Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye hotuba yetu ya Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametujalia na kufika hapa katika Bunge lako hili Tukufu na zaidi ya yote ninamshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa namna ya kipekee, kupitia mtumishi wake Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye aliniteua nimsaidie kwenye Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi sekta ya uchukuzi kama Naibu Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru wewe pia na nikupongeze sana kwa kuwa Spika, wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kwa asilimia 100. Zaidi pia nimshukuru Makamu wa Rais, Waziri Mkuu pamoja na Waziri wangu Profesa Mbarawa kwa namna ya kipekee umekuwa ukitusimamia kama Kaka, kama rafiki. Mimi na mwezangu pacha tuko tayari kufanya kazi utakayotutuma wakati wowote.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru pia na kuwapongeza Makatibu Wakuu wote wawili pamoja na Wakuu wa Taasisi zote ambao wamekuwa msaada katika kufanyakazi kwetu na zaidi ya yote niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao mmeshiriki kwa namna moja ama nyingine kuchangia bajeti yetu ya Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi, Mungu awabariki sana.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja zilizo mbele yetu ni nyingi, lakini kabla sijaendelea, napenda niwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Busokero ambao walinipa heshima ya kuwa mwakilishi wao na zaidi pia nimshukuru mke wangu, familia na leo niko na Waheshimiwa Madiwani, Baraza la Madiwani liko ndani ya ukumbi huu kushuhudia bajeti hii likiongozwa na Mwenyekiti wa Chama pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bajeti hii imechangiwa na wengi, lakini mimi nitajikita zaidi katika Sekta ya Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) pamoja na Kampuni ya Ndege nchini (ATCL), Mamlaka ya Viwanja nchini (TAA) na nyinginezo; TCAA, TMA, pamoja na TAZARA na LATRA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikianza na Mamlaka ya Bandari nchini (TPA). Bandari yetu ya Dar es Salaam ndiyo lango kuu la uchumi wa nchi yetu ya Tanzania. Zaidi ya asilimia 40 ya mapato yote yanayokusanywa na TRA yanatoka kwenye lango hili la Bandari ya Dar es Salaam. Kwa maana hiyo, niwapongeze pia viongozi wote nikianza na Mkurugenzi Mtendaji kwa Mamlaka ya Bandari nchini ambapo wameweza kukusanya fedha zaidi ya Shilingi bilioni 895 na tunatarajia watafikisha Shilingi trilioni moja kwa mwaka huu. Ni historia ambayo haijapata kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bandari yetu ya Dar es Salaam ilikuwa na bandari zipatazo 66, lakini chini ya uongozi wa Mheshimiwa Prof. Mbarawa, mwezi huu tumerasimisha bandari 20 na kufanya bandari 86 zikiwemo pamoja za pale Dar es Salaam. Zaidi ya yote pia tuna bandari bubu zisizopungua 693 na hii ni kazi ambayo tunaliomba Bunge lako litupitishie bajeti hii ili tuweze kuzirasimisha zikiwemo na zile bandari alizosema Mheshimiwa kutoka Mkoa wa Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bandari yetu ni lango kuu la uchumi wa nchi yetu, lakini kwa kuwa wateja wetu wakubwa wanaopitisha mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam wanatoka nchi za Kongo, Zambia, Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi, hatuna budi kuunganisha mawasiliano kati ya bandari yetu na reli zetu nchini.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa habari ya reli ya TAZARA na reli ya kati. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha ya kwamba chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye hadi sasa tumeshasaini mikataba zaidi ya trilioni 14 kwa ajili ya SGR tafsiri yake tunakwenda kukusanya ama kupeleka mizigo ndani ya nchi ya Kongo kama mkakati wetu wa biashara.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, tumekusudia kwenda kufungua ofisi za TPA katika hizi nchi jirani ikiwemo Uganda, Kongo, Malawi na Zambia ili wateja ambao wanapata usumbufu kwenda nchi jirani ama kwenda bandari nyingine tuwakamatishie huko huko kwa kushirikiana na balozi zetu za nchi hizo. Huo ndiyo mpango wetu wa mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia shehena ambayo imepita ama imetoka katika bandari zetu, Zambia tuna asilimia 40 pekee. Maana yake asilimia 60 inakwenda Beira na Durban Afrika Kusini. Ukienda DRC tuna asilimia 39 kwa shehena 2,357,886; pia ukienda Burundi tuna asilimia 99.9 ambayo ni shehena ya 507,000; ukienda Rwanda ni shehena ya 1,369,000 sawasawa na asilimia 91, maana yake 9% wanakwenda kwenye bandari nyingine; ukienda Uganda ni 2%. Hapa tuna kazi ya kufanya. Zaidi ya asilimia 98 wanakwenda bandari nyingine. Maana yake tunahitaji kukaza buti ili asilimia 98 hizi zije kwenye bandari yetu.
