Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Bunge lako tukufu kuchangia kwenye Wizara hii nyeti, Wizara muhimu sana ya akinamama. Awali ya yote ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan kwa kuunda hii Wizara muhimu sana kwa ajili ya wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanawake wa Tanzania nzima wanatambua sana na wanalijua hili, wanapokuwa wajawazito wanajua Serikali ipo, watajifungua salama na bila gharama yoyote. Kwa bahati mbaya sana kumezuka tatizo ambapo wanawake wanajifungua siyo wote, wanawake wengine watapata bahati mbaya ya kujifungua watoto wakiwa na mgongo wazi, wanawake wale wanakuwa hawajajiandaa chochote kuhusu masuala ya fedha kwamba watatokewa na hilo tatizo.
Lakini tatizo hilo mtoto akizaliwa ana mgongo wazi anapelekwa hospitali, anafanyiwa operation kwa gharama ya shilingi 500,000 mpaka shilingi 1,000,000 wanawake wale uwezo huo wanakuwa hawana. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri alichukue hili kwa umakini sana, hili tatizo ni la Tanzania nzima hasa wanawake wa Mkoa wa Mbeya wamepata matatizo makubwa sana juu ya kujifungua watoto wenye mgongo wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitafurahi sana na nitashukuru endapo Mheshimiwa Waziri atalizingatia hili kuangalia namna gani watapunguziwa gharama ama kuimaliza kabisa gharama za matibabu hayo ya kutibu watoto hao. Ninaipongeza sana Serikali na ninaishukuru sana kwa namna ambavyo wametoa fedha kwenye halmashauri zetu zile asilimia 10. Ile asilimia 10 ni kwa ajili ya wanawake 4%, vijana 4% na kundi la walemavu 2%.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kuishauri Serikali juu ya hili, ninaomba sana kwenye 10% ile iongezwe iwe 15%. Asilimia 15 kwa maana ipi? Asilimia 15 ili kwa wanawake maana wanawake wana majukumu mengi sana, wana mzigo mkubwa sana wa kutunza na kulea familia, ninaomba kwenye 15% hiyo 9% iende kwa wanawake, 3% iende kwa vijana, 3% iende kwenye kundi la walemavu. Ninamaanisha kwamba mwanamke hata mtoto mdogo maadamu amezaliwa ni mwanamke ni kama anaanzia majukumu yake hapo.
Mheshimiwa Spika, ninamaanisha kwamba kundi la vijana watoto wa kike nilikuwa naomba hao waingie kwa upande wa wanawake, nina maana kwamba mabinti hao wakiingia kwenye kundi la wanawake mpaka sasa hivi hiyo fedha inaonekana kama ni ya 4% ni ya wanawake, lakini pia tunakuwa na mabinti huko ndani, kwa hivyo wasichana waingie kwenye kundi la wanawake kwenye mkopo huo ambapo 9% iwe wanawake wakijumuisha na mabinti, vijana lakini vijana ambao ni wa kiume wapate 3% ninamaanisha kwamba mama endapo atasikia mtoto wake anaumwa ambaye ni kijana, mama ndiyo anashughulikia mwanzo mwisho, siyo kwamba atam-charge kijana kwamba nipe fedha zako....
SPIKA: Mheshimiwa Suma kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jackson Kiswaga.
T A A R I F A
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba katika lile kundi kubwa la vijana, pia wapo akinamama humo na nina wasiwasi aina ya mchango huu wakati mwingine unaweza ukatugawa namna unavyowasilishwa kwa sababu pia kundi la vijana ni kubwa, lakini ndani ya vijana pia wapo wakinamama humo. Kwa hiyo ndiyo hiyo nilipenda kumpa taarifa ahsante sana.
SPIKA: Ndiyo maana niliacha amalizie ile hoja yake kama umemsikiliza vizuri anataka hiyo asilimia iongezeke halafu hao mabinti waondolewe kwenye hiyo 4% wanayopewa pamoja na vijana wengine waingie kwenye wanawake. Kwa hiyo, ukitaja wanawake wote wawe kundi moja, ndiyo hoja yake ndiyo maana nilitaka umsikilize amalize halafu ndiyo umpe taarifa.
Kwa hiyo, hoja yako wewe ndiyo ambayo kidogo inaweza ikaleta mushkeli yeye anaenda na hoja yake ya kuongeza asilimia.
Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa ufafanuzi huo na hilo ndiyo lilikuwa lengo langu sana kwamba vijana wa kiume watakapokuwa wamebakiwa na hiyo 3% naamini itawatosheleza sana kwa sababu tutakuwa tumeondoa kundi kubwa la vijana kwa maana mabinti zetu kuingia kwenye kundi la akinamama.
Ninasema hivi kundi la wanawake liongezewe asilimia hizo kwa sababu mama anabeba majukumu mengi sana. Anabeba majukumu ya baba, anabeba majukumu ya hao vijana, anabeba majukumu ya watoto wote kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, mama ana huruma sana kwa watoto kwa baba kwa wamama na kwa kila mtu hivyo basi nitashukuru sana hili likichukuliwa uzito kwamba wapewe akinamama kwa maana ya 15%; ninaomba sana mumshawishi, mshauri hizo halmashauri iongezeke iwe asilimia 15 nasisitiza 9% iwe kwa wanawake, 3% kwenye kundi la vijana wetu lakini 3% kwenye kundi la walemavu nitashukuru sana hili kama litabebwa kwa uzito.
Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kubwa sana hapa nchini hasa kwetu mkoa wa Mbeya, anapokuwa akiishi ama wakioana baba na mama wanaishi pamoja, wanaanza kutafuta tangu shilingi moja pamoja baba na mama, lakini mwisho wa siku ikatokea mama ametangulia mbele ya haki baba atasononeka yeye pamoja na familia, lakini maisha yataendelea atakuwa tu burudani raha mustarehe hasumbuliwi na mtu yoyote.
Mheshimiwa Spika, lakini ikatokea amefariki baba ghafla kwa maana ya mume shida inaingia kwenye familia, shinda inaingia kweli kweli, anajitokeza baba hafahamiki kwenye hiyo familia anasema mimi ndio baba mkubwa, mimi ni mdogo wake, mimi ndio natakiwa niwasimamie, kwenye kusimamia mali kuzitafuta walikuwa tu baba na mama na watoto wao wakimuomba Mungu wafanikiwe kwenye hiyo familia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini watu wanajitokeza from nowhere, watoto hawa hawawajui wanasema unasikia mimi ndio baba yako mkubwa, mimi ndio baba yako mdogo hawawafahamu wametokea wapi? Mbona akifariki mama hawa watu hawajitokezi kuja kumbuguzi baba kwenye hiyo familia. (Makofi)
Nilikuwa ninaomba sana kule kwetu Mkoa wa Mbeya wanawake wajane wanasumbuliwa sana na haya, hivyo basi nilikuwa naomba sana kushauri Serikali ijaribu kuweka kama sio kuweka moja kwa moja kwa maana ya kutokujaribu, iweke mawakili kila Halmashauri ambao watakuwa wanawasaidia wanawake wajane ambao wanapatwa na matatizo kama haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii sheria naona iliangalia upande mmoja, unajua kwenye familia yamkini mama ndio mtafutaji mkubwa, baba ni msimamizi sawa kama kiongozi mkubwa kwenye hiyo familia, lakini akifariki baba ni shida, ni shida ni shida. Hivyo basi hiyo sheria kama ilikuwa imewekwa miaka ya nyuma sana kwamba baba ndio hatakiwi kusumbuliwa endapo mke atakuwa ametangulia mbele ya haki, hiyo sheria naomba ibadilishwe, hiyo sheria naomba ibebe uzito kote kote kwamba mama na baba wanakuwepo pale wanakuwa wanatafuta fedha pamoja, kwa ajili ya familia hivyo basi asisumbuliwe mwanamke yeyote pindi baba atakapokuwa ametangulia mbele ya haki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanawake wana majonzi makubwa sana, naona taa umeiwasha.
SPIKA: Muda umeisha.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nimalizie kidogo.
SPIKA: Sekunde 30 malizia.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana hivyo basi nitashukuru sana kama Serikali italichukulia hili kwa uzito mkubwa kuangalia mama anavyoteseka, mama anavyosumbuliwa na Mheshimiwa Rais ameunda hii Wizara kwa makusudi mazima kabisa ili tuendelee kuwatetea wanawake hapa ndani na katika kuwatetea hawa wanawake ninaomba mlibebe muwasaidie wanawake wanaoonewa pindi wanaume zao wanapokuwa wamekufa…
SPIKA: Haya ahsante sana.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, maana analia mara analia mara mbili analia msiba wa baba/wa mme wake analia msiba wa kupokonywa mali zake zote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, ahsante sana. (Makofi)