Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kunipa nafasi nichangie bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais wetu Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayofanywa katika sekta hii ya barabara nchi nzima. Pia nataka niwapongeze waziri Naibu Waziri na watendaji wote wa wizara hii, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sikumpongeza Meneja wangu wa TANROADS wa Mkoa wa Kilimanjaro, Eng. Mota Kyando Mama ambaye anafuatilia sana barabara za Mkoa wa Kilimanjaro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende katika mchango wangu ambao nitachangia barabara mbili katika Mkoa wa Kilimanjaro. Barabara ya kwanza ni barabara ya Tarakea Holili ambayo ina Km 53. barabara hii imetengewa Shilingi Bilioni 5.8 ninaishukuru Serikali, lakini barabara hii ina urefu wa KM 53 kwa maana ya kwamba hela iliyotengwa haitoshi, ninaiomba Serikali iongeze fedha ili barabara hii iweze kukamilika kwa kiwango cha lami. Kwa kuwa barabara hii ni barabara ambayo iko katika mpaka wa Kenya na Tanzania, ni barabara ambayo ina unganisha border mbili barabara hii inaunganisha border ya Tarakea kwenda katika border ya Holili, hii ni barabara ambayo inaongeza uchumi wa nchi na wananchi wa Rombo kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Rombo wanategemea kilimo na biashara hasa akina mama, wanategemea barabara kwa ajili ya kuvusha biashara zao, kule Rombo bila barabara watu wanashindwa kupeleka mazao yao katika masoko, ninaiomba Serikali iongeze bajeti hii hili barabara hii iweze kukamilika kwa kiwango cha lami, pia ikumbukwe kwamba barabara hii ni muhimu kwa ajili ya ulinzi na usalama katika mpaka wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuongelea barabara hii niongelee barabara nyingine ya Elerai - Kamwanga ambayo ina Km. 44. Ninaishukuru pia Serikali kwamba imetutengea Bilioni Mbili katika barabara hii, lakini nirudie kwamba Bilioni Mbili hazitoshi katika barabara ile, barabara ile inatumika sana kwa kupitisha watalii, wanaotoka KIA wakipitia Bomang’ombe kuja Sanyajuu, Kamwanga na kuingia katika Wilaya ya Rombo, kwa hiyo barabara hii inaunganisha Wilaya ya Rombo na Wilaya ya Siha.

Mheshimiwa Spika, wakina Mama wa Siha hawatofautiani na akina mama wa Rombo ni akina mama ambao wanajitafutia riziki kwa kupitia biashara ya viazi, hivi viazi vya chips tunavyokula huku vinatoka vingine Siha na kule Rombo ninaomba Serikali itengeneze barabara hii, kwanza kuinua uchumi wa maeneo haya Wilaya hizi, lakini pia ikumbukwe kwamba watalii watakuwa wanazunguka ule mlima kutoka Wilaya ya Siha kuingia Rombo na kuingia katika mpaka wa Holili au Tarakea.

Mheshimiwa Spika, mimi sina mengi niishukuru Serikali lakini naendelea kulilia Serikali iongeze hela hizi ili hizi barabara ziweze kukamilika kwa kiwango cha lami. Baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)