Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bagamoyo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushukuru sana kwa kupata nafasi ya kwanza katika uchangiaji wa leo. Kwanza kabisa napenda nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kupata tuzo ambayo imeiheshimisha nchi yetu kimataifa. (Makofi)
Pili napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mama yetu Mabula, Naibu wake Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Katibu Mkuu na iongozi wote wa Wizara, kwa kweli kazi kubwa wanaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mchango wangu nianzie katika suala la muster plan, sasa hivi nchi inajitahidi sana na hasa Wizara kuhakikisha kwamba master plan zinakaa vyema katika nchi yetu, lakini mimi ningependa tu niwashauri Wizara hii master plan wasiziachie Halmashauri zetu, waibebe moja kwa moja Wizara ndio washughulike nayo, kwa sababu Halmashauri zetu fedha zenyewe ni za kuokoteza na zina mambo mengi kwa hiyo miradi ya master plan katika Halmashauri tukiiachia miradi hii itachelewa sana kufanyika kwa sababu uwezo wetu ni mdogo wa kukusanya fedha katika Halmashauri ili tuweze kumudu gharama za master plan.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Wizara inatakiwa kwamba itoe fedha zote kuhakikisha kwamba master plan zinakuwa katika miliki yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nilikuwa nataka kuzungumzia ni suala la Serikali kuchukua ardhi za watu bila fidia. Imekuwa ni tatizo sugu sasa Serikali kuchukua ardhi pasipo kulipa fidia, mfano mmoja ni kule kwangu Bagamoyo EPZA wamechukua ardhi wa wananchi wa Zinga kwa miaka sasa 13 watu bado hawajalipwa fidia, lakini EPZA ipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, lakini katika hili dhambi zote na lawama zote zinawaangukia Wizara ya Ardhi kama vile wao ndio wahusika wakuu, lakini wao kazi yao ni kupima tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwaomba Wizara ya Ardhi mjaribu sasa hivi kuangalia kwamba mtakapowapimia…
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge wa Bagamoyo kwamba mchango wake mzuri sio tu eneo la Bagamoyo, EPZA kwenye kanda zote kumi ambazo wamechukua wameendeleza Kanda tatu tu, na hawajalipa maeneo mengi zaidi ya miaka kumi ikiwepo na Kata ya Guta, Bunda Mjini, ahsante.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Muharami, taarifa?
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa, kwakweli hali inahuzunisha na inasikitisha ukienda kwa wakazi wangu wa Mlingotini wakazi wa Zinga, wakazi wa Pande, wakazi wa Kondo, wana malalamiko makubwa sana kuhusu EPZA miaka 13 sasa bado hawajalipwa na unakuta unakwenda kuongea na wazee mtu unamkuta mzee ana umri wa miaka 70 analia anatoa machozi, haki yake hajapewa bado eneo limezuiwa hawezi kuuza, akienda ardhi anaambiwa eneo hili limeshawekwa GN ni mali ya Serikali hauwezi kufanya chochote. Sasa hii kwa kweli mimi naomba sana Serikali iliangalie upya Wizara ya Ardhi msiwapimie EPZA wala TIC, wahakikishe kwamba fedha ipo ubaoni ya kulipa wananchi ndio muwapimie, vinginevyo mtabeba lawala ninyi wakati nyinyi mnafanya kazi yetu kwa uzuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la migogoro ya ardhi; migogoro ya ardhi bado ni mingi kiasi kwamba inaanza kupungua Wizara inajitahidi sana, nimpongeze sana Waziri aliyepita Mheshimiwa Lukuvi kazi kubwa aliifanya alikuja kwangu tarehe 19 Julai, 2021 kwa kweli tulifanya mikutano kama miwili mikubwa sana na wananchi na aliwatia msukosuko baadhi ya watu kiasi kwamba kidogo mambo sasa hivi yanaanza kutulia, kwa kweli wanajitahidi sana Wizara katika kuhakikisha kutatua migogoro ya ardhi bado ni mingi, halafu wajitahidi kuzielekeza na kuzishawishi Mahakama za Ardhi kuhakikisha kwamba wanafanya kazi zake kwa uharaka zaidi maana yake masuala ya ardhi yanapokuwa mahakamani yanachukua muda mrefu, yanachukua miaka mingi kiasi kwamba haki za watu zinakuwa zinapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ninataka kuzungumzia suala la wananchi wangu la Lazaba Makurunge, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri umekwenda kule, umezungumza na watu wa Batini, lakini Lazaba inatatizo kubwa, wananchi wengi la Lazaba walikuwa wakiishi katika ardhi ya Serikali ambayo mwaka 2016 Mheshimiwa Rais Hayati Magufuli alimkabidhi mwekezaji Bagamoyo Sugar ambaye ni Bakharesa hekta 10,000 ambazo zilikuwa zikiishi watu ndani yake. Baada ya kukabidhi fidia zikafanyika, lakini wananchi wale hadi sasa bado wana tangatanga hawana pa kukaa, wanakaa katika eneo la Serikali bado na hadi sasa hawajielewi wanakwenda wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lile la Lazaba lilikuwa na hekta 28,000 hekta 10,000 amepewa mwekezaji, hekta 6,000 ni mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hekta 12,000 bado zimebaki mali ya Serikali. Kwa hiyo niiombe Wizara iwafikirie wale watu japo kuwapa hekta 1,000 tu waweke makazi kwa sababu hadi sasa yule mwekezaji bado anapata changamoto ya kupata rasilimaliwatu, anaenda kufuata rasilimaliwatu kilometa 25 wakati pale wangepewa makazi watu ambao jirani na mwekezaji watu wangeweza kuishi na wakafanya kazi katika kiwanda ambacho kinajengwa na mashamba ya miwa wakapata riziki zao.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, muda wako umekwisha. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)