Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwa muda tuliopewa kwa hoja iliyo mezani ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Spika, naomba niende moja kwa moja katika hotuba ya Waziri, ukurasa wa 225, mahali ambapo amesema Bodi ya Usajili wa Wahandisi katika nchi yetu. Chombo hiki najiuliza kinafanya kazi namna gani, lakini ukisoma katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba bodi hii hufanya ukaguzi wa shughuli za kihandisi katika nchi yetu. Ninachojiuliza je, chombo hiki kinasimamia ubora wa kazi zinazofanywa ambazo tunasimama hapa kupitisha fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara na madaraja? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu pamoja na kwamba tunaweka fedha nyingi na kwa sababu watu wanalia nchi nzima kwamba barabara hazijatengenezwa hapa na pale, lakini usimamizi wake katika ubora wake ukoje? Naomba kutoa mfano, iko barabara katika Mkoa wetu kutoka Biharamulo mpaka Kyamyorwa katikati na barabara hii ilijengwa wakati Hayati Marehemu Rais Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi. Barabara hii baada ya mwaka mmoja imeanza kutengenezwa, kufanyiwa repair mpaka leo hivi ninavyoongea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza kama kuna bodi inayosimamia Wahandisi hawa, je, nani anawa-allocate katika kufanya kazi? Huko nyuma tulipata nafasi ya kwenda Uturuki, tukaona namna gani chombo kama hiki kinavyosimamia kazi ambazo zinafanywa katika nchi yao. Ni kwamba Mhandisi yeyote anapokuwa assigned kazi yake lazima chombo hiki kijue kwamba mwandisi amekwenda kusimamia kazi hii na anapoboronga anawajibika katika chombo hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sasa nataka kujua chombo chetu hiki kinasimamiaje watu hawa? Kwa sababu ukitazama barabara hizi kuharibika ina maana hata kama ni wakandarasi, je, kazi ya Wahandisi wetu sisi ni nini? Ni kwenda kupita na kuangalia au na kutumia utaalam wao katika kuhakikisha kwamba kazi tunazotenda zinalinda nchi yetu, zinakuwa imara na tunatumia pesa kwa wakati na tuendelee kufanya mambo mengine. Hatuwezi kuwa tunajenga na kubomoa kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kule kwetu Bukoba Vijijini, kuna eneo moja linaitwa Kyabaramba. Eneo hili ni eneo ambalo ni tope na limekuwepo miaka nenda rudi, ni tingatinga. Wamekwenda kutengeneza sijui kama ni TANROAD au sijui kama ni TARURA, lakini wametengeneza ukifika pale hata mtoto mdogo atajua. Juzi hapa ninapokwambia siku tatu zilizopita mvua imenyesha, maji yamefurika katika barabara ambayo wametengeneza na wahandisi wamekagua, wamelipa, lakini magari yamesimama kwa sababu maji yamefurika kwa sababu wamejenga ndivyo sivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu dakika ni chache niende kwenye vivuko. Tunacho kivuko kinaitwa Kyagabasa. Kivuko hiki ukifika kimeandikwa MV yaani marine vehicle, lakini ukifika pale utashangaa kinaendeshwa na injini ambayo ina watts power 70. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nimefika mimi mwenyewe na nimevuka pale. Watts power ambazo zinaruhusu yaani ile mitumbwi ambayo inakwenda kuvua...
SPIKA: Sekunde 30, kengele imeshagonga.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, naomba waangalie kama kuna uwezekano wa kutengeneza daraja katika eneo hili kwa sababu ni fupi mno, ni pamoja na eneo moja linaitwa Kansinda na lenyewe wanaweza kufikiria kwa sababu linavusha watu katika Mto Ngono lakini wanaweza kutusaidia kutengeneza barabara. (Makofi)
SPIKA: Haya, ahsante sana.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)