Mheshimiwa Spika, ukienda Malawi asilimia 53 sawa na shehena kiasi cha 471,085. Kwa hiyo, nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika mamlaka ya bandari nchini kwamba lazima nguvu kubwa tupeleke huko kwa maana ya kutangaza bandari yetu na pia kuwe na mfungamanisho kati ya bandari pamoja na miundombinu ya kusafirishia mizigo kwenda nchi hizo jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza suala electronic single window system. Ni kweli pale bandarini tuna mfumo huu, lakini mfumo huo haufanyi vyema. Hivi sasa tuko katika mazungumzo na bandari zinazofanya kazi vizuri duniani kama T-World watakaofanya shughuli hii kwa maana ya ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na Serikali kupitia TPA inafanya mazungumzo na wawekezaji hawa DP-World kwa lengo la kuona uwezekano wa kuingia makubaliano uwendeshaji wa baadhi ya vitengo vya bandarini ili tufanye kama wanavyofanya wenzetu huko duniani.
Mheshimiwa Spika, nikihama kutoka bandarini, nije ATCL. Waheshimiwa Wabunge wamezungumza sana kuhusiana na kampuni yetu ya ndege hapa nchini, ni kweli Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan hivi sasa anavyosema ameshakutoa fedha kwa ajili ya kununua ndege zingine tano ambazo zitaongeza idadi kutoka 11 mpaka 16 hii itaongeza usafiri ndani ya nchi yetu na nje ya nchi yetu kwa hiyo niungane na Waheshimiwa Wabunge kwamba ATCL ni mkombozi kwetu lakini pia inarahisisha usafiri na sisi waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba unapotaka kwenda Dar es Salaam, tunapotaka kwenda mkoa wowote hususan kama Mwanza Mbeya na maeneo mengine tunatumia ndege hii kurahisisha usafiri wetu sasa safari ambazo tutaanza kuzitumia hivi karibuni kwa sasa tunakwenda nchi za Burundi Uganda, Comoro, China, Zimbabwe, Mumbashi, Kongo, Lusaka, Ndola Zambia, India Pamoja na Kenya.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tutafungua ofisi zetu nyingine na siyo tu kufungua ofisi katika hizo nchi, lakini pia tutaanza kwenda kwa Waheshimiwa Wabunge katika maeneo mbalimbali hususani tutaanza kwenda pemba, tutaanza kwenda Mombasa, tutaanza kwenda Musoma, maeneo yote ambayo viwanja sasa hivi vinajengwa na vinajengwa kwa sababu karibia tu tutaanza kwenda safari zetu za Air Tanzania.
Mheshimiwa Spika, pia tutakwenda maeneo mengine kama London, tutakwenda Dubai, tutakwenda Johannesburg, tutakwenda Mayotte, tutakwenda Kinshansa, hizi nimeshazitaja Mombasa, Musoma Pamoja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, waheshimiwa Wabunge pia wamezungumzia suala la fidia ni kweli kulikuwa na wafanyakazi katika shirika letu na makampuni yetu na ATCL lakini hivi ninavyosema zaidi ya Shilingi bilioni 131 zimekwishalipa kwa ajili ya wafanyakazi pamoja na kampuni ambazo zilikuwa zinaidai hii ATCL. Kwa maana hiyo, tunaomba Waheshimiwa Wabunge mtupitishie bajeti yetu ili twende kulipa madeni yaliyobaki ya kiasi cha Shilingi bilioni 5 kwenye kampuni yetu hii ya ndege.
Mheshimiwa Spika, najua ni mengi lakini niunge mkono hoja. Ahsante sana.