Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi, awali ya yote ningependa nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Kwa kweli ni jambo lenye tija sana na kwa dhati ya moyo wangu naomba nimpongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna tofauti kubwa kati ya ubakaji na ulawiti kwa watu wazima na ubakaji na ulawiti kwa watoto, na tofauti ni kwamba mtu mzima ana haki ya kuipigania haki yake, anaweza kuipigania haki yake kwa sababu nguvu anazo, utashi anao na maarifa anayo. Sasa hii ni tofauti kwa mtoto mdogo kwa sababu mtoto hawezi kupigania haki yake, haki ya mtoto inapiganiwa kwa utashi wa mzazi wake ama mlezi wake, na hapa ndipo ambapo tatizo linakuja kwa sababu ili haki ya mtoto iweze kupiganiwa inategemea utayari wa mzazi wa kupigania haki hiyo. (Makofi)

Kwa hiyo, mzazi anaweza akachagua mambo tofauti tofauti, kwanza anaweza akachagua aipiganie, lakini la pili anaweza akachugua asipiganie, la tatu akipewa mpunga anaweza akaamua akae kimya. Lakini kama yeye mwenyewe anahusika na matendo ya ukatili hataipigania haki hiyo kabisa. Sasa hapa lazima Wizara ikae na Wizara nyingine ambazo zinahusika ili kuweka mambo sawa. Na lazima wakubali kuweka uwekezaji kwa Maafisa Maendeleo wa Jamii. Nasema hivyo kwa sababu gani, Afisa Maendeleo ya Jamii ndiyo mtu kati ambaye anaweza kulinda haki ya mtoto na akamshurutisha mzazi atafute haki ya mtoto wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafahamu tutasema kwamba labda kuna tatizo la fedha na nini, lakini ulinzi wa haki ya mtoto unategemea hapa tutafanya uwekezaji wa aina gani. Lakini niende mbele zaidi kwenye kuishauri Wizara, sasa hivi hali ilivyo, namna ambavyo mashtaka yanaendeshwa ya masuala ya ubakaji na ulawiti kwa watoto yanaendeshwa sawasawa na mashtaka ya ubakaji na ulawiti kama ilivyo kwa watu wazima. Sasa hapa pia kuna tatizo lingine kwa sababu Mahakama inatuambia kwamba ushahidi mzuri unatoka kwa yule mtu ambaye amefanyiwa ukatili yeye mwenyewe na hapa tunamzungumzia mtoto mdogo yaani namna anavyotoa ushahidi wake lazima aseme alivyofanyiwa kile kitendo kwa maneno mahsusi yanavyotumika. Na akisema vile ambavyo sivyo ushahidi unapungua thamani yake. Sasa ukiangalia kwa mila zetu na desturi zetu za Kitanzania kwa maadili tuliyokuza nayo watoto wetu yale maneno kutamka ni ngumu sana. Kwa sababu mtoto lazima atamke zile nyenzo za kimwili zilizotumika kumfanyia uhalifu ambazo hata mimi mwenyewe binafsi siwezi kuzitamka. (Makofi)

Sasa nafahamu Mahakama inatumia utashi mara nyingine watoto wakishindwa kusema bado wanatumia utashi walionao kwa ajili ya ku-convict hawa watuhumiwa. Lakini lazima tuiweke kwenye sheria, lazima utaratibu wa kushughulikia matatizo ya ulawiti na ubakaji kwa watoto uwe tofauti kabisa na kifungu cha kushughulikia ubakaji na ulawiti kwa watu wazima kwa sababu watoto kama alivyo mtoto kama yeye mwenyewe hawezi kujipigania. (Makofi)

Kwa hiyo, mimi namshauri Mheshimiwa Waziri akakae na Waziri wa Sheria na Katiba waone namna ya kutofautisha haya mambo. Namwambia yeye kwa sababu yeye ndiyo analinda ustawi wa watoto katika Taifa letu. Kwa hiyo bila kuweka mambo sawa hapa naona kidogo kutakuwa na mushkeli.

Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kushauri kuhusiana na ulinzi wa mtoto, hapa kwa muda mrefu tumeongelea kuhusiana na watoto kubeba mabegi mazito mgongoni na yalishatolewa maelekezo, lakini kinachosikitisha bado watoto wanabeba mizigo mikubwa sana wakienda shuleni na inahatarisha afya zao. (Makofi)

Kwa hiyo, mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu yeye ndio anahusika na ustawi wa mtoto, yeye ndio anamlinda mtoto wa Kitanzania, naomba afanye jambo katika hili. Shule zetu zinaweza zikaweka utaratibu mzuri watoto wasibebeshwe mlima wa madaftari, ma-counter book na mlima wa vitabu migongoni mwao tunaharibu afya ya hawa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala langu la mwisho ni kwenye ulinzi wa afya ya mwanamke. Afya bora ya mwanamke ni uwekezaji kwa Taifa letu kwa sababu mwanamke anatumika kama nyenzo ya maendeleo kwenye mambo mengi sana. Ninachosikitika suala la utoaji wa mimba holela mtaani limeachiwa kupita maelezo. Takwimu zinatuambia wanawake 400,000 kila mwaka wanatoa mimba mitaani na asilimia 70 wanatumia nyenzo ambazo sio za kiafya. Wanatumia nyenzo ambazo sio za madaktari wenye sifa, ni asilimia 30 tu wa mjini ambao watakwenda kwa madaktari wenye sifa. Sasa masuala ya utoaji huu wa mimba inawezekana tusiyaongee sana, lakini wanawake 400,000 kwa mwaka ni wanawake 1,100 kila siku wanatoa mimba kwa njia zisizo salama.

Mheshimiwa Spika, sasa tunaomba ulifanyie kazi hili suala, nafahamu kuna situation ambazo zinaruhusiwa mwanamke aweze kutoa mimba, lakini kuna mambo ambayo tunaweza tukayaboresha. Kuna mazingira magumu ambayo tunaweza tukaboresha ili masuala ya utoaji wa mimba huko mtaani, pasipo kutumia nyenzo sahihi yaweze kupungua na yaweze kuhalalishwa yakafanywa katika hospitali zetu. Kwa mfano, kwa sababu sasa hivi tunaambiwa takwimu karibu wanawake 1,000,000 kila mwaka wanapata mimba zisizotarajiwa, sasa tuone tunaboresha vipi ili wanawake wasikimbilie kule mtaani kwenye nyenzo ambazo sizo na waende wakafanye katika mahali ambapo panastahili kiafya katika suala hilo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)