Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia Wizara ya Mifugo na Uvuvi; Wizara ndugu na Wizara ile ya Kilimo ambazo ni sekta za kiuzalishaji. Nilishaeleza mwanzo umuhimu wa sekta hizi, sasa niende kwenye undani wa sekta hizi, the agricultural sector, kwa wale ambao hawakusoma kilimo, inahusu mazao (growing crops) inahusu ufugaji wa ndege na kuku (poetry), inahusu kufuga wanyama (animal husbandry), inahusu kufuga samaki (aquaculture), inahusu maua horticulture na floriculture. Sasa tunazungumza kile kipande kingine baada ya kumaliza kipindi kile cha kwanza kilichokwenda na zawadi ya mama Mkoa wa Kagera. Ngoja nichambue hii nione kama na hapa kuna zawadi ya mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwanza suala la ufugaji wa vizimba. Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamezungumza na mwaka jana, 2021 nilizungumza, kwamba Misri anafuga samaki tani 1,400,000, lakini maji aliyonayo Misri ni madogo, ni machache kuliko maji ya Tanzania. Nakubaliana kuna kampuni moja ya simu zamani ilikuwa na kaulimbiu inasema: “Now You Are Talking.” Naweza nikasema Government, now you are talking, au now you are coming. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa ya Waziri anasema atatengeneza vizimba 19,500 na kufanya environment impact assessment ili atengeneze makazi kwa ajili ya ufugaji. Kagera atatupa maeneo tisa, lakini muhimu ni kwamba atazalisha tani 100,000. Kabla ya hapo tulikuwa tunazalisha tani 12,000. Tunatoka tani 12,000 anakwenda tani 100,000. Misri, now we are coming Misri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kuvutia kwamba mapato ya samaki hizo tani 100,000 ni Shilingi bilioni 600. Mauzo ya kahawa ya Tanzania kutoka Septemba, 2020 mpaka Septemba, 2021 ni dola za Kimarekani 163,000 au shilingi bilioni 383. Ina maana kwa kuwekeza kwenye vizimba vya Ziwa Victoria samaki watazidi kahawa, lakini hatutaacha kahawa, tutafanya kahawa, tunafanya na hiyo. Ndiyo hiyo Kamati yetu ilikuwa inalalamikia, ndiyo hiyo Kamati yetu ilikuwa inashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ambayo nami natumika naiunga mkono kwa maneno mawili; imeiambia Serikali changamoto za ugawaji wa vitalu zitatuliwe mara moja, nawaunga mkono. Jambo la pili, tuhimize kufuga, siyo kuchunga. Ndugu yangu Mheshimiwa Vita Kawawa kinachomwogopesha ni kuchunga, siyo kufuga. Tuhimize kufuga, siyo kuchunga. Huwezi kujenga uchumi wa nchi hii bila kufuga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze jambo lingine kuhusu upungufu; na katika hili namwomba samahani Mheshimiwa Mama Joyce, naishauri Serikali, simzungumzi mumeo Mheshimiwa Mama Joyce unisamehe, nanyi Wajumbe wa Kamati ya Siasa nazungumza kuhusu Serikali. Taarifa yote hatuzungumzi tutauza nini nje? Niliwaambia juzi, kiburi cha Ukraine anauza nje Dola bilioni 64 kwa mwaka, hatujazungumza hapa tunauza nini nje? Tunahitaji kuuza nje kusudi tuje tuweze kujenga Taifa imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake alitaja jina langu, baada ya kulitaja, simu zikaanza kurindima hapa; Wabaki Wabaki, umekuwaje Mwijage? Umekuwaje? Kwa nini Mheshimiwa Waziri alinitaja?

