Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kawe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja hii ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendelea na Makazi.
Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa bidii anazofanya kuzunguka kwenda kila mahali kutupigania sisi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hoja hii ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nataka kuzungumzia kwa habari ya migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali Tanzania, lakini kwa kuwa mimi ni Mbunge wa Jimbo la Kawe nataka tu nijikite zaidi kuzungumza kwa habari ya migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Kinondoni. Lazima nikiri kwamba Wilaya ya Kinondoni imekuwa ndio kinara wa migogoro ya ardhi inayochochewa na viongozi wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu sana ku-note hilo jambo kwamba inachochewa na viongozi wa Serikali. Viongozi wa Serikali badala ya ku-solve matatizo ya wananchi kuna baadhi ya viongozi wasio waaminifu wanachochea migogoro ya wananchi na kuwachonganisha na Serikali yao. Nitoe mfano mmoja; kuna kisa kimojawapo ambacho kimetokea kwenye eneo linaitwa Mbweni Mpiji. Mbweni Mpiji siku moja nikapigiwa simu na Katibu wangu (Katibu wa Mbunge) kwamba kuna matrekta, kuna buludoza zinabomoa nyumba za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikakimbia pale Mbweni Mpiji kwenye Kata ya Mbweni jambo la kusikitisha kweli nilikuta nyumba 103 kubwa zimeanguka chini na mbaya zaidi nikakuta baadhi ya watoto wameachwa kwenye hizo nyumba, polisi wanapiga mabomu, kina mama wanachapwa viboko na polisi wamejaa kwenye eneo hilo, sikuamini kwamba hii ndio Tanzania ninayoijua, kilichonishangaza ni kutaka kujua nini sasa kimetokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikamuona OCD kumuuliza je, kuna oda yoyote ya Mahamaka (eviction order) ambayo wewe umekuja kusimamia kubomoa nyumba za wananchi hana, nikawafuata viongozi waliokuwepo pale kama wana hati yoyote hawana, jambo la kushangaza lilikuwa ni hili kwa nini mnabomoa nyumba za wananchi! Wakasema tunabomoa nyumba za wananchi kwa sababu eneo hili kwenye mpango limepangwa kuwa bustani ya miti ya Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbuka haijajengwa hiyo bustani, haipo wananchi wamejenga nyumba zao zaidi ya miaka mitano wanaishi, mtu anakwenda kuangusha chini nyumba za wananchi 103 maskini, wananchi walewale ambao mwaka 2020 tumepita tukiwaomba kura za Mheshimiwa Rais na za Mbunge, leo nyumba zao 103 zimeanguka chini wanawake na wanaume wamekamatwa wamepigwa, huyu polisi/OCD anaye-executive hii order hana document yoyote, wanaobomoa hawana document yoyote na hakuna hata mmoja mwenye document. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inashangaza kweli kweli, nikazungumza waliokuwepo Maafisa wa Manispaa, wakasema wameelekezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, nikazungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri Dada Hanifa akasema hajawaelekeza, hawana maelekezo yoyote ya kwake, baadaye wakahamia kusema kwamba wamelekezwa na Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inashangaza kweli viongozi wa kiserikali waliowekwa kwa ajili ya kutetea wananchi, wanakuwa sehemu ya mgogoro ya kuwagombanisha wananchi na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri kukubali kiongozi yeyote ama wa kisiasa ama wa Serikali inayotokana na Chama cha Mapinduzi jukumu lake la kwanza ni kuhakikisha Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi amekaa kwenye kiti salama na yuko salama katika shughuli zake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inapotokea kiongozi ama wa kiserikali ama kisiasa anayetokana na Chama cha Mapinduzi hafanyi jukumu hilo basi huyo ni hujuma juu ya Rais wetu na ni hujuma juu ya chama chetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ninapoongea sasa hivi Jimbo la Kawe, lina migogoro ya ardhi mingi hakuna anayeonekana kujali kusuluhisha migogoro hii. Nimefurahishwa sana wiki iliiyopita na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi rafiki yangu Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, nilizungumza na yeye pamoja na Mheshimiwa Nape wakaja kwenye Jimbo la Kawe kwenye Mtaa wa Jogoo na Ndumbwi, ambao wananchi walikuwa wamezuiwa kuwekewa postcode kwa sababu eneo hilo kwenye mchoro linaonekana eneo la viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbuka ni zaidi 4,500 zimejengwa mle ndani na hakuna kiwanda chochote, hakuna kesi yoyote, hakuna anayewadai, lakini wananchi wamezuiwa kuwekewa postcode kwa sababu linasomeka kwenye ramani ni eneo la viwanda, wameishi miaka 30, Mheshimiwa Nape na Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete wakakaa pale ndani ya masaa mawili, walishatatua mgogoro ulioshindikana kutatuliwa ndani ya miaka 30 iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwambia Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete pamoja na Mheshimiwa Nape mmefanya kazi nzuri sana na hiyo ndiyo kazi ya kiongozi. Leadership is making decision wether negative or positive, ni afadhali kwa kulaumiwa kwa kufanya maamuzi yasiyo sahihi kuliko kutokuamua kabisa kabisa, nawapongeza sana kwa hiyo kazi mliyofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi viongozi wengi wa kiserikali wasio waaminifu wanachochea migogoro na kumgombanisha Rais pamoja na wapigakura wake. Kwa mfano, kwa dakika chache tu, kule kuna eneo linaitwa Mwembetogwa Boko Chama jana tu wamefika pale wameleta polisi kuwa-harass wananchi, kesi ipo mahakamani lakini wananchi wanakuwa harassed, watu zaidi ya 200 wametolewa kwenye makazi na kesi ipo mahakamani.
Ninaomba sana Wizara ya Ardhi mshughulike sana na suala la migogoro ya wananchi ili tumsaidie Mheshimiwa Rais kuwa na kura zake zilizonona katika Jimbo la Kawe na kuondoa uchonganishi kati ya wananchi na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)