Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia katika Wizara muhimu hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo mengi yanayoendelea katika Wizara hii ambayo kwa kweli nisiposema ninakuwa kama sijitendei haki. Nimpongeze Mheshimiwa Gwajima na timu yake wamekuwa wakiendelea kupambana sana kwa kuwafikia wananchi hadi ngazi ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijachangia nilipenda nitumie forum hii kuwashukuru vijana wawili katika Mkoa wa Songwe; Mshomari na Sam Midadi ambao kiupekee wamenitungia wimbo maalum nikiwa kama dada yao ambao imewapendeza wao kwa jitihada zao na bidii yao na fedha kuona wamuimbe dada Neema. Kwa hiyo ninawashukuru sana popote walipo wapokee shukrani zangu za dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nijielekeze katika kuchangia katika wizara hii na ningependa nianze na kipengele cha Ustawi wa Jamii; tunaona katika takwimu tulizoletewa tuna upungufu wa asilimia 97 ya Maafisa Ustawi wa Jamii katika nchi yetu na kimsingi uhitaji au umuhimu wa hawa Maafisa Ustawi wa Jamii unaonekana kutokana na ongezeko la vitendo vya ubakaji, ulawiti, mauaji na pia utelekezaji wa familia ambao umekuwa ukiendelea kwenye jamii yetu. Hivi ni viashiria vya msingi vya kuonesha kabisa kwamba watu hawapo salama afya ya akili ya vijana wengi, wazee wengi na akina baba wengi huko kwetu na wanawake wengi kwa ujumla yaani jamii kwa ujumla haipo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitamani sana kusema neno hili si kwa maana ya kwamba labda nina maana mbaya ila naona kwamba kitendo cha kutokuwa na Maafisa Ustawi wa Jamii inaonesha Serikali kwa namna moja au nyingine imeamua kuhalalisha vitendo hivi vya ubakaji, ulawiti na mauaji na utelekezaji wa familia kwa kutokuwa na mkakati maalumu wa kuhakikisha Maafisa Ustawi wa Jamii tunakuwa nao wengi wa kutosha. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, na…

SPIKA: Mheshimiwa Neema ngoja ngoja kidogo. Hiyo sehemu ya maneno uliyoyasema hapo kwanza yafute halafu uchangie upya hiyo sehemu maana siwezi hata kuyarejea. Kwa hiyo, yaondoe hayo maneno wewe mwenyewe halafu anza kuchangia upya ili pengine ukitumia lugha nyingine tutaelewa vizuri.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, naomba niyaondoe maneno kama ulivyoniambia ila ninataka niseme nini? Nataka niione dhamira ya Serikali kuhakikisha inatoa ajira kwa Maafisa Ustawi wa Jamii kwa wingi zaidi ili changamoto hizi za ubakaji, ulawiti, mauaji na utelekezaji wa familia zinazoendelea katika jamii yetu viweze kupungua. Tunaamini kabisa na tunafahamu kwamba Maafisa Ustawi wa Jamii ndiyo watu wenye elimu ya kuweza kufanya counselling kwa watu wetu na ndiyo watu wanaoweza kusaidia kubadili mwenendo na tabia ya jamii yetu na kufuatilia kwa ukaribu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninataka kuiomba Serikali kupitia forum hii kwamba wahahakishe Maafisa Ustawi wa Jamii wanaajiriwa wanakuwa wengi na mimi sidhani au sielewi ni kwanini Serikali haiipi kipaumbele kada hii kwa sababu hata ukiangalia mara leo wapo Afya, mara leo wapo Maendeleo ya Jamii, sijui kesho watakuwa wapi. Kwa hiyo ninatamani kwamba kada hii ya Ustawi wa Jamii ipewe kipaumbele na ikiwezekana itengenezewe sheria maalumu ya kuilinda taaluma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niseme tu hata kiwango cha bajeti kinachotengwa kwa Wizara hii kinaonesha kabisa dhamira ya Serikali kupambana na vitendo hivi bado haijawa wazi sana. Ninatamani kuona kwamba katika