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, katika randama ukurasa wa 42, mimi ni Mbunge wa Muleba. Niliiuliza Serikali, mgogoro wa eneo la Mwisa II utatuliwe ili wananchi na wafugaji waendeshe shughuli kwa tija kubwa na kwa amani. Ndicho nilichoiambia Serikali. Mgogoro wa Mwisa II utatuliwe ili wananchi na wafugaji waendeshe shughuli kwa tija na kwa amani. Katika kuendesha tija kwa amani, wazalishe maziwa na bidhaa nyingine za kilimo, ndiyo nilimwuliza Waziri. Halafu nikasema, katika kumwuliza Waziri na Serikali yake, wananchi wa eneo la Lutoro wapewe ekari sita, siyo ‘angalau’. Lile neno ‘angalau’ sikulisema. Wapewe ekari sita kutoka eneo la Mwisa II lenye hekta 67. Sikusema kutoka eneo la Mwisa II, rejea kwenye komuniki Mheshimiwa Waziri. Ni pale walipo; na pale walipo nitakuja nikupe vifungu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa akanijibu akasema suala la Mwisa II bado lipo chini ya uwezo wa Wizara, ambapo Wizara itashirikiana na mamlaka husika katika Mkoa wa Kagera kwa kumaliza suala hili. Nakubaliana naye. Kumbe kumaliza matatizo ya Mwisa, Waziri ana uwezo na mkoa una uwezo, mnasubiri nini sasa? Komuniki tuliandika, watu wanalala nje, mnasubiri nini? Watu wanalia, mnasubiri nini? Watu wanachunga kwenye makaburi ya watu, mnasubiri nini? Kumbe Mkoa wa Kagera unaweza, na Waziri anaweza, mnasubiri nini watu na wanalia? Nitaipata wapi zawadi ya mama hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende Lutoro. Aidha, mahitaji ya wananchi wa Lutoro yalibainishwa na Kamati Maalum ambayo iliwashirikisha wananchi kwenye funga na fungua semi “iliwashirikisha wananchi.” Iliwashirikisha wapi? Wananchi ulikutana nao wapi? Nani alikutana na wananchi? Utakutana na wananchi wa Lutoro bila Mwijage, utawapata wapi? Hujawahi kukutana na wananchi. Kwa pamoja ilibainisha, eti ilibainisha watu wapewe kaya ekari mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lutoro wanampongeza Mheshimiwa Bashe kwa kusema atatoa ekari tano kwa mtu, hii haijawahi kukaa mahali popote, wanakudanganya. Nimekuomba samahani Mheshimiwa Mama Joyce, umwombee mumeo, huyu ni rafiki yangu. Halafu watasema; nisikilize, jambo la maudhi anasema, watapewa ekari mbili na endapo kutakuwa na mahitaji zaidi, wananchi wanatakiwa kushauriwa kutafuta maeneo hayo nje ya ranchi. Wananchi wanatakiwa kutafuta, watu wa Ngorongoro mbona hamkuwashauri waondoke? Wananchi wangu ndio mnawashauri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Rutoro ni la kisheria suala la Rutoro ni la utu suala la Rutoro ni la kisiasa! Mwaka 2015 Gymkhana Club Bukoba aliyepanda jukwaa ni mimi hali ilikuwa mbaya kule nenda kwenye video muangalie Rutoro ndio iliamua watu hawawezi kuondoka hiyo ndio iliamua hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja nikwambie nazungumka kwa ajili ya watu ya Kyebitembe naizungumzia Karambi naizungumzia Kasharunga Mubunda na Ngenge naizungumzia Rutoro mimi ni Mbunge wa Muleba ndio mwakilishi wa wananchi asitokee mtu yeyote akasema ndio mwakilishi wa wananchi ni mimi na Kikoyo hakuna wa kuchonga na nikifa mimi nitazikwa kwetu hakuna mwingine. Na niwaeleze watu wanakwenda eti Mheshimiwa Mwijage hamsemei mama unakwenda kwenye eneo la watu unachoma nyumba 280 unawaambia kazi iendelee Samia hoyee! kuna mtu atakujibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba 280 zimechomwa Migomba imekatwa halafu mtu anasema Mheshimiwa Samia hoye, sio Mheshimiwa Samia ninaye mjua Mama Samia anatoa zawadi nakubaliana na wewe ninachokueleza tukubaliane…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwijage naomba umalizie sentensi yako.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema Wizara yako Wizara ya Ardhi Wizara ya TAMISEMI tukae chini, chini ya Waziri Mkuu tuweze tukatafuta mstakabali wa suala hili vijiji vilivyopo pale vimeandikwa kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nakaa chini kabla sijakaa naomba mezani kwako niwasilishi mgogoro wa Muleba na Naruko naomba niuwasilishe mezani. (Vicheko/Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. CHARLES J.P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wasaidizi wa Mheshimiwa njooni mchukue hapa.