Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kinipatia nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya makadirio na mapato ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Pili, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake pamoja na watendaji wake wote kwa kutayarisha na hatimaye kuiwasilisha hotuba hii katika Bunge lako tukufu kwa ufasaha na umakini mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hotuba hii napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kuhusu unyanyaswaji wa wavuvi katika baadhi ya bandari; napenda kuchangia hotuba kwa kutoa masikitiko yangu makubwa juu ya namna ya tabia mbovu ya baadhi ya Maafisa wa Uvuvi wanaojuilikana kama watu wa marine. Watu hawa wamekuwa wakiwapa shida kubwa wavuvi hasa wanaotoka upande mmoja wa Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, wavuvi wanaotoka Zanzibar wamekuwa na utaratibu wa asili kuja kuvua huku Bara. Wanapotoka Zanzibar huwa wanakuja na vielelezo vyote vinavyohalalisha kuwepo kwao. Vielelezo hivyo ni pamoja na leseni za uvuvi, barua kutoka maeneo wanayotoka kwenda maeneo wanayofikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachosikitisha ni kwamba wakifika katika maeneo husika huwa wanaambiwa kuwa vielelezo vile havitambuliki na kutakiwa kutafuta vingine kwa bei kubwa sana.

Aidha wanapoenda kuvua huwa wanawavizia na kuwasingizia kuwa wameharibu mazingira, hatua hii huwapelekea kuwanyang’anya leseni zao za uvuvu na kuwapiga faini kubwa sana ambayo kuna wakati huwa wanashindwa kulipa. Wanaposhindwa kulipa huwa wanawanyang’anya mashine zao za uvuvi mpaka watakapokamilisha malipo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya bandari hizo zinazowapa shida wavuvi ni pamoja na Mnyanjani, Mwarongo, Kigombe na Mwarongo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu katika jambo hili kwa Wizara ni kufuatilia tatizo hili mapema kabla halijageuka kuwa ni kero za Muungano ambazo Serikali yetu inajitahidi sana kuziondoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.