Wizara ambayo ingekuwa inapewa kipaumbele ni pamoja na hii kwa kutengewa fedha ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, ninapenda pia kwenda kwenye eneo la maendeleo ya jamii hususani kwenye hii ya mikopo inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Tunaona ni pesa nyingi inatengwa na tunaona kabisa ubunifu wa miradi unaoendelea kwenye halmashauri si toshelevu, si mzuri kwa maana gani naongea maneno haya tungekuwa na watu wa ku-design miradi wazuri tusingekuwa tunaona ya kwamba projects zinazoendelea ununuzi wa pikipiki tu, bajaji tu kila siku tunatamani kuona kwamba Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii wanakuja na mkakati wa kuajiri wataalamu wa ku-design miradi watakaowafundisha jamii yetu wanawake, vijana na hao watu wenye ulemavu ili kuepuka miradi ya aina moja kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajua kabisa uelekeo wa nchi yetu ulikuwa ni viwanda na hatutajua miradi hii kupitia mifuko ya wanawake yaani kuna miradi gani ambayo mpaka sasa hivi wameweza kuifanya ambayo inaonyesha kabisa uelekeo wetu niwaviwanda. Vikundi vipewe fedha ya kutosha, lakini pia uelekeo ungeendana na hii Sera ya Viwanda ingependeza zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kitu kingine ambacho nilitamani kukiongelea kuna kundi ambao lipo kwenye jamii, hawa mabinti wengine ambao walibakwa wengine ambao walilaghaiwa kwa namna moja au nyingine unakuta wamepata watoto, malezi ya watoto hawa mara nyingi yanakuwa yanayumbayumba. Ninatamani katika eneo hili la maendeleo ya jamii wangekuja na mkakati maalumu wa kuangalia namna ya kuwajengea uwezo hawa mabinti ili wawe na uchumi ambao ni stable, lakini mbali zaidi tunaamini kwamba wakijengewa uwezo hata utapiamlo kwa watoto wetu utakuwa haupo, hawa watu wote watakuwa wana uhakika wa chakula lakini na uhakika wa huduma zingine kama mavazi, malazi na matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nimekiona katika eneo hili la mikopo hii mpaka sasa hivi ni muda mrefu tumekuwa tukiendelea kutoa mikopo, lakini impact assessment ya mikopo hii haipo na ukiangalia mpaka sasa hivi ukiwauliza ni wanawake wangapi wamejikomboa kutoka kipato kipi kwenda kipato kipi au ni vijana wangapi walikuwa na uchumi huu saa hizi wapo uchumi huu taarifa hizi hazionekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kupitia forum hii, Bunge hili tukufu nilitamani kuiomba Wizara wakafanye assessment tuweze kujua tulipokuwa na tunapoelekea ili hata unaposema tunatoa pesa nyingi iwe kweli ni pesa nyingi lakini zenye tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nilitamani kukiongelea zaidi ni katika hili suala la ulinzi wa mtoto; tumekuwa tunaona ni kwa namna mbalimbali ambazo kila mwananchi, kila mtanzania anapambana kulea mtoto wake anavyojua yeye naniwapongeze kwa forum ambayo wameianzisha yakuwa na vituo vya malezi ya watoto katika kila kijiji na ninasikitika tu kwamba vituo vya mfano vyote vipo Dar es Salaam na vingine vinaletwa Dodoma. Mimi nadhani kama mfano ungeanzia kwa kila angalau yaani hata kwa angalau kila kanda kukawa na kituo kimoja ingependeza zaidi kwa sababu tungekuwa tunaendelea kuinua Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi niseme tu, kwa hili nawapongeza na ninaamini kupitia Bunge hili tukufu hiki tutakiona na kukipa kipaumbele na kuhakikisha kila kijiji Tanzania inakuwa na hizi centers za kulelelea watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa nafasi ya kunipa kuweza kuongea. (Makofi/Kicheko)