Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hotuba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi lakini kabla yayote nikutakie heri sana katika siku yako ya leo ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa.

NAIBU SPIKA: Ahsante bwana. (Makofi)

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazofanya kwa ajili ya nchi yetu pia nimpongeze kaka yangu Mashimba na Mtani wangu Mheshimiwa Ulega kwa kazi ambazo wanafanya katika Wizara hii ya Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipokuwa nasoma bajeti hii ya leo na bajeti iliyopita nimejifunza suala moja. Kila siku Waziri wa Maji Mheshimiwa Aweso hapa amekuwa akisema wali wa kushiba unauona kwenye sahani lakini leo ninaona wali wa kushiba sijauona kwenye sahani kwasababu bajeti ya Maendeleo Sekta ya Uvuvi 2021/2022 tulipanga Bilioni 99 mpaka Aprili, 2022 fedha zilizopelekwa kwenye Wizara ni bilioni 3.9 sawa na asilimia Sita, hii haiwezekani!

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba sasa Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Waziri wa Fedha aangalie Wizara hii kwa macho mawili kwa sababu kuna baadhi ya Wilaya kama Busega, chanzo cha mapato ni uvuvi. Kama wananchi wetu hawatapelekewa fedha kwa ajili ya uvuvi maana yake hatujataka kuwasaidia. Kwa hiyo, tukitaka kuwasaidia Watanzania wavuvi lazima tupeleke fedha kwenye Wizara ya Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilivyokuwa najaribu kufikiri namna ya kuchangia kwa Kaka Mashimba nikasema nitamuonea bure, bali nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha aangalie namna ya kuwasaidia watu wa Wizara ya Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo jambo moja ambalo naomba nilichangie kwa msisitizo. Kuna hawa watu wanaitwa BMU yaani Beach Management Unit, wamekuwa ni shida kwenye taasisi zetu, wamekuwa ni shida kuanzia kwenye Halmashauri lakini wamekuwa ni shida mpaka kwa Wavuvi, sasa wamebadilisha namna ya kufanyakazi zao wanaanza kuwasumbua wavuvi usiku na kuwabambikizia kesi na kesho asubuhi kuwapiga faini isiyopungua milioni tano hii kitu haiwezekani ni lazima tufikirie namna iliyobora kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi hasa samaki bila kutumia nguvu nyingi ambazo leo wanatumia hawa BMU. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaishauri Wizara ifanye mpango mkakati mzuri zaidi wa kuangalia namna ya kutunza na kuangalia hizi rasilimali za Ziwa kwa kutokuwatumia hawa watu ambao wanatusumbua sasa hivi, wavuvi wanawakimbia wanapigana na Mheshimiwa Ulega, nafikiri Bunge lililopita nilikuletea hizi kesi kuna watu Wanne walikufa kwa sababu ya kupigania na hawa watu wa BMU ni lazima tutafute namna iliyobora ya kuwasaidia Watanzania, namna iliyobora ya kuwashauri hawa wavuvi kutumia nguvu ambayo ni rafiki na isiwe nguvu ambayo ni hasi na kuendelea kupata maafa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili jambo pia kuna Maafisa wa Uvuvi kutoka Wizarani, hawa watu wanapoenda kwenye Wilaya zetu wanakuwa watu tofauti kabisa na Maafisa Uvuvi wa Halmashauri, unafikiri ni taasisi mbili tofauti, utafikiri ni nchi mbili tofauti, hawa watu wa Wizara wanakuja na sheria zao, watu wa halmashauri kuna Afisa Uvuvi nae ana sheria zake, anafahamu hivi, hawa wanafahamu hivi wanawatesa wavuvi bila sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ninakuomba haya malalamiko tumeyaleta, tunaomba Maafisa wanaotoka kwenye Wizara ya Uvuvi, wanapofika kwenye Halmashauri zetu wawasiliane na Maafisa Uvuvi wa Halmashauri ili wawe kitu kimoja kwa ajili ya utekelezaji wa kazi ambao mtakuwa mmewatuma kwenda kufanya. Mimi kama Mbunge nikimuuliza Afisa wa Halmashauri anasema mimi sijui, siyo maagizo ya Wizara lakini Wizara wanasema haya ndiyo maagizo ambayo tumepewa sasa mnawatuma hivyo ni lazima waende wakashirikiane na watu wa Halmashauri ili wafanyekazi iliyobora na haya itatusababishia sasa wananchi wetu waweze kujifunza kupata elimu chanya kutoka kwa hawa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikiwaza mara nyingi tunapokuwa tunakomesha uvuvi haramu na tunaenda kumkatamata mvuvi, tunaenda kukamata samaki sasa najifikiria suala moja, hivi tumeshawahi kufikiria hao wanaoleta hizi nyavu? Tumeshawahi kufikiria juu ya viwanda, hivi inakuwaje mvuvi anaenda kununua nyavu na mwisho wa siku anaenda kukamatwa lakini kuna mtu ameingiza nyavu kapitia bandarini, kuna kiwanda kinatengeneza nyavu kipo Tanzania, haiwezekani katika akili ya kawaida! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Wizara sasa ifanye jukumu lake, kama kuna kiwanda kinatengeneza nyavu ambazo si halali ni lazima tuanzie huko kwenye chanzo badala ya kwenda kumsumbua Mtanzania ambaye inawezekana ni layman kama mimi, hajui chochote hata hizo tunazoita sentimeta Sita za nyavu yeye hajui, anapewa nne lakini kumbe ninyi mnataka sita na mwisho wa siku mnamkamata na faini Milioni 20! Mtanzania anauza nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana kwenye hili tuanzie kwenye viwanda, tuanzie kwa watu wanaoingiza hizi nyavu, najua Ulega upo smart kwenye kukesha, nenda kakeshe bandarini, nenda kakeshe huko kwenye viwanda kuhakikisha kwamba hawa wanaoingiza nyavu ambazo siyo salama muanze nao huko kabla hamjafika kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia najifikiria swali moja, samaki anaenda kukamatwa pale sokoni kapita tayari Ziwani kuna mtu kakatisha ushuru, kachukua hela ka-deposit hela za Serikali tayari lakini mwisho wa siku mtu anaenda kukamatwa kwamba samaki siyo saizi inayotakiwa! Sasa najiuliza huyu aliyechukua ushuru wake yeye hawakuwaona hawa Samaki? Ni Mtanzania huyohuyo tunampa hasara mara mbili, Lazima tutafakari kama samaki alikuwa na shida, shida ianzie ziwani palepale na asiende kukamatwa kule sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine nichangie kwenye suala zima la mikopo. Siku zote tumekuwa tukiambiwa kuna mikopo ya wavuvi lakini wavuvi wa vijijini kama Busega hawanufaiki na hii mikopo, hawanufaiki na mikopo ya vikundi kwanini? Kwa sababu sijajua kama hii mikopo inaishia Mjini kule Vijijini haifiki. Mheshimiwa Waziri Mashimba nilishakufikia, nilishakuambia suala hili tusaidieni wananchi wetu nao waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na Wizara yako ili waweze kupata vifaa vya uvuvi kama vile engine, kama vile nyavu waweze kununua kutokana na ile mikopo ambayo mtakuwa mmewapa. Niombe sana suala hili tulichukulie maanani lakini kama itabidi Wizara yako watu watoke maofisini waende huko site wakawafundishe namna ya kuunda vikundi ili hawa watu waweze kujua namna ya kuunda vikundi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani sana Wizara yako sasa iamke kuhakikisha kwamba tunaenda kufanyakazi yenye tija kwa wananchi hasa wa Jimbo la Busega ambako kuna Ziwa nawewe bahati nzuri umefika mahapa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ulifika pale Nyamikoma tukiwa na wewe, alianza kufika Mheshimiwa Mpina akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi lakini pia na wewe ulivyoteuliwa tu ulifika pale Nyamikoma. Mliahidi kuwepo na mwalo wa kisasa, kwenye bajeti ya mwaka jana mliweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa mwalo lakini mpaka sasa hivi tunavyozungumza hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefika ofisini kwako nimepata majibu kwamba mmetangaza Mkandarasi, ninavyokwambia mpaka leo hakuna cha Mkandarasi, hakuna kinachoendelea katika mwalo wa Wanyamikoma. Ninakupongeza katika mwalo wa Ihale angalau kazi imefanyika pale tulipata milioni 162 ninakushukuru sana Ulega ulifika pale tukapiga siasa kidogo, wananchi wakafahamu juhudi ambazo unazo, lakini sasa tumalizie na huu mwalo ambao tumekuwa tukiuahidi zaidi ya awamu tatu. Mheshimiwa Mpina aliahidi pale nafikiri ilikuwa mwaka 2018 na wewe Mheshimiwa Mashimba umeahidi pale 2021 sasa tuende tukafanye kazi tupate fedha ili tuweze kutengeneza ule mwalo wa kisasa kama ambavyo uliahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna suala ambalo nilichangia hata bajeti iliyopita. Mmekuwa mkisema kuna ukosefu wa samaki viwandani. Nami nafikiria suala moja, tutaendelea kusema hakuna samaki kwenye viwanda vyetu kwa sababu ya bei ya samaki. Hakuna mwananchi ambaye anateseka usiku kucha ataenda kuuza samaki kilo moja kwa Shilingi 8,800/=. Hakuna mwananchi atakayeenda kuuza samaki kilo tano, kwa maana ya kilo moja kwa Shilingi 11,500 likiwepo na bondo lake, haitawezekana, kwa sababu bondo lina bei kubwa. Mwananchi anaamua sasa bora agawe zile samaki kipande kipande, auze kidogo kidogo, lakini mwisho wa siku anufaike na bondo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilishauri Wizara mwaka 2021, mkitaka kufanikisha eneo hili na kuwasaidia Watanzania, ni lazima ijulikane kiwandani, bei ya mnofu ijulikane, na bei ya bondo pia iweze kujulikana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Simon.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja.