Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutupa afya njema na kibali cha kusimama mahali hapa.
Mheshimiwa Spika, lakini namshukuru sana na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa kuanzisha Wizara hii mama ambayo inashughulika na ustawi wa jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katia hotuba ya bajeti ya Wizara hii iliyoko mbele yetu kuna vipaumbele kadha wa kadha ambavyo wameviweka. Moja ya kipaumbele ni kuendelea kuimarisha huduma za ustawi wa jamii na haki kwa familia na watoto ikiwemo malezi ya kambo na kuasili, malezi makuzi na maendeleo ya jamii, lakini zaidi ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na maendeleo ya awali, ulinzi na usalama kwa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili.
Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la ukatili wa kijinsia, ukatili wa kingono, ukatili wa kifikra, lakini ukatili wa kimwili. Ukiangalia hasa katika Mkoa wa Shinyanga inaonesha kabisa ni dhahiri kwamba kuna ukatili mkubwa wa kijinsia. Ukiangalia takwimu inaonesha kwamba kutoka Juni, 2020 hadi Disemba, 2021 ukatili wa kingono kwa watu wazima umekuwa na matukio karibia 217; lakini kwa watoto ukatili wa kingono watoto jumla 661 wamefanyiwa ukatili wa kingono. Katika hiyo idadi ya watu wazima 217 ambao ni wanawake kwa wanaume waliyofanyiwa ukatili wa kingono, kesi ambazo zilipelekwa Mahakamani ni 149 kati ya 217 na ambazo zilipelekwa Makamani zikahukumiwa ni kesi 80 peke yake. Hii inasikitisha sana, watu wazima 217 lakini watoto 661, kesi ambazo zimepelekwa Mahakamani ni 149 tu na ambazo zimekuja kuamuliwa kesi 80 hii haikubaliki. Tatizo ni nini, hapa kuna tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jamii yetu imekuwa ikinyanyasika katika ukatili wa kijinsia, ukatili wa kingono, ukatili wa kimwili, lakini ukatili wa kihisia. Kesi zinapelekwa Mahakamani na ukizingatia sheria hii ya watu wanaofanya ukatili hasa la suala zima la wanaobaka, wanaolawiti, wanaofanya vitendo vyovyote vile vya unyanyasaji wa kingono, sheria inampa dhamana mhusika, wakishawekewa dhamana wanatoroka, kesi zinapotelea hewani.
Ningeomba Mheshimiwa Waziri kama inawezekana sheria inawa-favor wale watu ambao wanafanya uhalifu, basi sheria iletwe hapa Bungeni tuweze kurekebisha. Kwa sababu kama mtu anahujumu uchumi, anakuwa hana dhamana, je, anayehujumu uhai wa mtu inakuwaje, hili halikubaliki. Tunajenga kizazi ambacho kinakuwa na maisha magumu, angalia watoto wa mitaani walivyo wengi, ukitafuta historia ya hawa watoto ni wengi ambao wamenyanyasika majumbani na watu ambao wanawanyanyasa hawa watoto au wanawafanyia vitendo vya ukatili ni watu ambao wanatuzunguka, wanaweza wakawa ni ndugu zetu, wanaweza wakawa ni majirani, wanaweza wakawa ni walimu. Lakini anapobainika ya kwamba amefanya ukatili akafikishwa kwenye chombo cha sheria anahaki ya kupata dhamana. Akishapata dhamana, amewekewa dhamana na watu wanne anatoroka, anakwenda kusikojulikana, huko kusikojulikana ni wapi ambako hawezi kupatikana. Ninafikiri kuna umuhimu wa sheria hii kubadilishwa ili hawa watu ambao wanaowabaka watoto wetu, ambao wanafanya ukatili kwa jamii wasiwe na dhamana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inasikitisha kule Shinyanga mwaka huu mapema mtoto wa mwaka mmoja na miezi 11 alifanyiwa ukatili wa kingono na baba yake wa kambo. Mtoto akaharibika vibaya, Shinyanga Government pale ikashindwa kumtibu ikampeleka Bugando. Lakini huyu mtu aliyefanya unyama huu bado ana haki ya kupata dhamana, kweli akipata dhamana akakaa nje anajua kabisa kwamba ninathibitika nilifanya huu ukatili atabaki, si atakimbia. Vitendo vimeongezeka na ndiyo maana tunajenga jamii ambayo inakuwa ina ukatili, ukiangalia wale watoto wako mitaani Dar es Salaam au hapa Dodoma, wanavuta unga, wanavuta gundi ni kwa sababu ya malezi na ukatili ambao yumkini wamefanyiwa kule nyumbani.
