Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuwa hai na kuwa na afya njema ya akili jioni ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Mtwara. Mtwara tuna Bahari ya Hindi yenye kina kirefu na samaki wengi sana tu, lakini tunashindwa kuwapata kwa sababu ya uwekezaji finyu katika sekta hii, hivyo kupelekea uvuvi kuonekana kama ni shughuli ndogo ndogo ya watu wanyonge ambao hawajiwezi. Ukisoma, utaona kuna nchi nyingi duniani zimenufaika, zinaingiza pato kubwa la Taifa kwenye nchi zao kutokana na sekta hii ya uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua hii Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina watu wawili. Mheshimiwa Ulega yeye ni mtaalam wa uvuvi, tulitarajia kwamba tunavyokwenda kwenye mambo ya uvuvi, kwa sababu yupo mtaalam, aweze kulipeleka hili gurudumu mbele. Mheshimiwa Ndaki yeye ni mtaalam wa mambo au ana uzoefu na mambo ya mifugo, tulitarajia kule kwenye mifugo nako kufanye vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa sana la kusikitisha, miongoni mwa Wizara ambazo mimi naweza kusema kama Serikali haizitilii maanani ni Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Wakati mwingine tunatamani kuwalaumu hawa Mawaziri, lakini watafanya kazi wakati fedha hawana? Mimi ndiyo swali langu la msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2021 wakati nachangia kwenye Wizara hii, nilisema nimepata mshtuko, watu wakacheka. Nilisema nimepata mshtuko kwa sababu fedha za maendeleo ambazo zimetengwa ni nyingi wakati hii Wizara hawawapi fedha, kwa nini wanawaacha wanatenga fedha nyingi na hawawapi? Kilichotokea ni nini? Wamewatenga fedha za maendeleo kwenye Sekta ya Uvuvi, (mimi leo nitajikita tu kwenye uvuvi) wametenga Shilingi bilioni 99.14; fedha za ndani shilingi bilioni 62.5 na fedha za nje shilingi bilioni 36.5.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka tunakuja leo kwenye Hotuba ya Waziri, fedha ya maendeleo ambayo imepelekwa Wizara hii ni Shilingi ngapi? Shilingi bilioni 3.95. Tunakaa hapa tunafanya nini? Huyo ndio unamtegemea sasa aende akafanye shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye sekta ya uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakupa mifano michache, si tuliwapitishia hizi! Kazi ya Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali, tukapitisha, tukasema tunawashauri, tunawasimamia; sijui tumefeli kuwasimamia, sielewi, lakini habari ndiyo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakupa mifano, katika bajeti ile walikuwa na malengo, pamoja na mambo mengine wanasema: “ukarabati na utanuzi wa kituo cha ukuzaji viumbe maji, Ruira Songea. Shilingi ngapi imetengwa? Shilingi milioni 791. Mpaka hapa tunapoongea, hata shilingi 10/= haijaenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati na utanuzi wa kituo cha ukuzaji viumbe maji Nyengedi, Lindi; kuna Tandahimba huko kwetu Mtwara na wapi; shilingi ngapi zimetengwa? Shilingi milioni 715; mpaka leo tunapoongea hata shilingi 10 haijaenda. Ujenzi wa kituo cha ukuzaji viumbe maji bahari cha Ruvula, kipo Mtwara kwetu huko; shilingi ngapi? Shilingi milioni 983; mpaka hapa tunapoongea, hata shilingi 10 haijaenda. Sasa nimekupa mifano michache. Kuna watu wa TAFIRI ndiyo tunategemea huko utafiti na vitu vingine vikafanyike. Walitengewa shilingi milioni 700; hata shilingi 10 haijaenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakaona wajifariji kidogo, wakapunguza tena bajeti ya maendeleo kwa mwaka huu ambao tunaoujadili; kujifariji tu kwa sababu umetoka shilingi bilioni 99, umepewa shilingi bilioni tatu. leo unapunguza, shilingi bilioni 92, unataka kuniambia huo muda uliobaki ninyi mtapata hizo fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, concern yangu kubwa, sisi tunaotoka maeneo ya wavuvi, tunajua ni namna gani Sekta ya Uvuvi ina umuhimu kwa watu wetu na kwa wananchi wetu. Yaani kama mnavyoona kwenye maeneo mengine, wao wana migodi huko ya madini wanachimba wanapata fedha, nasi tunaotoka kwenye maeneo ya uvuvi, tunajua umuhimu wake. Kutufanyia mambo kama haya, siyo sawa. Wapeni hela hawa Mawaziri wafanye kazi, tuje hapa tuwaulize hawafanyi kazi wakati fedha mmewapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha yupo hapa, mwaka 2021 alitusikia, na leo anatusikia, na nawaambia tukirudi mwakani Mwenyezi Mungu akitupa uhai, tunakuja kuyajadili mambo haya haya. Tunafanya mambo gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa, kule Kilwa Masoko wametenga shilingi bilioni 50 mwaka 2021 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya uvuvi, haikutoka hata shilingi 10; mwendelezo ule ule! Mwaka huu tena wametenga shilingi bilioni 59, Mheshimiwa Waziri akija hapa kumalizia hoja yake, naomba atueleze zile shilingi bilioni 50 za mara ya kwanza zinakwenda lini? Vile vile hizi zitakwenda? Tunachotaka sisi, bandari ile ikijengwa vizuri ndiyo ile dhana ya Uchumi wa Bluu inaanzia hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jamani, hivi tangu nchi hii ipate uhuru, leo ni miaka sitini ngapi, bado tunazungumzia watu wanaenda kuvua na boti za kusukuma na makasia? Wapeni fedha TAFIRI wafanye utafiti, wawaambie watu samaki wako wapi? Waambie watu mazalia ya samaki yako wapi? Mnafanyaje, hamtoi fedha? Kuna Waziri, kuna Katibu Mkuu, wanafanya nini kama Serikali, kama Wizara ya Mheshimiwa Mwigulu haitoli fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na kusema hii Wizara haifanyi kazi, lakini anayekwamisha kwa kiasi kikubwa Wizara hii isifanye kazi ni Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. Kwa hiyo, tukimtafuta mchawi, wa kwanza ni Wizara ya Fedha na Mipango. Yaani hawa watu wa Mifugo na Uvuvi, nitakuja kuwasema hapa baada ya kuona wamepewa fedha na wameshindwa kufanya kazi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante, ni kengele yako ya pili.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, lakini ujumbe huo ufike na ufanyiwe kazi. (Makofi)