Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu, hoja ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Mheshimiwa Spika, nami pia naomba niungane na wenzangu wote waliotangulia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuiunda upya tena Wizara hii na tumeona kabisa faida ya kuundwa Wizara hii na tunaona viongozi ambao wamekuwa wakifanya kazi katika Wizara hii jinsi wanavyofanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa sana ambayo wanaifanya, lakini pia kuandaa bajeti hii. Mimi naomba nijikite katika masuala mawili, kwenye suala la ukatili, lakini sambamba na hilo, uanzishwaji wa madawati ya jinsia katika vyuo vya elimu ya juu na elimu ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wenzagu wengi wamezungumzia, mimi pia naomba nipongeze mikakati mbalimbali ya Serikali ya kuhakikisha ukatili unatokomezwa kwa mpango mkakati yaani wa MTAKUWWA ambao dhamira ya mkakati huu ni kuhakikisha kwamba, ukatili dhidi ya wanawake na watoto unapungua kwa asilimia 50 ifikapo Juni, 2022. Nina taarifa kuwa tathmini ya mkakati huu iko kwenye stage ya consultant kwamba wako kwenye inception report, naamini kabisa ripoti hii itakapotoka itatuonesha hali halisi ya ukatili ilivyo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukurasa wa nane wa taarifa hii umezungumzia kuendelea na kampeni ya kutokomeza ukatili; nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, kwa kweli hata hivyo kama walivyozungumza wenzangu kumekuwa na ukatili wa kingono, ukatili wa vipigo, kuuawa wanawake na wenza wao au waume pia, kuchomwa moto kwa watoto, lakini pia ukeketaji, usafirishaji haramu wa watoto, ubakaji na ulawiti. Ukweli ni kuwa ukatili umekithiri kupita kiasi, na pia, kwa kuwa vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa mbalimbali, matukio yamekuwa yakiripotiwa, utakuta kwamba baba, ndugu wa karibu, wanabaka na kulawiti.
Mheshimiwa Spika, nitoe mfano, hivi karibuni kuna matukio ambayo yameripotiwa, mfano Mkoa wa Kilimanjaro kuna mume amemuua mkewe mbele yam toto wake wa miaka minne. Sasa je, huyu mtoto akikua akili yake itakuwaje?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo ni tatizo, lakini pia kuna mwanaume ambaye amemuua mke wake kwa kumpiga risasi saba, hili tukio limetokea hivi karibuni. Sambamba na hili tarehe 5 Mei, 2022 kuna mfanyakazi kuke Dar es Salaam wa baa aliuawa na mpenzi wake. Tarehe 26 Machi mtoto alinyongwa, lakini sambamba na hilo kuna baba ambaye alimvunja mtoto wake shingo kwa kushindwa kusoma, sasa sijui yeye amesoma kiasi gani mpaka akamuue mtoto wake!
Mheshimiwa Spika, lakini pia unaona kwamba, tunawapa ndugu zetu, rafiki zetu kuweza kutusaidia kutulelea watoto wetu, kuna mama mkubwa naye amemuua mtoto wa mdogo wake. Kwa hiyo, haya mambo kwa kweli, yanatisha.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, ukurasa wa nne wa hotuba hii pia umezungumzia kuhusu utekelezaji wa MTAKUWWA ambao ulianzia Julai, 2017 na utafikia ukomo mwaka 2022, lakini bado kesi zinaonekana zinaripotiwa, nyingine hazifikiwi uamuzi. Kwa hiyo, taarifa pia inaendelea kusema kwamba, pamoja na matukio kupungua kutoka 42,414 mwaka 2020 hadi kufikia 29,373 mwaka 2021, lakini pamoja na takwimu hizo tunazozipata bado ukatili upo. Kwa hiyo, matukio haya tunayapata kwa sababu ya Serikali kufanya kazi kubwa sana ya kuelimisha jamii ili kusudi iweze kutoa taarifa. Kwa hiyo, naendelea kuipongeza Serikali, lakini wito wangu ni kwamba inabidi lazima elimu iendelee kutolewa ili kusudi jamii iweze kuachana na matatizo haya ya ukatili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilitaka kulizungumzia pia, katika shule zetu. Katika baadhi ya shule nako sio salama kwenye madarasa kwa sababu, kuna baadhi ya watoto ambao madarasa ya juu wamekuwa wakiwalawiti watoto wa madarasa ya chini, na hili jambo nalo inabidi lazima tuliangalie kwa kuona jinsi gani tunaielimisha hii jamii jamani kwa sababu hawa watoto inawezekana kuna baadhi ya tabia wanazirithi kutoka katika nyumba zao au katika familia zao. Kwa hiyo, ni budi sasa ifikie wakati jamii ibadilike.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ushauri wangu ni kwamba kwanza niseme Tanzania bila ukatili inawezekana. Kila mtu akichukua nafasi yake, kila mtu kuanzia kwenye ngazi ya familia tuhakikishe kwamba tunawalea watoto wetu vizuri ili kusudi tuweze kupambana na ukaktili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ushauri wangu Sheria ya Kanuni ya Adhabu kuhusu mimba zinazotokana na kubakwa na ndugu wa damu,yaani mahirimu akiwemo baba, mjomba, kaka, baba mkubwa, iangaliwe upya ili iwaondolee sonona wale mabinti na kama itafaa ujauzito huo utolewe na wataalam.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nililokuwa napenda kupendekeza wazazi wa kiume wanaotelekeza watoto wao wawajibishwe, kwa sababu hii pia inasaidia sana kwenye suala zima la ukatili kwa sababu, baadhi ya akinamama wanashindwa kuwalea watoto wao.
Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine naomba nishauri, sheria iangalie jinsi ya kushughulikia madalali wanaosafirisha wasichana wa kazi, kwa sababu wasichana wa kazi nao wamekuwa wakipata madhifa sana huko wanakokwenda. Wengine wanauawa, wengine wanapewa mimba na kufanyiwa ukatili wa aina mbalibali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri mwingine, Serikali iangalie jinsi ya kutoa ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto ambao wanatetea haki za binadamu. Kwa sababu kuna wengine huwa wanapewa vitisho ili kusudi wasiweze kwenda kutekeleza majukumu yao hasa na wale ndugu wa wahanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri mwingine ni kwamba vyombo vya kupambana na rushwa vifuatilie mienendo ya kesi za ukatili wa ngono na ubakaji, kwani kesi nyingi zinapoteza ushahidi, kwamba hawa watu ambao wanafanya hivi vitendo vya ukatili mara nyingi wengine wanakuwa na uwezo wa kipesa au ndugu zao kwa hiyo, inafikia wakati kwamba, haki inakiukwa kwa hiyo, wale ambao ni waathirika wanashindwa kupata haki yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine nilikuwa nashauri Serikali ione umuhimu wa kujenga nyumba salama za wahanga wa ukatili iwapo mtu atafanyiwa ukatili asirudi nyumbani, kwani akirudi nyumbani ndugu watakwenda pale wamrubuni, ili kusudi aweze kubadilisha mawazo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watoto wapewe mafunzo ya kujilinda mapema; kwamba tuwafundishe watoto wetu katika ngazi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Naomba nimalizie. Tuwafundishe watoto wetu ili kusudi waweze kujilinda…
SPIKA: Sekunde 30; muda wako umeshaisha.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)