Mheshimiwa Spika, tunatakiwa tuziangalie sheria zetu vizuri, kuangalia ni kwa nini wanapata hiyo favor ndiyo ni haki na ninajua wanasheria sasa hivi wanaoshughulika na haki za binaadam wanajitahidi sana kuhakikisha kwamba inakuja sheria ya makosa yote kuwa na dhamana, lakini kwa kosa la ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanaume na wanawake halikubaliki hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ningependa pia nizungumzie kidogo kuhusu suala zima la mikopo ya wanawake, vijana pamoja walemavu. Kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuhamasisha na kuendelea kuhakikisha kwamba fedha kwa ajili ya mikopo ya wanawake, fedha kwa ajili ya mikopo ya vijana, lakini na watu wenye makundi maalum - walemavu wanapata. Niwapongeze sana, sana Wakurugenzi wa Mkoa wa Shinyanga, sisi Shinyanga katika 10 percent ya mikopo hii ambayo wanapewa watu wenye makundi maalum nikiwa na maana ya wanawake, vijana pamoja na watu wenye ulemavu jumla ya shilingi bilioni 18 zimeweza kutolewa katika Mkoa wetu wa Shinyanga hadi kufikia Februari, 2022.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli nawapongeza sana Wakurugenzi pamoja na Waheshimiwa Madiwani kuhakikisha kwamba wanasimamia hizi fedha, ili wanawake waweze kunufaika ni zaidi ya asilimia 91 ya mapato ya ndani kwa kweli ni kazi na ni hatua kubwa sana. Lakini nimpongeze Rais pia kwa kuwajali Wamachinga amewaweka katika group la makundi maalum, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais na tunasikia sijui ilikuwa tarehe ngapi pale, aliweza kusema kwamba atawapa shilingi milioni 10 wamachinga Tanzania nzima kila Mkoa. Kwa kweli hili ni suala la kumpongeza ni jinsi gani ambavyo anawathamini wananchi wake, ni jinsi gani ambavyo anataka kila mtu ajikomboe kiuchumi kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ningependa kuishauri Wizara ya Maendeleo ya Jamii, hii mikopo pamoja na kwamba inatolewa na haya makundi, lakini kule vijijini sina hakika kama hii mikopo kule vijijini inawafikia walengwa wengi. Mikopo mingi hii inatoka kwenye vile vikundi vya mjini ambavyo watu tayari wanauelewa wa nini wanafanya au tayari wameshaanza biashara zao. Ningeomba mjielekeze katika sehemu ambazo ziko pembezoni kule wanawake wana uhitaji, wanawake wanataka kufanya biashara lakini hawajui waanze kufanyaje hiyo biashara.
Mheshimiwa Spika, tungeomba Wizara kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao wako kule pembezoni waweze kuwafikia wanawake wengi, waweze kuwafikia vijana wengi, waweze kuwafikia watu wenye ulemavu ili basi waweze kujikimu na wao waweze kufanya biashara. Lakini ningeomba hili suala la kujenga vituo vya wamachinga ninaomba Serikali ilichukue kwa uzito mkubwa. Tumeona baadhi ya mikoa mfano hapa Dodoma kuna sehemu ambapo inajengwa hilo soko la wamachinga kwa kweli ni soko zuri. Basi hata mikoa mingine iweze kuiga huo mfano, ihakikishe kwamba wamachinga wanatengewa sehemu nzuri, wanaweza kufanya biashara zao bila kubugudhiwa, wanaweza kuendelea kuongeza pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kunipa hii nafasi ninaomba Wizara hii iwajali pia wale watu ambao ni wanasaikolojia. Tunajua watu wakishafanyiwa ukatili wa kijinsia, wakishafanyiwa ukatili wa kiuchumi, wakifanyiwa ukatili wa aina yoyote ile kisaikolojia wanakuwa hawako vizuri. Kuna hawa watu ambao wamesoma wako barabarani, hawajapata ajira…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, wanasaikolojia tunaomba waajiriwe ili kupunguza tatizo. Nakushukuru sana. (Makofi)