursa hizo. Kwa hiyo, nilikuwa naomba ukiachilia kwamba inaenda kuwasaidia wakazi wa ukanda ule lakini bado inaweza kusaidia kunyanyua mapato ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru juzi Mkoa wangu wa Katavi Shirika la Ndege wametuongezea safari nyingine ya nne tulikuwa na safari tatu katika wiki kwa maana Jumanne, Alhamisi na Jumamosi tumeongezwa na trip nyingine ya Jumatatu, kwa hiyo, tumekuwa na trip nne. Tafsiri yake ni nini? eneo lile linaendelea kufunguka. Kwa hiyo, niwashukuru katika hilo lakini na watu wengine muendelee kufahamu Katavi inafikika fursa hizo zipo, tumieni ndege, tumieni reli tumieni barabara.

Mheshimiwa Spika, upande wa fidia; kuna wananchi ambao wameendelea kusubiri maeneo ya Magamba, Misungumilo na Kawajense, hawa watu kwa muda mrefu wanasubiri fidia. Naomba sana tuwaangalie watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, reli; Mheshimiwa Waziri analo deni kwa maana ya kujenga kibanda cha kusubiria abiria katika stesheni yetu ya Mpanda. Namwomba sana sambamba na kuongezewa mabehewa, reli kwa ujumla wake, naomba wabadilike wasifanye kazi kizamani, wale watu wa Mpanda hawapandi bure, wanapanda kwa kulipa. Unapotafuta mabehewa yaliyochoka yaani sehemu nyingine zote mabehewa yaliyochoka ndiyo yanapelekwa kule Mpanda, wanatufanya tuonekane wa kizamani. Naomba tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)